Sanamu la Mwalimu Nyerere kujengwa makao makuu AU

Dar es Salaam. Waziri Bashungwa ataka wachongaji kuchangamkia tenda ya kutengeneza sanamu la Mwalimu Nyerere litakaliwekwa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) yaliyopo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Wazo la kutengezwa kwa sanamu hiyo, kulitolewa na aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, hayati Robert Mugabe katika kikao cha SADC kilichofanyika Harare mwaka 2015 ambapo yeye alikuwa Mwenyekiti.
Kampuni itakayoshinda zabuni hiyo, itapatiwa zaidi ya Sh700 milioni fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao unapaswa kutekelezwa katika mwaka 2021/2022, huku moja ya kigezo cha atakayeshinda awe amewahi kufanya kazi hiyo.
Akizungumzia jambo hilo leo Jumatatu Machi 13, 2021 na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, alipokutana na wasanii wa uchongaji na uchoraji.
Bashungwa alizungumzia tenda hiyo ambapo alieleza sanamu hilo linapaswa kutengenezwa kwa madini hayo ya shaba nyeusi.
HGata hivyo Waziri Bashungwa alisema licha ya Tanzania kupewa kipaumbele katika tenda hiyohakuna kampuni ya kitanzania iliyojitokeza na hii ni kutokana na nchi hiyo kuwa na mchango mkubwa katika ukombozi kwa nchi za Afrika na kazi alizifanya baba wa Taifa katika kulikomboa bara hilo.
“Pamoja na upendeleo huo wa Tanzania kupewa kipaumbele, hakuna hata kampuni moja iliyojitokeza yenye sifa ya kufanya kazi hiyo na taarifa nilizonazo ni kwamb watarudia tena kutangaza zabuni hiyo mwaka huu, hivyo nawaomba wasanii itakapofika muda mfanye hivyo,”alisema Waziri huyo.
Hata hivyo katika hili alisema wasanii hao wanapaswa kuelewa kwamba kazi hiyo sio lazima aifanya mtu mmoja na badala yake wanaweza kuungana kushirikisha maarifa hayo na kazi ikafanyika vizuri.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema kuhusu malalamiko ya kukosa soko la bidhaa wanazozotengeneza wachoraji na wachongaji, ipo haja ya Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) na Chama cha Haki Miliki (Cosota), kutoa mafunzo ya namna wasanii hao sasa wataweza kufanya biashara hiyo kwa njia ya mtandao kutokana na dunia sasa kubadilika katika kufanya biashara.
“Yale mambo mliyozoea ya kusafirisha vinyago au michoro mpaka mtu asafiri kumfikia mteja yamepitwa na wakati, Cosota, Basata tafuteni namna ya kuwapa mafunzo wasanii wetu hawa kutumia mitandao kufanya biashara ikiwemo hata kuanzisha minada ya mitandaoni,”.
Awali wasanii hao wakiwakilishwa na Katibu wao kwa upande wa chama cha wachongaji (Chawasawata), aliyejitambulisha kwa jina la Mwintanga Ramadhani, alisema baada ya kutokea janga la corona hali ya biashara yao imekuwa mbaya ukizingatia kuwa wateja wakubwa wa kazi zao ni mataifa ya nje.
“Watanzania bado hawana utamaduni wa kununua bidhaa zetu, na hivyo soko kubwa tunalolitegemea ni nchi za nje, lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, biashara imeyumba kwa kiasi kikubwa,” amesema Ramadhani.
Wakati kwa upande wake Katibu wa Chama cha ushirika cha wachoraji maarufu Tingatinga, Ramadhani Mangula, alisema licha ya sanaa hiizo kutopewa kipaumbele hapa nchini kama zilivyo za muziki na nyingine, ukweli ni kwamba ndizo zinaongoza katika kuliingizia pato taifa na kueleza ni wakati sasa wa kuwawezesha wasanii kufanya kazi zao kisasa ili kuendana na teknolojia na kushindana na matifa mengine yanayofanya kazi hiyo.