Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SMZ na kipaumbele cha miradi ya  uwekezaji

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Sharif Ali Shariff akikata utepe kuashiria Ufunguzi wa taasisi ya Coldwell Banker Tanzania Zanzibar ambayo itasaidia katika uendelezaji wa majengo ya biashara kisiwani hapa

Muktasari:

Kwa miaka minne, Zanzibar kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (Zipa), imesajili miradi 430 yenye thamani ya Sh11 trilioni, kati ya miradi hiyo asilimia 30 ni majumba ya biashara huku ikitarajia kutoa ajira za moja kwa moja 25,000 hususani kwa wazawa

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kupitia sera zake imetoa kipaumbele miradi ya biashara na vivutio vinavyowavuta wawekezaji kwa lengo la kuwekeza.

Kwa miaka minne, Zanzibar kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (Zipa), imesajili miradi 430 yenye thamani ya Sh11 trilioni, kati ya miradi hiyo asilimia 30 ni majumba ya biashara huku ikitarajia kutoa ajira za moja kwa moja 25,000 hususani kwa wazawa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff leo Jumapili, Februari 2, 2025 wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Coldwell Bankers Tanzania & Zanzibar (CB) kisiwani hapa.

Shariff amesema hatua hiyo inaonyesha utayari wa Serikali kuwekeza katika miradi yenye tija na yenye kuleta mabadiliko katika uchumi wa nchi hiyo.

 Uwepo wa mradi huo mkubwa uliowekezwa katika nchi zaidi ya 40 duniani, utanyanyua nyumba za kibiashara kisiwani hapa na kuwavuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza.

"Miradi kama hii Serikali imetambua namna inavyokuwa na mchango wa kukuza uchumi, kupanua firsa za ajira, ni malengo yetu ni kutengeneza ushindani wa kimataifa katika kuvutia uwekezaji kisiwani hapa,” amesema. 

Amesema kupitia Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2023, Serikali  imetoa kipaumbele kwa wawekezaji katika miradi mikubwa kuendelea kuvutia uwekezaji wa miradi hiyo yenye manufaa kwa Taifa.

“Kwa hiyo brand hii kuja kisiwani hapa itasaidia kuinua uchumi wa nchi yetu na kuwavuta wawekezaji,  jambo hilo ni faraja kwetu," amesema Shariff. 

Amesema Serikali itatoa msaada watakapokwama kwa lengo la kuhakikisha miradi yao inafanikiwa ikiwamo kupatiwa ruhusa na vibali kutoka kwa wadau kwa kuwa, maendeleo ya uwekezaji yamekuwa na spidi kubwa kwa sasa.

Waziri Shariff amesema wanatambua ardhi ya Zanzibar ni ndogo ndio maana wanahitaji miradi inavyokwenda juu (ghorofa) na yenye tija kwa kuwa, haichukui nafasi kubwa katika ujenzi wake.

 "Baada ya kuona ardhi yetu ni ndogo, tunahitaji miradi inayokwenda juu na yenye tija na hatutaruhusu miradi inayotambaa chini," amesema Shariff. 

Mkurugenzi wa CB Tanzania, Gina Washington amesema wamefurahi kufungua kampuni hiyo Zanzibar kwa kuwa inaonesha kisiwa hicho kinakuwa kwa kasi  katika ujenzi wa ghorofa.

 Amewakaribisha wananchi wanaohitaji kujifunza waende kwa sababu sekta ya uwekezaji imekuwa muhimu katika uchumi wa Zanzibar, hivyo wasiache kutumia fursa hiyo.

Washington amewahakikishia wananchi kwamba, hawataachwa nyuma na watafanywa kuwa sehemu ya kampuni hiyo kwa kuwafunza jinsi ya kupata faida kutokana na maghorofa.

 Pia, amewataka wawekezaji kufika katika kampuni hiyo kupata huduma ya kuwekeza katika kisiwa hicho kuelewa maeneo gani ambayo yanafaa kwa miradi ya uwekezaji.

 "Kampuni hii imekuwepo kwa miaka 100 na nchi zaidi 40 duniani na inatoa njia kwa wawekezaji kuwekeza sehemu sahihi, vipi kuweka fedha zao na wapi ili kuona faida zaidi, tunafanya tafiti mbalimbali na kuwasaidia watu kupata mikopo ya nyumba," amesema. 

Meneja wa Kampuni ya Johari Developer Construction, Walid Khalfan amesema kutokana na ardhi iliyopo inapaswa kuwekwa katika sehemu mbili kati ya hizo moja kwa ajili ya kujengwa na nyingine kutunzwa kwa kupanda miti ili kuvutia.

 Hivyo, amesema ujenzi wa maghorofa ndio njia nzuri inayotumika kulinda ardhi katika nchi.