SMZ kutoa kipaumbele ajira kwa wenye ulemavu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Ndeliananga wakimkabidhi Aksam Masoud futari katika hafla ya kuwakabidhi futari watu wenye ulemavu Zanzibar
Muktasari:
- Miongoni mwa hatua inazochukua ni pamoja na kufuta sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2006 na kutunga sheria mpya ya watu wenye ulemavu namba tisa ya mwaka 2022 ambayo imeweka misingi imara ya kuwalinda na kuwaendeleza.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema itatoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa sawa katika nafasi za utendaji ndani na nje ya nchi
Hayo yamesemwa leo Machi Moshi, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika hafla ya ugawaji wa futari kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya kusaidia watu wenye ulemavu (TFED).
Katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali inatambua umuhimu na mchago wa watu wenye ulemavu na katika nafasi ambazo imetoa kwa viongozi wameonyesha ufanisi mkubwa kutekeleza majukumu yao.
"Niwahakikishie ikiwa kuna nafasi shindani, ikitokea ajira kama kuna mtu mwenye ulemavu basi kipaumbele cha kwanza kitakuwa kwake, huu ni mpango wa Serikali," amesema.
Amesema katika kutambua changamoto za walemavu, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa kama wengine.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufuta sheria namba tisa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2006 na kutunga sheria mpya ya watu wenye ulemavu namba tisa ya mwaka 2022, ambayo imeweka misingi imara ya kuwalinda na kuwaendeleza.
"Pia, Serikali imeanzisha mabaraza katika wilaya zote ya watu wenye ulemavu kwa lengo la kuhakikisha wanatambulika na kujumuishwa katika sera, sheria, mipango na programu mbalimbali za maendeleo," amesema.
Katika kulijali kundi hilo, Serikali imejenga shule mbili za bweni kwa ajili ya watu wenye ulemavu katika kuwaendeleza kielimu.
Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa watu hao kwa vikundi vyao mikopo isiyo na riba kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).
Pia, itaendelea kuzisimamia taasisi zinazotoa vibali vya ujenzi kuhakikisha inakuwapo miundombinu rafiki na wezeshi ili wazifikie fursa na huduma mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFED, Christina Mngara amesema wanapenda kuona watu hao wanathaminiwa bila kutazama viungo vyao.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Ummy Ndelinanga amewataka watu wenye ulemavu wasijisikie vibaya kwa kuwa Mungu alikuwa na makusudi yake kuwaumba hivyo.
"Tufurahie jinsi tulivyo na tusijikatie tamaa wala kujisikia vibaya, naomba niwatie moyo kwamba Mungu ana makusudi yake na uwezo tunao kufanya mambo makubwa," amesema huku akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba iwapo angejikatia tamaa asingefika katika nafasi hiyo aliyonayo.
Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harus Said Suleiman amesema kuna watu wengi wenye ulemavu wanaohitaji kusaidiwa akiwataka wenye uwezo wa kufanya hivyo kujitokeza kuwasaidia.
Amesema jumla ya familia 500 zimepewa futari hiyo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema kundi hilo limekuwa likisahaulika na kuwafanya wawe wanyonge kwenye jamii.
"Mara nyingi utaratibu wa kuwapa watu hawa unakuwa tofauti kidogo, wengine wanawapa wasio na mahitaji wanaachwa wenye kuhitaji, kwa hiyo sisi tutawatazama kwa ukaribu bila kuwabagua na kuhakikisha wanaopewa ndio walengwa," amesema Ayoub
Naye Waziri wa Afya, Ahmed Nassor Mazrui amesema watahakikisha wanapata matibabu bila ubaguzi katika vituo na hospitali zote za Serikali.
Baadhi ya watu wenye ulemavu waliopewa futari hiyo, akiweo Mahira Hamad pamoja na kushukuru ameomba wafikiwe na wengine wenye mahitaji kama wao katika maeneo mbalimbali