Polisi yaonya madereva, wahalifu sherehe za Idd

Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi, Richard Thadei Mchomvu akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake Madema.
Muktasari:
- Jeshi la Polisi limewaonya madereva wenye tabia ya kuendesha vyombo kwa mwendo kasi na kupiga misele (drifting) kuacha tabia hiyo.
Unguja. Jeshi laPolisi Mkoa wa Mjini Magharibi limewataka wananchi kuitumia vyema sikukuu ya Idd el Fitr na isiwe chanzo cha kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo wizi, uporaji, unyang'anyi, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia.
Jeshi hilo limetoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.
Wito huo umetolewa leo Machi 28, 2025 na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Richard Mchomvu alipozungumza na waandishi wa habari ofisi kwake Madema.
Mchomvu amesema kutokana na umuhimu wa sikukuu hiyo, wamejipanga vyema kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote, yakiwamo ya viwanja vya sikukuu, barabarani kwa doria na misako mitaani.
"Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu kwa amani na utulivu na isiwe chanzo cha kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani ikiwemo, wizi, uporaji, unyang'anyi, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia," amesema.
Amesema wapo askari zaidi ya 500 mitaani kwa ajili kulinda amani na usalama wa wananchi na hawatafumbiwa macho wanaovunja sheria.
Kamanda Mchomvu amewataka madereva wenye tabia ya kuendesha vyombo kwa mwendo kasi na kupiga misele (drifting) katika barabara eneo la Michenzani, barabara ya Fumba, Fuoni, Uwanja wa Ndege na maeneo mengine kuacha tabia hiyo.
Amesema kufanya hivyo ni kosa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi watakapobainika.
Mchomvu amewaomba wananchi kutotumia magari yasiyo rasmi au yasiyosajiliwa kubeba abiria kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kuhatarisha maisha ya dereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Pia ametoa angalizo kwa wazazi na walezi kutowaacha watoto kwenda viwanja vya sikukuu bila uangalizi kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha watoto kupotea, kupata ajali na kudhalilishwa.
Kwa wamiliki wa kumbi za starehe, amewataka kuhakikisha wanafuata taratibu za uendeshaji kwa kuzingatia muda wa kufunga kama ulivyoelekezwa katika vibali vyao.
Amesema maeneo ya kucheza watoto yatafungwa saa nne usiku kwa kipindi chote cha sikukuu.
Mchomvu amesema katika kudhibiti ajali za barabarani kwa kipindi cha sikukuu baadhi ya barabara zitafungwa kwa muda.
Barabara hizo ni za Ng’ambo Polisi hadi Kariakoo, Kwa Bizredi hadi Kariakoo, Kibanda Hatari hadi Miembeni, Round About Miembeni hadi Kariakoo.
Nyingine ni Maisara hadi Mnazi Mmoja, Baraza la Wawakilishi la zamani hadi Shirika la Magazeti ya Serikali na Kwa Mzee Mwinyi hadi Bosnia.