Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vituo 10 vya bunifu kujengwa kwa gharama ya Sh15 bilioni

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Habiba Hassan Omar (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Tanzania, Dk Nkundwe Mwasaga wakionesha hati ya baada ya kusaini makubaliano ya kujenga kituo cha kukuza ubunifu Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Kati ya vituo 10 vya bunifu vitakavyokengwa, vinane vitakuwa ni vya kukuza ujasiriamali wa kutengeneza mifumo na viwili vitakuwa vinatumika kutengeneza vifaa.

Unguja. Katika kukuza na kuwaendeleza wabunifu wa kidijitali na wajasirimali, vinajengwa vituo 10 vya bunifu nchini vitakavyogharimu Sh15 bilioni.

Kati ya hivyo, vinane vitakuwa ni vya kukuza ujasiriamali wa kutengeneza mifumo na viwili vitakuwa vinatumika kutengeneza vifaa.

Vituo hivyo vinavyojengwa katika mikoa minane, mifumo yake itaunganishwa ili fursa zinazopatikana nchini, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) vijana watakaokuwa kwenye vituo hivyo waweze kuzifanya kwa pamoja.

Hayo yamebainika katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya kuanzisha kituo cha kukuza bunifu za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) eneo la Bwefum, Zanzibar kati ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar na Tume ya Tehama Tanzania (ICTC).

Akizungumza katika hafla hiyo Machi 29, 2025 Mkurugenzi Mkuu Tume ya Tehama Tanzania, Dk Nkundwe Mwasaga amesema utiaji saini wa ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa programu ya Tanzania ya kidijitali katika kujenga uchumi wa kidijitali nchini.

“Wajasirimali wanafanya kazi mchanganyiko, hivyo vituo hivi vitafanya kazi kwa pamoja, watakaoingia kwenye vituo hivi baadaye watapelekwa Chuo cha DTI Dodoma kinachojengwa na Korea,” amesema.

Amesema wataangalia mnyororo mzima wa ubunifu kwa Tanzania kuanzia chini kabisa.

Amesema hiyo ni dhamira ya Serikali kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kidijitali na kijasiriamali.

Dk Mwasaga amesema wamelengwa wabunifu na wajasirimali wa kidijitali, akieleza mjasirimali anaweza kuwa mtu yeyote lakini wabunifu wa kidijitali wapo tofauti.

Amesema mwanafunzi anaweza kutoka chuoni akiwa na ubunifu lakini ili ukuzwe kuwa kampuni inahitaji vituo vya namna hiyo ndiyo maana vinajengwa nchi nzima.

Akizungumza kuhusu kituo cha Zanzibar, Dk Mwasaga amesema kitagharimu Sh2 bilioni. Amesema wapo wabunifu wengi Zanzibar ambao mara nyingi mashindano ya Tehama ya kitaifa yanapofanyika huona kampuni nyingi na vijana wengi wakishinda, hivyo kujenga kituo hicho kutaongeza chachu ya kutengeneza kampuni za kijasiriamali visiwani humo.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), haiwezi kubaki nyuma katika masuala ya kidijitali na itahakikisha inakwenda kwa kasi ya dunia katika masuala hayo.

Amesema hivi sasa dunia inakwenda kwa kasi kubwa katika dijitali, hivyo Serikali itahakikisha haimuachi mtu nyuma katika teknolojia.

“Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 imeweka mkazo katika kufikia uchumi wa kidijitali na hata katika mpango wa kati wa maendeleo (Zadec) imetilia mkazo jambo hilo,” amesema.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na SMZ zimefanya kazi kubwa kuweka miundombinu, ikiwemo mkongo na juhudi kubwa za kuhakikisha inaunganisha kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar kupitia Fumba na kuunganisha Tanga na Pemba.

Miundombinu mingine amesema Serikali inataka kuweka mkongo wa pili utakaotoka Mombasa nchini Kenya hadi Fumba ili kuungana na kimataifa.

Akizungumzia kituo hicho, Dk Khalid amesema kimeakisi dhamira ya Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ambacho kitaweza kuwanufaisha vijana na kupunguza tatizo la ajira. 

Vituo vingine vitajengwa Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya na wajasiriamali watakuwa wanafanya kazi kwenye mnyororo mmoja.