Programu ya Mobile Youth Space kuwaunganisha vijana na ajira Z’bar

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya Mobile Youth Space (MYS).
Muktasari:
- Programu hiyo inalenga kuwaunganisha vijana na fursa za kiuchumi, kisiasa, kijamii pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwa wazalendo, mshikamano na kuwaimarisha washiriki katika upatikanaji wa taarifa kupitia nyanja hizo.
Unguja. Katika kuimarisha ushiriki na upatikanaji wa taarifa kwa vijana katika ngazi ya uamuzi, uongozi na ajira, Baraza la Vijana Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la SOS limeandaa programu ya Mobile Youth Space (MYS) na kampeni ya ‘Amani ni tunu, vijana tuienzi’.
Programu hiyo inalenga kuwaunganisha vijana na fursa za kiuchumi, kisiasa, kijamii pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwa wazalendo, mshikamano na kuwaimarisha washiriki katika upatikanaji wa taarifa kupitia nyanja hizo.
Akizindua programu hiyo leo, Jumatatu Aprili 14, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab amesema programu hizo zitaimarisha ushiriki na upatikanaji wa taarifa kwa vijana pamoja na kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
"Bado vijana wanakabiliwa na changamoto ya ushiriki na ushirikishwaji, hususan katika mambo yanayowahusu na kukosa fursa, hivyo programu hizo ni chachu ya upatikanaji wa taarifa sahihi kwa vijana ili kutimiza lengo na ndoto zenu za kimaisha," amesema Fatma.
Akizungumzia kampeni ya ‘Amani ni tunu, vijana tuienzi’, Katibu Fatma amesema itatumika katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kuanzia mwezi huu hadi Desemba 2025.
Hata hivyo, amesema kampeni hiyo itaendelea kutumika hata baada ya uchaguzi katika programu endelevu za baraza la vijana.
Amesema suala la kuhamasisha amani ni la kila siku, halipaswi kufanyika katika kipindi cha uchaguzi mkuu pekee.
Waziri huyo amesema inapofikia kipindi cha uchaguzi, vijana ndio wanaotumika kuivuruga amani, “Kwa hiyo programu hii inalenga kuwajengea uelewa na kujitambua katika kulinda nchi yao,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan amesema lengo la programu ni kuimarisha ushiriki na upatikanaji wa taarifa kwa vijana kupitia nyanja mbalimbali.
Hassan amesema programu hizo zitakuza ushirikiano na taasisi nyingine zinazoshughulikia maendeleo ya vijana nchini kwa kuhamasisha kulinda amani na usalama, na kuimarisha ushiriki wao katika kutunza amani na utulivu nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la SOS, Gharib Abdalla Hamad amesema shirika hilo ni wadau wakubwa wa maendeleo ya vijana, hivyo watashirikiana na Baraza hilo kufikia lengo lililokusudiwa.
Amesisitiza kuwa vijana wana nafasi ya kuchangia katika maendeleo ya taifa endapo watapewa fursa; upo umuhimu wa kuwasaidia kupata fursa zinazolenga kuwawezesha kutoa mchango katika maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mbali na hayo, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha vijana wanapata maarifa ya mafunzo ya amali na kujikwamua kiuchumi.