Viongozi wa dini: Tuilinde amani inakuza uchumi, ustawi wa jamii

Sheikh Idd Hussein Idd na Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa CCT Zanzibar, Canon Barankena wakizungumza kuhusu maadhimisho ya siku ya amani yatakayofanyika Kitaifa Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Unguja. Wakati maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani yakifanyika kitaifa kesho kisiwani Zanzibar, viongozi wa dini wamewakumbusha wananchi kujiepusha na migogoro inayoweza kuibua vurugu na kuchochea uchumi wa taifa kudidimia.
Siku ya amani kimataifa hudhimishwa Septemba 21 kila mwaka baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) kuitangaza kuwa siku maalumu ya kukumbushana kuimarisha amani na kutokuwa na ghasia kupitia azimio namba 36/67 la mkutano mkuu wa baraza hilo la mwaka 1981.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 20, 2023 kuhusu maadhimisho hayo yanayoandaliwa na UN, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa (CCT), Zanzibar, mchungaji Canon Barankena amesema kukosekana amani kunarudisha nyuma maendeleo.
“Upendo ukitamalaki tutaishi kwa amani na utulivu, tutapendana na kuabudu kwa uhuru, kila mmoja wetu anawajibika kujiepusha na migogoro,” amesema Mchungaji Barankena.
Akizungumza kaulimbiu ya siku ya amani isemayo ‘vijana waleta amani kuhakikisha maendeleo endelevu’ Mchungaji Barankena amewataka vijana wasijiingize kwenye migogoro kwani amani ikitoweka hakuna atakayesalimika.
Sheikh Idd Hussein Idd kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar amesema faida za amani inaleta maendeleo, kukuza uchumi na uwekezaji wa wageni kutoka nchi mbalimbali.
“Amani si katika ngazi ya nchi tu lakini katika ngazi ya mitaa inapotamalaki eneo hilo lazima liwe na maendeleo tofauti na maeneo yenye vurugu,” amesema.
Amesema amani na utulivu vinapostawi katika nchi, maendeleo ya kitaaluma kiuchumi na kijamii yanakuwa kwa kasi huku hofu ikiondoka kwa wananchi na kufanya mambo yao kwa uhuru.
Ofisa Habari Kitaifa Kituo cha Habari UN, Nafisa Didi amesema kutokana na umuhimu kesho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutterez atagonga kengele maalumu mjini Newyork kuashiria kuwakumbusha nchi wanachama kuiadhimisha siku hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Shirika la Global Peace Foundation, Dk Fatma Waziri alisema kauli mbiu ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa vijana kuweza kuwa chachu katika masuala ya amani na maendeleo endelevu.
"Mkutano huo umelenga katika uchochezi wa maendeleo na mabadiliko ya tabia mbalimbali ambazo zitasababisha kuendelea nchi kuwa na amani,” amesema Dk Fatma.
Katibu Mkuu Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa (Yunatz), Kelvin Edward amesema wanasisitiza vijana kuacha kutumika katika kuvuruga amani kwani ikitoweka hakuna mbadala.
Katika kuadhimisha siku hiyo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji, Mudrick Ramadhan Soraga ambapo mada mbili zitajadiliwa: Uwezeshaji wa vijana katika kuleta amani na namna ya kujenga jamii zenye amani.