Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakazi Bonde la Serenge wadai kuchapwa na wasiojulikana

Unguja. Wananchi wa Kijiji Muwanda katika Bonde la Serenge, Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja wamelalamika kuwapo kikundi cha watu wasiojulikana walichodai kinawacharaza viboko bila sababu na kisha kutokomea kusikojulikana.

Wametoa madai hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohammed Mahmoud alipofika kusikiliza kero zao.

Vuai Said, mkazi wa kijiji hicho alisema kumeibuka watu ambao hawajulikani wanatoka wapi, lakini wamekuwa wakiwacharaza wananchi viboko na kusababisha taharuki kwenye jamii.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuna watu huwa wanatuchapa viboko bila sababu za msingi kisha wanatokomea, wakishafanya hivyo wanakimbia kusikojulikana,” alisema mkazi mwingine, Iddi Sultan.

Mkuu wa mkoa huo, Ayoub aliagiza Jeshi la Polisi la Mkoa huo kulifuatilia kwa umakini tatizo la kupigwa kwa wananchi wa kijiji hicho, jambo ambalo alisema linawakosesha amani ya kuishi.

Alisema, kitendo cha watu wasiojulikana kuwapiga wananchi wasiokuwa na hatia kinasababisha kuvunjika kwa amani katika shehia hizo.

Akizungumzia hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi, Mussa Hassan Kombo, alisema ni vyema wananchi waendelee kushirikiana na jeshi hilo, kwani mwarobaini wa kuzuia vitendo hivyo ni kuanzisha vikundi shirikishi na kufanya doria katika shehia zao.

Aliwasisitiza wananchi kuwa na utaratibu wa kwenda kuripoti katika vituo vya polisi na kutoa ushahidi wakati wa kesi, ili hatua ziweze kuchukuliwa na kupatikana kwa wahalifu wanaoingia katika shehia zao.

“Nawaombeni sana mwende mahakamani mkatoe ushahidi kuhusiana na kesi hizo,” alisema.

Kuhusu eneo la bonde la kilimo linalojulikana kwa jina la Serenge, mkuu wa mkoa alisema asili yake ni bonde lililotengwa kwa kilimo na si makazi ya watu, hivyo aliwataka wananchi waliokuwepo katika bonde hilo kulitumia kulingana na makusudio.

Alisema chanzo cha kuwepo matukio ya wananchi kupigwa ni kuwepo kwa watu wanaokiuka tamaduni, kunywa pombe na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, alisema hakuna mazingira mabaya katika sehemu hiyo na kuwa Serikali itafanya tathmini na endapo itajiridhisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa watu hao, watatakiwa kila mmoja kurudi katika kijiji cha jirani ili kubaki salama.