Utalii wa Zanzibar washika kasi ongezeko la wageni

Muktasari:
- Ingawa ongezeko hilo halijafikia lengo la wageni 800,000 lililowekwa, linaonesha mvuto unaoongezeka wa Zanzibar kama moja ya vivutio vinavyoongoza Afrika, kutokana na kuimarika kwa usafiri wa anga duniani na kuendelea kwa hamasa kutoka kwa masoko ya Ulaya
Unguja. Zanzibar imeshuhudia ongezeko kubwa katika sekta ya utalii mwaka 2024, kwa kuwapokea wageni wa kimataifa 736,755, sawa na ongezeko la asilimia 15.4 kutoka wageni 638,498 waliowasili mwaka 2023, kwa mujibu wa ripoti mpya ya takwimu za utalii.
Ripoti hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali na Tume ya Utalii Zanzibar.
Ingawa ongezeko hilo halijafikia lengo la wageni 800,000 lililowekwa, linaonesha mvuto unaoongezeka wa Zanzibar kama moja ya vivutio vinavyoongoza Afrika, kutokana na kuimarika kwa usafiri wa anga duniani na kuendelea kwa hamasa kutoka kwa masoko ya Ulaya.
Watalii kutoka Ulaya waliendelea kutawala taswira ya utalii Zanzibar, kwa kuchangia asilimia 71.6 ya jumla ya wageni waliowasili yaani wageni 527,845 mwaka 2024.
Miongoni mwao, Italia ilijitokeza kama soko la kuu kwa kutoa watalii 87,202 sawa na asilimia 11.8, ikifuatiwa kwa karibu na Ujerumani (9.7), Ufaransa (9.4) na Poland asilimia 7.
Uingereza pia ilibaki na uwepo mkubwa wa wasafiri takribani 42,000 kutoka Uingereza.
Kwa upande wa masoko yanayochipukia kama Poland, India, China na Ukraine kulikuwa na ongezeko kubwa huku maeneo hayo yakisajili ongezeko la asilimia 12.8 ya idadi ya wageni ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Wakati watalii wa Ulaya wakiendelea kutawala kwa idadi ya jumla, mataifa ya Afrika yalionesha ongezeko kubwa, likionyesha umuhimu wa safari za ndani ya Afrika kwa uchumi wa utalii wa Zanzibar.
Nchi za Afrika zilichangia wageni 98,402 mwaka 2024, sawa na asilimia 13.4 ya jumla ya wageni wa kimataifa waliowasili.
Hii ni ongezeko la asilimia 16.9 kutoka wageni 84,158 waliorekodiwa mwaka 2023, ikionesha mwelekeo chanya katika safari za kikanda na kuongezeka kwa hamasa miongoni mwa wasafiri wa Kiafrika kuichagua Zanzibar kama chaguo lao kuu.
Afrika Kusini na Kenya ziliiongoza bara kwa idadi ya watalii. Afrika Kusini iliongoza kama soko la juu kwa kuleta watalii 31,254 sawa na ongezeko la asilimia 28.6 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Kenya ilifuatia kwa wageni 23,530, ikionesha ongezeko la asilimia 26.2.
Nchi nyingine za Afrika zilichangia wageni 40,475, wakiwamo wasafiri kutoka Nigeria, Uganda, Rwanda, na Msumbiji. Misri iliona kupungua kidogo, ikiwa na watalii 3,143 kupungua kwa asilimia 0.8 kutoka mwaka 2023.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliendelea kuwa lango kuu la kuingilia Zanzibar, ukipokea wageni 646,830, sawa na asilimia 87.8 ya jumla, huku 592,613 waliwasili kwa ndege za kimataifa. Wasafiri wa njia ya baharini walikuwa 89,925, wakiwamo abiria 5,869 wa meli za kitalii na 84,056 waliowasili kwa feri kutoka Tanzania Bara.
Takwimu zinaonesha kuwa Zanzibar bado ni kituo kinacholengwa na watalii wa mapumziko. Asilimia 98.3 ya watalii wote wa mwaka 2024 walikuja kwa ajili ya likizo, huku asilimia 0.6 walitembelea ndugu na jamaa na asilimia 1.1 waliweka sababu nyinginezo.
Mgawanyo wa kijinsia ulikuwa na upendeleo kidogo kwa wanawake, asilimia 51.9 ya wageni walikuwa wanawake na asilimia 48.1 wanaume. Idadi ya wageni wa kiume na wa kike iliongezeka kwa asilimia 10.7 na 20.1, mtawalia.
Kwa mujibu wa makundi ya umri, asilimia 86 ya wageni walikuwa kati ya miaka 15 hadi 64 kundi la watu wa umri wa kufanya kazi wakati watoto na wastaafu walichukua kila mmoja asilimia 7 ya wageni wote.
Kwa wastani, watalii walikaa Zanzibar kwa siku nane mwaka 2024, karibu asilimia 19.5 ya wageni walikaa kwa siku saba kamili.
Kisiwa kilikuwa na nafasi za malazi milioni 9.2 mwaka mzima, nafasi milioni 5.9 ziliuzwa Julai pekee, sawa na kiwango cha ujazaji wa asilimia 64.3 katika mwezi huo wa msimu wa juu.
Miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kama vyanzo vya watalii, Ukraine ilionesha ongezeko la asilimia 62.3, China asilimia 78.7 na Japan ilishuhudia ongezeko kubwa la asilimia 92.7 ya wageni.
Wachambuzi wanasema mafanikio ya utalii Zanzibar mwaka 2024 ni ushahidi wa mvuto wake wa kimataifa, uwekezaji katika miundombinu na juhudi endelevu za kupanua wigo wa wageni.
Kwa ukuaji thabiti kutoka masoko ya jadi na mapya, visiwa hivyo vinaelekea kuwa na mwaka wa 2025 wenye mafanikio zaidi.