Wengine watatu warejesha fomu ZEC
Mtiania urais wa Zanzibar kupitia chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir akikabidhi fomu za kuomba uteuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibr (ZEC), Jaji George Joseph Kazi katika ofisi za Tume hiyo Maisara Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Kesho Septemba 10, 2025 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za kuomba uteuzi,vyama 17 vilichukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea urais
Unguja. Watiania watatu wa kiti cha urais wamerejesha fomu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya kukamilisha masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria, ikiwamo kupata wadhamini 1,000 kutoka mikoa mitano iliyopo Unguja na Pemba.
Idadi hiyo inafanya jumla ya vyama vinne kurejesha fomu za kuomba uteuzi kati ya 17 vilivyochukua fomu hizo vikitanguliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mgombea wa CCM katika nafasi hiyo, Dk Hussein Mwinyi, ambaye ni Rais anayemaliza muda wake alirejesha fomu Septemba 6, 2025.
Mtiania urais wa Zanzibar kupitia chama Cha UPDP, Hamad Mohamed Ibrahim (kushoto), akikabidhi fomu za kuomba uteuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Maisara Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Kwa mujibu wa ratiba ya ZEC, kesho Septemba 10, 2025 saa 10:00 jioni ni mwisho wa kurejesha fomu.
Waliorejesha fomu leo Septemba 9, 2025 ni mtiania ya urais kupitia Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir; wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib na mgombea wa UPDP, Hamad Mohamed Ibrahim.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kurejesha fomu, watia nia hao wamesema kushirikishwa vyama vyao kunaonesha wazi kwamba, demokrasia inaendelea kukua.
Wameeleza mazingira mazuri yaliyowekwa na ZEC kwa wagombea hao ni kwa mustakabali wa siasa za Zanzibar na demokrasia nchini.
Ameir Hassan Ameir, kutoka Chama cha Makini ameahidi kuvaa viatu vya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kwa kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.
"Nitawafuata wananchi walipo iwe kwa kutumia gari, mguu, baiskeli, bodaboda au vyovyote vile ilimradi nitimize azma ya kuwafikia wananchi waweze kusikiliza sera za Chama cha Makini, kwani ni sera za matumaini za kuwakomboa wananchi walipo na kwenda katika maisha bora ya kila Mzanzibari watakaponipa ridhaa," amesema.
Amewataka Wazanzibari kukaa tayari kusikiliza sera katika mikutano yake na kuandaa kampeni za kupita kila maeneo ya vijana wa bodaboda, sokoni na mengine kwa lengo la kuzungumza na wananchi, akilenga wampigie kura siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Amewaomba Wazanzibari kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake, mtiania nafasi ya urais kutoka Ada Tadea, Juma Ali Khatib amesema chama hicho kinaendelea kusimamia msimamo wake wa kuitaka nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
"Tunaamini katika uwazi na demokrasia iliyopo, tuna matumaini ya chama chetu kupata kura nyingi za kutosha na kupata nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais na kushirikiana na Serikali itakayoongozwa na Dk Hussein Mwinyi, kwa sababu sote tukishaingia katika chombo cha kutunga sheria na Serikali tunatekeleza ilani ya CCM hata kama una ilani ya chama chako unaiweka mfukoni," amesema.
Mtiania urais wa Zanzibar kupitia chama Cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib (kushoto), akimkabidhi fomu za kuomba uteuzi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi katika ofisi za Tume hiyo Maisara Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Ameahidi watahakikisha wakati ukifika wananadi ilani na sera za chama chao na kuishauri Serikali ili mipango ya chama hicho iweze kusaidia kuwatumikia Wazanzibari.
Naye mgombea wa UPDP, Hamad Mohammed Ibrahim, ameviomba vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu na kunadi sera za vyama vyao ili uchaguzi ufanyike kwa amani na usalama.
Amesema hivi sasa siasa za uchochezi na mifarakano hazina nafasi, kwani wananchi wa Zanzibar wanataka maendeleo na siyo jambo lingine.