Prime
Nje ya siasa, Lissu humwambii kitu kwa Yanga, ugali

Muktasari:
- Anasema hakuanza kuifuatilia na kuipenda timu hiyo juzi wala jana; ni mpenzi wa Yanga tangu utotoni.
Ikiwa ulidhani Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu yupo kwenye siasa pekee, unakosea sana.
Mwanasiasa huyo anasema yeye ni mpenzi wa michezo kama riadha na tenisi, lakini ni mfuatiliaji mzuri wa soka na hapa Tanzania na ni Yanga kindakindaki.
Anasema hakuanza kuifuatilia na kuipenda timu hiyo juzi wala jana; ni mpenzi wa Yanga tangu utotoni.
“Japo sijawahi kuhudhuria mechi ya watani wa jadi hata moja hivi karibuni, lakini nyingi za za miaka ya 1970 nilizifuatilia.
“Mechi za miaka hii sizifuatilii sana, naona nikienda uwanjani kuna siasa nyingi, hivyo naishia kuangalia kwenye televisheni, japo dabi hii (itakayochezwa Machi 8, 2025) nitakuwa Dar es Salaam, nitakwenda uwanjani” anasema Lissu katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Anasema aliipenda Yanga tangu enzi za kina marehemu Gibson Sembuli, mchezaji aliyekuwa akimvutia kutokana na aina ya uchezaji wake.
“Sio Sembuli tu, kulikuwa na Juma Pondamali Mensah, Mohamed Yahaya, Sunday Manara aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kwenda kucheza Ulaya, akiitwa Computer, wakati huo hizo computer tunazisikia tu,” anaeleza.
Kumbe aliwahi kucheza soka
Mbali na kuipenda Yanga, Lissu anasema aliwahi kucheza soka japo si kwa kiwango kikubwa.
“Nilicheza nilipokuwa shule msingi, nilipofika sekondari nikakuta watu wakubwa sana sikuendelea,” anasema.
Mbali na soka la Bongo, Lissu anasema kwa Ulaya, anafuatilia zaidi soka la Uingereza na ni mnazi wa Manchester United.

“Wakishuka daraja, wakichuma majanga watakula na sisi mashabiki wao, naipenda Manchester,” anasema na kuongeza.
“Nafahamu mpira wa duniani na ninaufuatilia. Nafuatilia michezo pia, ikiwamo riadha, tenisi, I wish (natamani) ningekuwa mchezaji, lakini sikufikia huko japo vijana wangu ni wataalamu zaidi kwenye soka,” anasema.
Lissu na familia
Mwanasiasa huyo machachari, tofauti na alivyozoeleka katika majukwaa ya kisiasa, anasema akiwa nyumbani ni baba wa kawaida anayependa kuipikia chakula familia yake.
“Nikiwa nyumbani ni baba wa kawaida sana, hata ukizungumza na hawa walinzi wangu watakueleza hivyo, ambacho nakifurahia zaidi familia yangu imekuwa baraka kubwa mno kwangu,” anasema na kuongeza:
“Wanangu huwa wananiambia we mzee, siku siasa ikikushinda, tunafungua mgahawa wa break fast (mlo wa asubuhi).’’
Lissu mume na baba wa vijana wawili wa kiume pacha wenye miaka 23 sasa, anasema familia yake huwa inapenda mapishi yake akiwa nyumbani.
“Mimi najua kupika sana, naweza kupika ukashangaa, ninapenda kuwapikia wanangu, nao wanajua mimi ni mtaalamu sana wa kupika, wamekuwa wakifurahia zaidi mapishi yangu,” anasema Lissu katika mazungumzo aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake hivi karibuni.
Kwa kusisitiza utalaamu huo, Lissu anasema anajua zaidi kupika vyakula vya asubuhi.
“Lakini ukitaka nikupikie uwe na subira,” anasema Lissu huku akicheka na kufafanua kwamba, akiingia jikoni sio mtu wa kupika kwa haraka, kwani huchukua saa kadhaa aandae msosi maridhawa kwa mlaji.
Licha ya kuwa mtaalamu wa mapishi hayo ya asubuhi, Lissu ni mpenzi mkubwa wa ugali na maziwa mtindi.
Anasema zikipita siku mbili bila kula ugali, hayo ni huwa ni maisha magumu sana kwake.
“Aisee, siwezi, zipite siku mbili sijala ugali? Yatakuwa ni maisha magumu sana kwangu, napenda ugali na mboga yoyote, lakini maziwa mtindi yasikosekane.
“Kwa Wanyanturu (kabila lake) ugali na mboga za majani kama mlenda, mchicha na maziwa ni chakula chetu, mimi nikila wali siku mbili tatu mfululizo hayo ni maisha magumu, napenda ugali," anasema.
Familia inavyopokea misukosuko yake kisiasa
Licha ya kupitia misukosuko kadha wa kadhaa ukiwamo kunusurika kifo, kuwekwa mahabusu na misukosuko mingine, Lissu anasema katika changamoto hizo, hakuna mtu kwenye familia yake aliyewahi kumshawishi kuachana na siasa.
‘Si mke wangu wala watoto wangu, hata wazazi wangu wakati wapo hai hakuna aliyewahi kuniambia niachane na siasa, kwa kuwa wanafahamu haya ndiyo maisha yangu," anasema na kuongeza:
“Mtu yeyote katika familia yangu hajawahi kuniambia mbona hiki kitu (siasa) kinaleta usumbufu achana nacho. Nakumbuka niliwekwa rumande kwa mara ya kwanza katika mkesha wa Krismasi mwaka 2002 baada ya hapo hali hiyo imetokea mara nyingi, nawekwa ndani na makosa wanayonipa ni yale yale ya uchochezi, lakini familia haijawahi kunishawishi niache siasa, haya ni maisha yangu."
Katika ibada ya shukrani hivi karibuni nyumbani kwao Singida, familia yake ilisema itakuwa ya kwanza kumrejea pale utakapokengeuka, jambo ambalo Lissu anasema kauli kama hiyo wamekuwa wakimueleza mara kwa mara.
“Siku hiyo walisema hadharani, ni kitu ambacho wanakisema siku zote tukiwa pamoja, kwamba inuka nenda kafanye kazi yako, sisi tunakuunga mkono, usibadilike, usiwe kitu kingine, pengine kwa watu kauli ya familia yangu imesikika mara ya kwanza, lakini mimi wananiambia mara nyingi,” anasema na kuongeza kuwa familia yake imekuwa ni baraka kwake.
Anasisitiza kuwa japo mkewe na watoto wake hawataki kujishughulisha na siasa, hawajawa kikwazo kwake.
Anasema inawezekana familia yake inatamani awe baba kama kinababa wengine, lakini inajua kuwa ana dhamira fulani katika maisha yake.
"Hawataki wao kushiriki, lakini huwa hawaachi kuniambia wewe endelea, inapotokea nimekamatwa nimewekwa mahabusu wananiuliza wewe mzee vipi tunasikia umekamatwa? Nawambia ndio sehemu ya kazi, hata mimi mwenyewe, haijawahi kunitokea nikawaza kutoka kwenye siasa," anasema.
Siasa sio cheo
Kwa Lissu siasa sio kuwa na nafasi fulani au cheo fulani, Anasema anafanya siasa kwa sababu
ndivyo anavyoona inatakiwa kufanyika kupigania nchi na si kupata nafasi.
"Watu wengine wanafikiria siasa ni cheo, ubunge au uwe na nafasi fulani labda ya uenyekiti, niwakumbushe tu kwamba siasa ya aina hiyo kama ndiyo siasa yako inaweza kuku disappoint ( kukukatisha tamaa) usipozipata hizo nafasi.
"Mimi sifanyi siasa ili nipate cheo, siasa ni maisha yangu, unafikiri nafanya yote sababu nataka ka cheo fulani, nafanya hivi sababu ndivyo ninavyoona inatakiwa kufanyika," anasema.
Anasema japo akiwa na
cheo inasaidia kupaza sauti, ukiwa mbunge unakuwa na uwanja mpana wa kusikika.
"Ukiwa mwenyekiti wa chama una uwanja mkubwa, hicho ni kipaza sauti chako, lakini kitakuwa kikubwa kama unacho cha kusema kama huna hata uwe R
rais hutokuwa na cha kusema," anaeleza Lissu aliyenusurika kuuawa kwa risasi mwaka
Anasema yeye yupo Chadema daima na hata akiwa na cheo au asiwe nacho, amekuwa na cha kusema kinachohusu siasa za nchi.
"Mtu akiniambia niachane na siasa maana yake niache kuishi, niache kuhangaika na haya ninayohangaika nayo, niache kufikiria. Nikiona jambo linaenda ovyo ovyo nisilisemee, niache! siwezi," anasema.
Maisha ya watoto wake
Anasema wakati ukifika Lissu ataozesha vijana wake hao wawili, ambao amekuwa akiwatania mara kadhaa na kuwataka wamtambulishe kwa watu watakaokuja kuwa wenza wao.
"Ni vijana wakubwa sasa, wana miaka 23 ni kinababa sasa, siku moja niliwauliza wananishangaa wakaniambia wewe mzee vipi? Niliwauliza mbona hamnitambulishi (kwa wachumba wao) nimekaa wiki nzima hapa hata kutambulishwa sijatambulishwa? wakasema wewe mzee achana na hizo usiwe na haraka," anasema Lissu huku akitabasamu.
Hata hivyo, anasema wakati vijana wake hao watakapotaka kuoa, yuko tayari kumpokea mkwe yeyote atakayeletewa, akisisitiza yeye si miongoni mwa wazazi wanaowachagulia watoto wao watu wa kuoa.
"Siko hivyo kabisa, wewe utakayemleta ndiye huyo huyo si umemkubali wewe? si utaishi naye? Sasa mimi ni nani wa kuanza kukwambia aaahh, najua huwa mnafanyaje huko mkiwa peke yenu?, sijui umempendea nini? Sina presha kabisa kwenye hilo," anasema.
Humwambii kitu kwa Bob Marley
Mbali na soka na siasa, Lissu anasema anapenda muziki, lakini sio tu muziki wa kuburudisha, bali wa kujenga.
Anasema yeye ni shabiki wa nguli wa reggae, na anapenda kusikiliza zaidi nyimbo za Bob Marley.
“Huwezi kuacha kumsikiliza Bob Marley. Nyimbo zake ni za kujenga na ukiwa mwanaharakati kama mimi huwezi kuacha kumsikiliza siku zote,” anasema.