Kofia ya Yemi Alade yahamia kwa Zuchu

Muktasari:
- Mnamo Aprili 8, 2020 ndipo Zuchu alitambulishwa akiwa ni msanii wa saba na wa pili wa kike baada ya Queen Darleen, mwanamuziki aliyeibuka kufuatia kushirikishwa na Dully Sykes katika wimbo wake, Historia ya Kweli (2002).
Dar es Salaam. Mwanamuziki Zuchu ametimiza miaka mitano tangu alipotambulishwa katika rekodi lebo ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambayo imetengeneza majina ya mastaa wakubwa ndani ya Bongofleva tangu 2015.
Mnamo Aprili 8, 2020 ndipo Zuchu alitambulishwa akiwa ni msanii wa saba na wa pili wa kike baada ya Queen Darleen, mwanamuziki aliyeibuka kufuatia kushirikishwa na Dully Sykes katika wimbo wake, Historia ya Kweli (2002).

Kabla ya Zuchu, lebo hiyo ilishawasaini Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava na Mbosso aliyeunda kundi la Yamoto Band akiwa na wenzake watatu, Enock Bella, Beka Flavour na Aslay.
Miaka mitano chini ya WCB Wasafi, Zuchu amefanya mengi katika muziki wake akitengeneza mashabiki wengi pamoja na fursa za kiuchumi zinazotokana na ukuaji wa chapa yake. Na hizi ni rekodi 10 alizoziandika ndani ya kipindi hicho.
1. Tuzo saba za TMA
Baada ya kurejea Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) msimu wa 2021 tangu ziliposimama 2015, Zuchu ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi licha ya kutoshiriki katika msimu wa kwanza ila hiyo miwili ya mwisho kufanya kweli akishinda tuzo saba kwa ujumla.
Tangu msimu wa 2021, wanaomfutia Zuchu kushinda tuzo nyingi za TMA ni Alikiba (6), Harmonize (6), Diamond (5), Nandy (4), Young Lunya (4), Marioo (4) na Phina (4) ambaye ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018 akitokea Mwanza.
2. EP yake tishio
Hadi sasa EP yake, I Am Zuchu (2020) ndio EP pekee ya msanii wa kike Bongo iliyofanya vizuri zaidi ikisikilizwa mara milioni 34.5, pia ilikaa tano bora kwenye chati za Boomplay Album kwa wiki 75, huku ukishika namba moja kwa wiki 35 mfululizo!.

3. Namba moja Afrika
Desemba 2021, video ya wimbo wake, Sukari (2021) iliandika rekodi kama video ya muziki iliyotazamwa zaidi YouTube Afrika mwaka huo ikitazamwa zaidi ya mara milioni 60, huku ikifuatiwa na ile ya Wizkid ft. Tems, Essence (2021) iliyotazamwa mara milioni 53.
Hata hivyo, mwaka uliofuatia Zuchu alishindwa kuifikia rekodi hiyo mbele ya Rema wa Nigeria ambaye video ya wimbo wake, Calm Down (2022) ilitazamwa zaidi ya mara milioni 300 na kuongoza Afrika ikifuatiwa na remix yake ambayo sasa imefikia bilioni 1.
4. Wiki 100 katika chati
Zuchu anayefanya vizuri na albamu yake, Peace and Money (2024), pindi alipotambulishwa na WCB Wasafi kupitia EP, I Am Zuchu (2020), alikaa katika chati za YouTube Music Tanzania kwa wiki zaidi ya 100 na ndiye msanii pekee wa kike Bongo aliyefanya hivyo.
5. Sukari yake tishio
Video ya wimbo wa Zuchu, Sukari (2021) ndio ya kwanza kutoka kwa msanii solo Tanzania na Afrika Mashariki kwa kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikifanya hivyo Machi 2024, kisha ikafuata Jeje (2020) yake Diamond hapo Agosti 2024.
Kabla ya hapo, video za nyimbo zote zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ni zile ambazo walishirikiana wasanii kuanzisha wawili, nazo ni Yope Remix (2019), Inama (2019) na Waah! (2020) zake Diamond, na Kwangwaru (2018) yake Harmonize.
6.Tuzo tano kwa mpigo
Tangu kurejea tena TMA, Zuchu ndiye msanii wa kike aliyeshinda tuzo nyingi kwa usiku mmoja, msimu wa 2022 alishinda tuzo tano ikiwa ni sawa na 20 Percent 2011 na Alikiba 2015 & 2021, na wote hawa wanaifukuzia rekodi ya Diamond aliyeshinda tuzo saba 2014.
7. Namba moja Boomplay
Hadi sasa Zuchu ndiye msanii wa kike Tanzania aliyesikilizwa (most streamed) zaidi katika mtandao wa Boomplay Music, tayari nyimbo zake zimesikilizwa zaidi ya mara milioni 382 huku akipata wafuasi 146,000 katika jukwaa hilo.
Kwa ujumla Zuchu anashika nafasi ya pili kwa kusikilizwa zaidi Boomplay nyuma ya Diamond, kisha nafasi ya tatu ni Rayvanny, Jay Melody, Mbosso, Marioo, Alikiba, Nandy na Jux, mshindi wa Trace Awards 2025 kama Msanii Bora wa Kiume.
8. Namba moja YouTube Afrika
Kwa sasa Zuchu ndiye msanii namba moja wa kike Afrika kuwa na wafuasi (subscribers) wengi YouTube akiwa nao milioni 3.85 akiwa anafuatiwa na Yemi Alade kutokea Nigeria mwenye milioni 2.46 ingawa ndiye alitangulia kujiunga na mtandao huo kabla ya Zuchu.
9. Anauza zaidi YouTube
Licha ya kuwakuta wakali kibao katika tasnia, Zuchu kwa sasa ndiye msanii wa kike aliyetazamwa zaidi (most viewed) YouTube kwa muda wote, maudhui yake ambayo analipwa na jukwaa hilo linalomilikiwa na Google, yameshatazamwa zaidi ya mara milioni 827.3.
Kwa ujumla Zuchu anashika nafasi ya nne Afrika Mashariki nyuma ya Harmonize ( bilioni 1.22), Ravanny (bilioni 1.25) na Diamond (bilioni 2.92) ambaye ni namba mbili Afrika kwa kutazamwa zaidi YouTube nyuma ya Burna Boy (bilioni 3.24) kutokea Nigeria.
10. Tuzo mbili za AFRIMMA
Tayari Zuchu ameshinda tuzo mbili za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kutoka Marekani ikiwa ni sawa na Nandy 2017 & 2020, ikumbukwe Zuchu ameshinda AFRIMMA kama Msanii Bora Chupukizi 2022 na Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2022.