RC Kusini Pemba apiga marufuku kuhamisha watendaji baraza la manispaa

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid
Muktasari:
- Uhamishaji wa wafanyakazi unatajwa kuchangia shughuli za Manispaa ya Chakechake kuzorota.
Pemba. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba (RC), Rashid Rashid ameuagiza uongozi wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Chakechake kusitisha uhamisho kwa mtendaji anayetaka kuhamia taasisi nyingine kwa kuwa, jambo hilo linalifanya baraza kushindwa kutimiza wajibu wake kutokana na uhaba wa wafanyakazi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 21, 2025 wakati akizungumza na wananchi pamoja na uongozi wa baraza hilo huko Madungu Mjini Chakechake katika kampeni maalumu ya uhamasishaji wa usafi katika mkoa huo.
Amesema kumekuwa na uhamisho wa kiholela kwenye manispaa hiyo.
“Haiwezi ikawa watu wanatolewa kiulani kwa vile mtu ana jamaa yake wakati yeye aliomba ajira kwa makusudi kufanya katika baraza hilo,” amesema.
Amesema kuanzia sasa hakuna ruhusa kwa uongozi wa baraza hilo kuhamisha mtu maana sasa hivi tayari baraza limeshakuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi wanaoshindwa kufanya kazi kwa ukamilifu.
Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya amesema kutokuwepo utaratibu mzuri katika kuwaondoa watendaji kunaweza kusababisha kuzorotesha harakati za usafi katika manispaa hiyo jambo jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa wananchi unaotokana na milipuko ya magonjwa mbalimbali katika kipindi hichi cha mvua kubwa zinazonyesha.
“Lazima kuwepo utaratibu mzuri sio kila mtendaji mwenye jamaa yake anamhamisha, hili sio jambo zuri linaweza kutuathiri, maana mazingira yataweza kushindwa kuwekwa vizuri.”
“Ni lazima katika kufanya uhamisho kuwepo na utaratibu mzuri sio tu mtu akitaka kuhama anamtafuta jamaa yake bila kuangalia matokeo ya baadaye hili sio jambo zuri,”amesema Mgeni.