Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar kuanza uwindaji wa kitalii

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma (kushoto) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Michael Mantheaks Safari Ltd, Michael Mantheaks wakisaini hati ya makubaliano kufanya uwindaji wa wanyamapori katika misitu ya Mkoa wa Kusini Unguja

Muktasari:

  • Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeingia makubaliano kuwezesha uwindaji wa kitalii wa wanyamapori katika maeneo ya Msitu wa Kijamii Mtende, eneo la Kunguwi na Kirijo Nongwe, yaliyopo Muyuni mkoani Kusini Unguja.

Unguja. Katika kuendeleza misitu na kukuza utalii, Zanzibar imepiga hatua nyingine baada ya kusaini makubaliano ya kufanya uwindaji wa kitalii wa wanyamapori.

Miongoni mwa wanyama watakaowindwa ni jamii yote ya paa, kima mweusi na ndege aina ya kanga, jambo ambalo halikufanyika awali, hivyo kusababisha uharibifu na uvamizi.

Akizungumza wakati wa kusaini makubalinao hayo leo Machi 28, 2025 Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma amesema ni dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhamasisha jamii kutunza na kuhifadhi rasilimali za misitu.

Makubaliano ya miaka mitano yameingiwa kati ya Wizara ya Kilimo na mwekezaji kutoka kampuni ya Michel Mantheakis Safari Ltd.

Mbali ya kuendeleza misitu na kukuza utalii, kampuni hiyo pia itaboresha kipato cha jamii.

Ali amesema makubaliano hayo yanahusisha kufanya uwindaji wa kitalii wa wanyamapori katika maeneo ya Msitu wa Kijamii Mtende, eneo la Kunguwi na Kirijo Nongwe, yaliyopo Muyuni mkoani Kusini Unguja.

“Hii ni hatua kubwa kuwa na uwindaji wa kitalii ambao kwa Zanzibar hatukuwa nao. Kwa hiyo mbali na kuongeza mapato, itaongeza ufanisi katika utunzaji wa mazingira na misitu kwa ujumla,” amesema.

Amesema mkataba huo utasaidia kuongeza nguvu kwa wizara na jamii katika kuhakikisha misitu inaendelea kutunzwa na kulindwa kwa manufaa ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, amesema uhifadhi wa misitu hauwezi kufanikiwa iwapo hakuna ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo husika.

Mwekezaji, Michael Mantheakis amesema mkataba huo utasaidia kuleta nguvu na ushirikiano katika kuendeleza shughuli za uwindaji wa kitalii wa wanyamapori, ambao utachangia uhifadhi wa misitu na maendeleo ya jamii.

Mwananchi kutoka Kamati ya Uhifadhi Muyuni C, Salum Rashid Juma, ameishukuru Serikali kwa kutoa mamlaka kwa wananchi kusimamia na kuhifadhi misitu.

Amesema uamuzi huo ni hatua muhimu inayowapa wananchi nguvu na umoja katika kulinda rasilimali za misitu, jambo ambalo litafaidisha vizazi vya sasa na vijavyo.