Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara wa dagaa waiangukia Serikali

Mkuu wa Kambi ya Fungu Refu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Abdulrahman Mohammed Bakar akianika dagaa katika eneo hilo.

Muktasari:

  • Zanzibar ina jumla ya wafanyabiashara wa dagaa wapatao 16,000, ambapo 14,000 wanapatikana Unguja na 2,000 wako Pemba.

Unguja. Wafanyabiashara wa dagaa kisiwani hapa wameiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwapatia vifaa maalumu vya kuanikia, ili kuhakikisha bidhaa hiyo inakuwa na ubora unaokidhi viwango vya soko.

Wakizungumza leo Aprili 24, 2025 na Mwananchi Digital katika eneo la Fungu Refu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wamesema takriban wajasiriamali 3,000 huendesha shughuli za uanikaji wa dagaa katika eneo.

Abdulrahman Mohammed Bakar, Mkuu wa eneo hilo, akizungumzia adha wanazokumbana nazo, amesema mvua na upepo mkali ni kikwazo kikubwa kwao kwa sababu hutumia maturubali kuanikia dagaa ardhini, jambo ambalo linaathiri ubora wa bidhaa hiyo.

"Wajasiriamali wanapoweka dagaa kwenye maturubali ardhini, bidhaa huathiriwa na mchanga hasa wakati wa upepo mkali, na hilo hupunguza ubora wa dagaa,” amesema kiongozi huyo.

Hivyo, ameiomba Serikali kuwasaidia vifaa vya kisasa vya kuanikia na kukaushia dagaa, ikiwamo matumizi ya sola, ili kuhimili mazingira ya mvua.

Kwa mujibu wake, wakati wa jua kali, inachukua saa tatu hadi tano kukausha dagaa, lakini wakati wa mvua, huchukua hadi siku tatu mpaka nne, hali inayosababisha bidhaa kupoteza ubora au hata kuharibika.

Changamoto nyingine aliyoitaja ni ukosefu wa soko la uhakika na bei za chini zinazowekwa na wanunuzi wa kigeni, hasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Wanunuzi kutoka DRC hutupangia bei baada ya kutuwezesha mtaji wa kuchakata dagaa, lakini mwisho wa siku wanalipa bei wanayotaka wao. Hii hutufanya tushindwe kupata faida,” aliongeza.

Abdulrahman pia alitoa rai kwa Serikali kuweka bei elekezi au kununua bidhaa hiyo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kuwasaidia kiuchumi.

Halima Mansour, mfanyabiashara wa dagaa, amesema ni muhimu Serikali kulipa uzito suala hilo kwa sababu eneo hilo limewatoa vijana wengi kwenye shughuli zisizofaa na kuwapa ajira halali.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini Zanzibar, Dk Salum Soud Hamed alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa Serikali iko katika hatua ya kuzitatua.

“Tumeanza na maeneo ya Kama na Ndagoni ambapo tumejenga viwanda vya kuchakata dagaa na kuwapatia chanja za kuanikia pamoja na miundombinu ya kukaushia bidhaa kipindi cha mvua,” amesema Dk Salum.

Aidha, amebainisha kuwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2025/2026, Serikali imepanga kujenga kiwanda cha kuchakata dagaa katika eneo hilo, sambamba na utoaji wa vifaa vya kuanikia kwa wajasiriamali.

Dk Salum amesisitiza jitihada hizo zina lengo la kuboresha ubora wa bidhaa, kuongeza tija kwa wajasiriamali, na kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.