Zanzibar inavyojipanga kuwa kitovu cha utalii wa mikutano

Dar es Salaam. Visiwa vya Zanzibar ambayo ni maarufu kwa utalii wa mambo ya kale, fukwe na viungo sasa vinapambana kuwa kitovu cha utalii wa mikutano kama turufu mpya ya maendeleo ya sekta hiyo muhimu kiuchumi.
Kwa sasa Zanzibar inatajwa kuwa na jumla ya hoteli 710 zenye madaraja tofauti, kati ya hizo 38 ni hoteli zenye hadhi ya nyota tano, jambo linalovifanya visiwa hivyo kuwa miongoni mwa maeneo yenye mvuto wa utalii wa mikutano, makongamano na maonyesho (MICE).
Kulingana na Baraza la Utalii Duniani, thamani ya utalii wa mikutano Afrika ni Dola za Marekani 13 bilioni (zaidi ya Sh32.5 trilioni), ikiwa ni asilimia mbili ya thamani ya utalii huo duniani.
Takwimu hizo za baraza la utalii ni kielelezo kuwa, fursa hiyo ya utalii haijachangamkiwa zaidi katika nchi za Afrika, hivyo inabaki kuwa turufu muhimu kwa uchumi, iwapo itatokea nchi itakayoichangamkia.
Hicho ndicho kinachofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hasa katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuingia madarakani kwa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi.
Tangu kuingia kwake madarakani akiiwakilisha Serikali ya awamu ya nane visiwani humo, ameweka mikakati madhubuti kuhakikisha utalii huo unakuwa miongoni mwa nyenzo ya uchumi wa Zanzibar.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Simai Mohammed Said anasema msukumo wa utalii huo katika visiwa hivyo, unatokana na kuwa sehemu ya maelekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020.
Kadhalika, anasema utalii wa mikutano upo katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEF) wa 2020/25.
Si hivyo tu, anasema utalii wa mikutano ni miongoni mwa maagizo ya Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi kwani aliahidi kwa wananchi.
Mipango hiyo, kwa mujibu wa Said, imeimarisha utalii huo ambapo sasa Zanzibar imekuwa ikiandaa mikutano mbalimbali ya wakuu wa nchi, mawaziri, mikutano ya kikanda na taasisi za kimataifa.
“Hali hii imetokana na kuwepo kwa hoteli zenye hadhi na kumbi kubwa kwa mikutano zinazokubalika kimataifa. Ubora wa mazingira pia unaongeza mvuto katika kumbi hizo, kwani nyingi zipo pembezoni mwa fukwe,” anasema.
Ilivyojipanga
Ili kufikia azma ya Zanzibar kuwa kitovu cha utalii wa mikutano, anasema hekta 60 zimetolewa na Serikali kwa mwekezaji katika eneo la Nyamanzi kwa ajili ya kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano, utakaoizidi mingine ya Afrika Mashariki.
“Kufikia mwaka 2025 Zanzibar itakuwa ikiongoza kwa kuwa na ukumbi mkubwa wa mikutano Afrika Mashariki,” anasema.
Anafafanua ukumbi huo utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 1,500 hadi 2,000 kwa wakati mmoja, kadhalika utahusisha kumbi ndogo za mikutano.
Mtindo wa ukumbi huo, kwa mujibu wa Said, utajengwa kuendana na kumbi za Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Madola na aina nyingine ambazo zimebainika kuwa na soko duniani.
“Kwa ufupi Zanzibar itakuwa kituo kikuu cha mikutano ya kimataifa kwa bara la Afrika,” anasema.
Anaeleza kwa sasa, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale zinaendelea na hatua za ufanikishwaji wa utekelezaji wa mradi huo.
“Hivi sasa kuna timu ipo katika safari maalumu ya kikazi nchini Korea Kusini kufuatilia hatua za ujenzi wa ukumbi huo,” anasema.
Si ukumbi pekee, Said anasema ujenzi wa hoteli mpya ya Emarald iliyopo Matemwe unakaribia kukamilika na ndani yake kutakuwa na ukumbi utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 1,000, unaotarajiwa kuimarisha utalii wa mikutano visiwani humo.
Anasema hamasa inatolewa kwa wawekezaji mbalimbali visiwani humo, wanapojenga hoteli wahakikishe zinakuwa na kumbi kubwa za mikutano kwa kuwa soko la utalii wa mikutano ni kubwa visiwani humo.
Mbali na kumbi, Said anasema yapo maeneo ya nje ambayo mikutano mbalimbali hufanyika na kwamba Serikali imeshayawekea mkakati wa kuyaboresha.
Utalii wa mikutano kabla na baada ya Mwinyi
Said anasema utalii wa mikutano ulikuwepo tangu kabla ya Rais Mwinyi kuingia madarakani, ingawa haukuwa wa kiwango kikubwa kama ilivyo sasa.
Anasema msukumo huo umesababisha kuongezeka kwa idadi ya mikutano katika visiwa hivyo.
“Tangu Rais Dk Mwinyi aingie madarakani haziwezi kupita siku tatu hapa Zanzibar kusifanyike mikutano wa kimataifa, ni jambo linaloshuhudiwa na kila mtu,” anasema.
Kabla ya hapo, anasema mikutano kama hiyo ilifanyika kwa nadra na kilichowavutia waandaaji ilikuwa ni mandhari ya visiwa hivyo, lakini sasa wizara yake inasimamia kutangaza fursa na vivutio vya utalii na hivyo kuwavutia wengi.
“Kwa sasa wizara imelivalia njuga suala la kutangaza utalii na inatumia njia zote katika maonyesho ya kitaifa na kimataifa na njia za mitandaoni,” anasema.
Sekta ya utalii, anasema inachangia asilimia 29.2 katika pato la taifa la Zanzibar, ndiyo maana Rais Mwinyi ameupa nafasi kubwa katika uchumi.
“Utalii wa mikutano unakuza uwekezaji na unazalisha ajira nyingi, hivyo Dk Mwinyi amekuwa akiielekeza Wizara ya Utalii kutumia nguvu nyingi katika kuvuna fursa hii, ikizingatiwa kuwa utalii wa fukwe, jua na mchanga mzuri tayari umeshatangazwa na ni bidhaa yenye ushindani inayopatikana katika visiwa vingine pia, lakini mazingira ya mikutano yaliyopo Zanzibar ni tunu kwingineko ulimwenguni,” anasema.
Hali ya amani, usalama na utulivu katika visiwa hivyo iliyoimarika katika utawala wa Dk Mwinyi, anasema ni turufu nyingine katika soko la utalii wa mikutano.
Kulingana na Said, ni mikutano mingi imefanyika visiwani humo tangu kuingia madarakani kwa Dk Mwinyi, ingawa ni vigumu kuhesabika.
“Mikutano hiyo imeongezeka kwa sasa kiasi cha kuonekana kama ndio kivutio kikuu cha utalii kwa Zanzibar,” anasema.
Anasema katika visiwa hivyo, aina zote za mikutano hufanyika, ikiwemo ile yenye washiriki wenye ukubwa au vyeo au unyeti na mingine inayofanywa na taasisi kubwa.
“Kuna mikutano inayoshirikisha watu wachache, ila ni mikubwa kutokana na hadhi ya washiriki wake ambao hufuata unyeti wa kumbi za Zanzibar kwa kufanyika mikutano ya watu wazito kama wao,” anasema.
“Kumbi za aina hiyo zipo katika hoteli za Zanzibar nyingi mno,” anasema.
Anasema mikutano mingine inayofanyika ni ile ya taasisi kubwa za Kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zilizo chini yake.
“Zanzibar imekuwa New York ndogo kwa kufanyika vikao vingi vya taasisi hizo kwa Afrika Mashariki,” anasema.
Kwa mujibu wa Said, mikutano ya benki, mashirika mengine ya kitaifa, yote imekubali katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk Mwinyi, imekubali Zanzibar kuwa ndio kituo chao cha mikutano.
“Hili limefanyika kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe kuwaalika rasmi kutumia kumbi za mikutano za Zanzibar,” anasema.
Anaeleza tayari kuna mikutano mikubwa iliyothibitishwa kufanyika katika visiwa hivyo mwaka 2024, ikiwemo Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi za Jumuiya ya Madola utakaofanyika Machi 5-8 mwakani.
“Mikutano mingine mikubwa ya kitalii pia nayo itafanyika mwaka 2024 na mingine iliyofanyika mwaka 2023 itafanyika tena mwaka 2024,” anasema.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZATI), Rahim Bhaloo alisema kumekuwa na mwamko mkubwa wa utalii wa mikutano katika visiwa hivyo, ingawa bado hakuna miundombinu ya kutosha kuzidaka fursa hizo.
Anaeleza Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali kufanikisha hilo, kadhalika sekta hiyo binafsi inaongeza juhudi kuwekeza katika hoteli zilizopo ili kuwezesha fursa zilizopo.
“Kwa sasa tunapaswa kutumia miundombinu tuliyonayo kwa kuwa zipo zenye viwango vikubwa vinavyokubalika kimataifa,” anasema.
Anasema moja ya vitu vinavyochagiza mwamko wa utalii huo ni kuwepo miundombinu na hilo ndilo linalofanyika na sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali.