Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wa usafiri kujadili fursa mpya za biashara, uchumi

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohammed akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la  Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha Afrika Mashariki na Kati (Fiate Rame) unaotarajia kufanyika Aprili 30 na Mei mosi mwaka huu Mjini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan atafungua Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha

Unguja. Watunga sera na wataalamu wa usafiri na usafirishaji kutoka mabara manne wanakutana Zanzibar katika Mkutano wa Kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha Afrika Mashariki na Kati (Fiata Rame) kujadili fursa na changamoto za sekta hiyo.

Wataalamu wengine watakaoshiriki ni wa uwezeshaji biashara, mamlaka za udhibiti, mamlaka za bandari, wasafirishaji mizigo, watafiti na wabunifu wa sekta kutoka mabara ya Asia, Ulaya na Afrika.

Mkutano huo utakaofanyika Aprili 30 hadi Mei mosi mwaka huu kisiwani Zanzibar, unatarajiwa kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 25, 2025, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salim Mohammed amesema mkutano huo utajadili masuala ya urahisishaji biashara, ufadhili, bima, teknolojia na uboreshaji wa taaluma ndani ya tasnia ya usafiri na usafirishaji.

"Washiriki watapata nafasi ya kufahamu fursa zinazotokana na Mpango wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na mchango wa tasnia ya usafiri na usafirishaji katika kusaidia ukuaji wa uchumi endelevu barani Afrika, Mashariki ya Kati na ulimwenguni," amesema.

Ametoa rai kwa wadau wa sekta ya uchukuzi kutoka Tanzania na Zanzibar kutumia fursa hiyo kwa kushiriki kwenye mkutano huo muhimu, kwani wataongeza ujuzi na kubaini fursa mpya zinazopatikana, ikiwa ni pamoja na kuongeza ujuzi.

Pamoja na mambo mengine, malengo mahususi ya mkutano huo ni kuchunguza mageuzi ya kidijitali, teknolojia mpya na suluhisho za ubunifu katika sekta ya vifaa ili kupunguza athari za kimazingira.

Pia, Waziri Khalid amesema kupitia mkusanyiko huo, utaimarisha ujuzi na ushindani katika sekta ya vifaa na usafirishaji, kukuza mazingira ya kisheria yanayounga mkono sekta bora na endelevu ya vifaa, na kutoa jukwaa la washiriki kuungana na wateja, wawekezaji na washirika wapya.

Mbali na malengo hayo, pia mkutano huo utakuwa na mambo mengine tofauti, ikiwemo maonesho na majadiliano ya wataalamu, vikao vya biashara kati ya kampuni na biashara za Serikali, maonesho ya bidhaa na huduma, na safari za utalii.

Rais wa Chama cha Wakala wa Ushuru na Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio amesema kuleta mkutano huo ni kuheshimu nia ya Serikali katika kukuza uwekezaji, hususani katika sekta ya buluu.

"Usafiri na usafirishaji umeendelea kuwa uti wa mgongo katika biashara na uchumi. Kupitia mkutano huu, zitazungumzwa fursa, changamoto na suluhisho, kwa hiyo utakuwa na tija kubwa sana," amesema.

Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Ushuru na Forodha Zanzibar (ZFB), Omar Said Mussa amesema fursa hizo ni kubwa siyo tu kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta hiyo, bali kwa taifa kwa ujumla.

"Kampuni zetu zitajenga uimara. Kwa takribani miaka 12 sisi tumekuwa tukitoka kwenda nje ya nchi zingine. Sasa fursa hii imekuja nchini, kwa hiyo hata washiriki wengi watapata fursa hiyo na kuifungua nchi yetu," amesema.