SMZ: Malalamiko dhidi ya bandari ya Malindi yana mashiko

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Muhamed akifafanua mambo kadhaa kuhusu malalamiko ya wadau bandari leo Novemba 29, 2023. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Licha ya Mamlaka ya Usafiri Baharini, Shirika la Bandari na Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL), wafanyabiashara kuahidiwa kufanyika maboresho yatakayoleta ufanisi, inaelezwa kuwa hali ya mambo ni tofauti.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi (SMZ) imekiri imesema malalamiko yanayotolewa dhidi ya huduma za bandari ya Malindi yana mashiko hivyo imeunda kamati shirikishi kutafuta suluhu.
Tangu kubinafsisha shughuli za uendeshaji wake mara kadhaa kumekuwa na malalamiko ya kutoka kwa wadau wa bandari kuhusu tozo kubwa na mabadiliko mengine ya uendeshaji wa bandari ya Malindi kisiwani hapa.
Kamati hiyo itakayoanza kufanya kazi Desemba 2, 2023, inahusisha, wajumbe kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA).
Wengine ni Shirika la Bandari (ZPC), Shirika la Meli (Shipco) na Kampuni ya Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT) inayoendesha bandari hiyo kwa sasa.
Makabidhiano rasmi kati ya SMZ kupitia ZPC na Kampuni ya Afrika Global Logistics (AGL) ya nchini Ufaransa kupitia kampuni tanzu ya ZMT, yalifanyika Septemba 18 mjini Unguja lengo lilikuwa ni kuleta ufanisi na kuondoa malalamiko ya muda mrefu.
Hata hivyo, tangu bandari hiyo upande wa mizigo ilipokabidhiwa na kampuni hiyo kuiendesha Agosti 18 mwaka huu, yamekuwapo malalamiko kadhaa kutoka kwa wafanyabiashara wanaotumia bandari hiyo wakidai hakuna ufanisi unaoonekana bali imezidi kuongeza gharama na tozo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Novemba 29, 2023 katika ofisi za ZPC, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Muhamed amesema Serikali imebaini baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa zina mashiko.
Miongoni mwa malalamiko hayo ni pamoja na malipo kulipwa kwa Dola badala ya Shilingi, kuwapo tozo tofauti kati ya bandari na Dar es Salaam, wanataka muda wa kazi uongezeke na kutokuwapo tofauti ya tozo kati ya meli za ndani na za nje.
“Haya ni miongoni mwa malalamiko kutoka kwa wadau wa bandari, yapo mengi lakini haya ni yale ambayo tumeona yana mashiko na yanaweza kuzungumzika, lengo ni kuleta ufanisi,” amesema Dk Khalid
Wadau hao pia wanataka muda wa saa za kazi uongezeke. Kwa sasa muda wa saa za kazi kwa siku za kawaida ni saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Malalamiko mengine ambayo yatashughulikiwa na kamati hiyo ambayo haina muda maalumu wa kufanya kazi, ni pamoja na kuongezeka kwa tozo za kusafirisha makasha kutoka Bandarini hadi bandari kavu ya Maruhubi.
Nyingine ni kupanda kwa tozo ya kutafuta makasha kutoka dola tano za Marekani hadi dola 30.
Kwa mujibu wa Dk Khalid, kamati hiyo lazima iweke viashiria vya ufanisi jambo ambalo wana imani litaleta mabadiliko na changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi.
“Lazima tukumbuke kwamba hiki ni kipindi cha mpito na haya yanayolalamikiwa yapo kwenye kitabu cha tozo cha mwaka 2018 lakini tulikuwa hatuyatekelezi, kwa hiyo napenda kuwatoa wananchi wasiwasi malalamiko haya yanashughulikiwa,” amesema
Kuhusu malalamiko ya kuzuia kontena zisitoke nje licha ya kushushwa, Dk Khalid amesema utaratibu ni lazima zikaguliwe na mamlaka husika ili kujiridhisha iwapo hakuna vitu visivyofaa huku akitolea mfano kwamba katika ukaguzi huo imewahi kubainika baadhi ya makontena ambayo yalikuwa na bidhaa zisizo hitajika.
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara hao wameileza Mwananchi kwamba walichoelezwa wakati wanaipatia kampuni hiyo kuendesha bandari ni tofauti na kinachotokea kwa sababu hakuna ufanisi wowote.
Mmliki wa meli, Mansour Said amesema tozo zinakuwa kubwa lakini utaratibu unaotumika sio mzuri akitolea mfano wa kulipia meli kabla haijafika wala kushusha mzigo
“Tulichoelezwa sio na tunayoyaona, kwa kweli inazidi kuongeza gharama lakini tumekubaliana tumewapa wiki moja iwapo yasipotekelezwa haya tunakusudia kugoma,” amesema
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZPC, Akif Ali Khamis amesema katika bandari zote utaratibu ndio huo unaotumika kulipia meli kabla, lakini wataangalia utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na kutanguliza malipo ya awali wakati mfanyabiashara akisubiri meli yake.