Rais Mwinyi awaweka pembeni RC, ma- DC wakiwamo wanaoutaka uwakilishi, ubunge

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amefanya uteuzi wa mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya watano kufuatia baadhi ya waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi za uwakilishi na ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano ya Rais Ikulu kwa vyombo vya habari usiku wa jana Jumanne Julai mosi, 2025 ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Hamida Khamis Mussa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Hamida anachukua nafasi ya Ayoub Mohamed Mahmood ambaye amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge wa Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rajab Ali Rajab ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati akichukua nafasi ya Gallos Nyimbo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Magharib A akichukua nafasi ya Sadifa Juma Khamis.
Kabla ya uteuzi huo Rajab alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Bandari katika Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA).
Miza Hassan Faki ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkoani akichukua nafasi ya Hamad Omar Bakar. Kabla ya uteuzi huo Miza alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkoani Pemba.
Mwingine aliyeteuliwa ni Moh'd Ali Abdallah ambaye anakwenda Wilaya ya Mjini akichukua nafasi ya Hamid Seif Said. Kabla ya uteuzi huo Abdallah alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amour Yussuf Mmanga ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B ambaye anachukua nafasi iliyoachwa na Hamida aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja. Amour ni diwani mstaafu.
Uteuzi huo umeanza Julai mosi na wateule wote wataapishwa Ikulu Zanzibar kesho Alhamisi Julai 3, 2025 saa 7:00 mchana.