Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chenga: Tulimteka Nasma Kidogo kimafia

Pichani kulia ni Norbert Chenga muasisi wa muziki wa taarabu majukwaani, hapo awali ulikuwa ukipigwa ndani. Chenga pia ndiyo muasisi wa Kundi la Muungano Cutural Troup lililokuwa na ushindani mkubwa wa miondoko ya muziki wa taarabu kati yake na Kundi la Tanzania One Theatre (TOT). Katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili Tuzo Mapunda anaeleza mbinu walizokuwa wakitumia kuleta ushindani katika muziki huo .

Muktasari:

Nasma hakuanzia kuimba taarabu katika kikundi cha Muungani Cultural Troupe, alianzia Tanzania One Theatre (TOT), ambako alitekwa kimafia kupelekwa Muungano.

Achia ngazi bibi mchuma unaondoka huo...achia ngazi bibi mchuma unaondoka huo...

Hii ni baadhi ya mistari inayopatikana katika wimbo ‘Mtu Mzima Hovyo’, ulioimbwa na marehemu Nasma Khamis Kidogo, alipokuwa na kundi la muziki wa taarabu la Muungano.

Nasma hakuanzia kuimba taarabu katika kikundi cha Muungani Cultural Troupe, alianzia Tanzania One Theatre (TOT), ambako alitekwa kimafia kupelekwa Muungano.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, muasisi na kiongozi wa kikundi cha Muungano, Norbert Chenga anaeleza namna walivyomteka kimafia Nasma na kuwa gumzo mjini lililokoleza ushindani wa muziki wa taarabu kipindi hicho.


Kuchochea ushindani

Chenga anasema kazi ilianza alipoitwa na Makamu wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, iliyokuwa inaongozwa na Rais Benjamin Mkapa, Dk Omar Ali Juma kuombwa mwimbaji mahiri wa kikundi cha Muungano, Khadija Kopa na Othman Soud wahamie TOT, wakasaidie kampeni za CCM.

Anasimulia hiyo ilikuwa mwaka 1997/98 na kwa kuwa asilimia kubwa kwenye bendi hiyo walikuwa wanachama wa CCM, walikubali ombi la kiongozi huyo, hivyo kina Hadija Kopa na Othman Soud waliokuwa mke na mume wakaondoka.

“Baadaye tukagundua TOT wamejaa mastaa karibu wote, wakiwamo Khadija Kopa, Nasma Kidogo, Leila Khatibu na wengine wote wazuri, tukafikiria kuanza kuwaiba wasanii wao tulivizia ilipokaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tulianza kufanya mazungumza na Nasma Kidogo,” anasimulia Chenga huku anacheka kwa nguvu.

Anasimulia kwa kuwa wote wanatoka mkoa mmoja wa Lindi kasoro wilaya na walikuwa wakiitana dada na kaka haikuwa kazi ngumu kumshawishi na kukubali kuhamia Muungano.

“Kwa kuwa nilitaka akihamia isiwe kinyonge nilimueleza ninachotaka kufanya.

“Nilijua akihamia bila kashkash haitaleta maana na atakuja kuishiwa kimuziki, hivyo nikapanga namna ya kulifanya jambo hilo kuwa kubwa lakini kuleta ushindani pia kwa TOT,” anasema Chenga.

Anasimulia kuwa kawaida ilikuwa ikikaribia sikukuu wasanii wanajipanga kwa ajili ya kutoa burudani ya kukata na shoka siku wa sikukuu.

Hivyo Nasma naye alikuwa katika mazoezi makali na bendi yake wakijiandaa kwa ajili ya sikukuu wa Idd, baada ya kukamilika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Nikamwambia aendelee na mazoezi na bendi yake ili isijulikane kama ataondoka, hivyo akawa anafanya huko mchana, saa 2:30 usiku tunakwenda kumchukua na gari na kumpeleka Mabibo - Snake Garden kufanya mazoezi na kumrudisha nyumbani kwake saa 7 za usiku.

“Hii ilikuwa inafanyika kwa usiri mkubwa hakuna mtu aliyekuwa anajua tulikuwa tunamfungia kwenye chumba cha hoteli anajifundisha nyimbo za kutoka nazo,” anasema.


Nasma aanikwa saa chache kabla ya shoo

Norbert anasema wakati umafia huo unaendelea walikuwa wamelipia nusu ukurasa katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo ikiwa inakaribia kumalizika mfungo ili iingie Sikukuu ya Idd.

“Tulitoa tangazo la shoo kabambe wakati wa Sikukuu ya Idd na ujio wa wasanii wapya, katika tangazo kulikuwa kunaonekana miguu, kila siku linapanda kuelekea kichwani kwa muda wa siku saba

“Misikiti ilipoanza kupiga takbira kuashiria mwezi umeandama na kesho ni Sikukuu ya Idd, nilikimbilia Redio Tanzania kuwaambia wapige matangazo 20 niliyolipia mfululizo na waeleze wazi anayehamia Muungano na Nasma, vivyo hivyo katika magazeti nako niliwaeleza wafunue na msanii anayehamia aonekane,” anasema.

Chenga anasema wakati matangazo yanachezwa redioni ili kuhofia kuhujumiwa siku ya tukio tulimchukua Nasma na kumpeleka Kigamboni na kumnyang’anya simu na ilikuwa kila wakimpigia hapatikani,” anasimulia.

Anasema alijua viongozi wa TOT wangempata kwenye simu wangemshawishi kwa namna yoyote ile abaki au na wao wangemficha.

“Kama tulivyobashiri, kwani viongozi wa TOT wa wakati huo walikwenda kumtafuta Nasma nyumbani kwake walipofika walimkuta mfanyakazi walipomuuliza aliwajibu hajui alikokwenda, ingawa alipanda kwenye gari.

Anasema siku ya tukio walikodi gari kubwa lililokuwa likitoa matangazo kuhusu shoo hiyo.

“Kikubwa zaidi tulikwenda kutangaza kwa fujo kwenye makao makuu ya TOT, pale Mwinjuma Mwananyamala, ambapo pia tuliweka tambara kubwa kuitangaza shoo hiyo, hakika ulikuwa ni ushindi mkubwa,” anasema.


Chenga ashonesha nguo za Nasma Unguja

“Walimtafuta kila kona wakabaki wanatoa vitisho kuwa hajafanya mazoezi hivyo ataimba nyimbo zao na hana nguo kali za kuvaa ukumbini, hivyo atavaa nguo zao.

“Wakadhamiria akiimba nyimbo zao ukumbini wamkamate na akivaa nguo zao wamvue, kumbe walikuwa hawajui kama ule mchezo nimeucheza kiakili sana, mazezi alikuwa anafanya na nilichukua vipimo vya nguo kwa maelekezo ya fundi nikavituma Unguja ambako nguo ilishonwa na ikatumwa kwa boti nikaenda kuipokea mwenyewe na alipoijaribu ilimkaa vema,” anasema Chenga huku akicheka kwa kusikitika pamoja jinsi alivyopanga hilo jambo kwa akili na umakini mkubwa.

Komba avamia ukumbini Anasimulia siku ya tukio marehemu Kapteni John Komba aliyekuwa kiongozi wa TOT na wenzake saba walitoka Kinondoni Ukumbi wa Vijana na kwenda kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese Argentina ambako Muungano walikuwa wanafanya onyesho kubwa na kumpokea Nasma Kidogo.

“Saa 9:30 siku hiyo tulianza programu ya kupiga ngoma na vibwagizo wakati huo Kapteni Komba akiwa ukumbini amefungua vishikizo vya shati cha kwanza mpaka cha tatu amekaa kwenye kiti anatweta huku akiwa haamini kinachoendelea.”

“Muda wote ananiambia, Chenga kama hii ni kweli basi utakuwa umefanya kazi kubwa sana…. Wakati huo tumemjaza Nasma maneno ya uongo kwamba akirejea tena TOT watamroga na kumuua kabisa ….Nasma alamini na kuniambia kaka ni kweli hata tunamopita kuimba mimi naimba wimbo mmoja tu wakati zamani nilikuwa naimba mbili hadi tatu katika shoo nzima,” anasimulia Chenga na kuongeza;

“Tukamuambia na unakoendelea hautaimba kabisa tulimjaza hadi ilifikia hatua akaichukia sana TOT, tulijua hakuna ukweli tulifanya hivyo ili asirubuniwe na kutusaliti.”

Chenga anasimulia licha ya Kapteni Komba kuwasili kwenye ukumbi huo walikuwa bado hawaamini kama kweli umafia huo wa kumuiba Nasma umefanikiwa, lakini mwishowe wakati ulipowadia walianza kusikia sauti kwa kuwa alianza kuimba kutokea nje akiwa na maiki ya wireless.

“Kitendo cha kuingia kwenye ule ukumbi Komba na wenzake walipigwa na butwaa, huku wakitufuata viongozi wa Muungano kutupongeza kwa kazi nzuri tuliyofanya kumuiba msanii mkubwa kama Nasma na kumfanyisha mazoezi pasipo wao kujua,” anasema.


Komba atunza bia na pesa Anasimulia siku hiyo Nasma alivaa nguo mpya alizoshonewa Unguja na aliimba wimbo mpya kabisa uitwao ‘Umelichuna buzi umeshindwa kulila,” wakati anaimba na kucheza kwenye ukumbi huo Kapteni Komba alishindwa kujizuia na kujikuta ameinuka na kwenda kumtunza Sh60,000 msanii huyo.

“Mpeni kreti moja ya bia Chenga ametumia akili sana kumpata Nasma bila timu yangu kujua, umefanya kazi kubwa sana,” anasema Chenga.

Anasema walimpa Nasma dau la Sh2 milioni kumuhamishia Muungano ilhali kina Hadija Kopa walipokwenda TOT kutoka Muungano walipewa Sh3 milioni kila mmoja.

TOT walianza

Chenga anasema kabla hawajamuiba Nasma, TOT walimchukua Ali Star akiwa jukwaani.

“Alikuwa ameimba beti mbili za wimbo akaweka kipaza sauti chini na kuhamia jukwaa la TOT na kushika maiki nyingine na watu wa TOT walikuwa wanashangilia na kule alikuwa anaimba wimbo mpya ndio maana nikaumiza kichwa kufuta aibu hii kwa kumbeba Nasma kimafia,” anasema huku anacheka na kugonga meza.