Watu 12,000 wahofiwa kuugua himofilia

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (katikati), akika utepe kuashiria uzinduzi wa kliniki ya himofilia, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Himofilia Duniani katika hafla iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Ijitimai, Visiwani Zanzibar, jana. Pamoja naye ni wawakilishi kutoka Chama cha Himofilia Tanzania (HST), Taasisi ya himofilia ya novo nordisk, Wizara za afya kutoka Tanzania na Zanzibar, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chama cha Himofilia Duniani na wadau wengine.
Muktasari:
- Licha ya idadi kubwa ya Watanzania kudaiwa kuwa na ugonjwa wa himofilia ni 451 pekee ndio waliopimwa na kugundulika na tatizo hilo.
Zanzibar. Kati ya watu 6,000 hadi 12,000, wanahofiwa kuugua ugonjwa wa himofilia nchini huku idadi ya waliogundulika kuwa na ugonjwa huo ni 451 pekee, hadi sasa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, kati ya watu 10, mmoja anadaiwa kuugua ugonjwa huo, huku asilimia 97 ya wagonjwa hawajagundulika.
Mazrui ameyasema hayo hivi karibuni katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya himofilia duniani iliyofanyika pamoja na uzinduzi wa kliniki ya ugonjwa huo katika Hospitali ya Wilaya ya Ijitimai, visiwani humo.
“Kama tunavyofahamu himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda unaosababishwa na ukosefu wa kiwango cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu, hivyo kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu mtu anapopata jeraha,” amesema.
Amesema mwaka 2020 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikishirikiana na Taasisi ya himofilia ya Novo Nordisk ilianzisha mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu.
Sababu ya hatua hiyo, amesema ni kuiunga mkono Serikali kupunguza madhara ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo himofilia na selimundu.
Amesema wanacholenga zaidi katika mradi huo ni kuwezesha upatikanaji wa vipimo vya wagonjwa wa damu, selimundu na himofilia katika hospitali za rufaa nchini sambamba na kuanzisha kliniki za magonjwa hayo, mafunzo na kupatikana wataalamu waliobobea.
“Katika maadhimisho haya nina furaha kuwaambia kuwa mradi huu katika kuanzia kipindi cha kwanza hadi kipindi cha pili tayari umefanikisha ukarabati wa kliniki za himofilia katika hospitali 13 zikiwemo hospitali za Muhimbili, KCMC, mbeya na Bugando,” amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha himofilia Tanzania (HST), Dk Stella Rwezaura amesema asilimia 70 ya wagonjwa wanarithi na inabebwa katika kinasaba cha kike.
“Mwanamke ana ‘x’ mbili na mwanaume ana ‘xy’, endapo mwanamke ana ‘x’ yenye vinasaba vya himofilia, asilimia 50 ya watoto wake wa kiume watakuwa na tatizo hilo, hivyo kufanya asilimia 99 ya wagonjwa wa himofilia kuwa wanaume,” amesema.
Amesisitiza lengo lao ni kuwatambua wagonjwa wengi zaidi ili wapatiwe huduma, hivyo kwa msaada wa wafadhili, vyama vya wagonjwa na Serikali na wadau wengine, huduma zinafika karibu kwa wananchi.
Mmoja wa wagonjwa wa ugonjwa huo ambaye pia anauguza watoto wawili wenye ugonjwa huo, Regina Shirima amesema anakabiliwa na changamoto ya hali duni ya kiuchumi baada ya kutumia muda mwingi kuhudumia watoto.
“Changamoto nyingine ni kwa watoto wenyewe hawapati muda wa kusoma, kucheza na wenzao ama kuwa na furaha kwani muda mwingi wanakuwa wagonjwa,” amesema.
Ametoa wito kwa jamii kuondokana na mitazamo kuwa, wanawake ndio chanzo cha watoto kuzaliwa kwa ugonjwa huo kwa kuwa mtoto hapatikani bila baba.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya HST, Dk Lawrence Museru amesema wagonjwa wengi wametambulika baada ya kupoteza maisha.
“Wagonjwa wamekuja kutambulika baada ya kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu kwa sababu ugonjwa huo haukutambulika,” amesema.
Amesema matibabu ya ugonjwa huo ni ghali kiasi kwamba, Serikali pekee haiwezi lazima uwepo ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali.