Othman: Kamati ya amani haijafanikiwa Zanzibar

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi (kushoto), akimkabidhi Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud kitabu cha mwongozo wa viongozi wa dini kuhusu uchaguzi wakati kamati ya Aman Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mufti Mkuu ilipomtembelea ofisini kwake Unguja.
Muktasari:
- Amesema ili kustawisha amani kabla na baada ya uchaguzi, lazima kamati hiyo ijikite kwa kuyaeleza bayana na wazi yale yanayochangia kuvunjika kwa amani pindi unapofika uchaguzi mkuu.
Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, amesema suala la kutafuta amani ya nchi linahitaji dhamira ya kweli, inayojali misingi ya utu, haki na uadilifu, wala si jambo la msimu kwa ajili ya kupata shukrani na fadhila za kisiasa.
Amesema kwa maoni yake, Kamati ya Amani Zanzibar inayohusisha viongozi mbalimbali wa dini bado haijafanikiwa, kwa sababu chanzo kinacholeta migogoro ni kutokuwepo haki kwa watu kunyimwa haki zao.
Amesema ili kustawisha amani kabla na baada ya uchaguzi, ni lazima kamati hiyo ijikite kwa kuyaeleza bayana na wazi wazi yale yanayochangia kuvunjika kwa amani pindi unapofika uchaguzi.
Othman amesema hayo leo Jumamosi, Mei 3, 2025, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Kamati ya Amani inayojumuisha viongozi mbalimbali wa dini, wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi.
“Ni wajibu kwa kamati na mamlaka yoyote inayohubiri amani ya kweli, kuzingatia misingi muhimu ya haki, uadilifu, ambayo hatimaye yatabakiza nchi ikiwa salama na yenye utulivu,” amesema.

Hivyo, ameitaka kamati hiyo kushughulikia changamoto na malalamiko yanayojitokeza kila mara, akisema kuanzishwa kwa kamati hiyo ni jambo jema lakini kinachohitajika ni kuwepo nia thabiti na dhamira ya kweli ya kuyakabili mambo yote yanayoleta mkanganyiko wa amani kwa watu wa Zanzibar katika miongo mitatu ya uchaguzi uliopita.
Othman ameieleza kamati hiyo kuwa iwapo ina dhamira ya kupigania amani ya kweli katika visiwa hivyo, lazima isimame imara na kuwakabili wenye mamlaka wote waliopo madarakani, na itoke hadharani kuyakemea pindi yakitokea yasiyokubalika.
“Hata ukiwa kwenye mashindano ya mpira, kama refarii hatendi haki, amani hiyo ambayo ni tunu ya kila mtu, itapatikanaje iwapo patakosekana uadilifu na mwamuzi wake dhahiri hatendi haki,” amesema, huku akihimiza haja ya kuhusisha amani ya taifa na uchaguzi huru na wa haki.
Pia, ametumia fursa hiyo kuhimiza haja ya kulinda mshikamano wa wananchi katika jamii, maridhiano, umoja wa kitaifa, huku akisema wafuasi na wapenzi wa chama chake na hata waasisi wake, akiwemo Maalim Seif Sharif Hamad ambaye hadi anafariki dunia aliwausia juu ya kulinda amani, na wamekuwa mfano wa kwanza kutekeleza hilo.
Hata hivyo, Othman ameipongeza na kueleza kuunga mkono juhudi za kamati, huku akiahidi kuipa ushirikiano, na kwamba anaifungulia milango wakati wowote watakapohitaji msaada wake kwa ajili ya amani ya taifa.
Kwa upande wake, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Kaabi, amemshukuru Othman kwa ukarimu wake, huku akiahidi kuyatendea kazi maoni, mapendekezo na miongozo aliyotoa kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi.
Mufti Kaabi ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, pia amemuombea dua na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake, wakati huu ambao nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu.
Katika hatua nyingine, Mufti Kaabi amemkabidhi Othman nakala ya kitabu cha kamati hiyo cha mwongozo wa viongozi wa dini kuhusu uchaguzi.
Wakiwasilisha salamu fupi za kamati hiyo, wajumbe Sheikh Thabit Nuuman Jongo na Askofu Dickson Kaganga wamesema dhamira ya kuhasisiwa kwa chombo hicho ni kutokana na madhila, masaibu, machungu na maumivu wanayopata wananchi wasiokuwa na hatia, hususani wazee, wanawake na watoto.
Askofu Kaganga ambaye ni katibu wa kamati hiyo, amesema walipatwa na msukumo tangu yalipotokea maafa ya uchaguzi mwaka 2001, 2002, kisha walikaa viongozi wa dini mwaka 2004 kuangalia namna ya kushughulikia changamoto hizo.
“Wapo waliopoteza macho na miguu, wengine wamekuwa walemavu wa kudumu, tulikuwa tukijiuliza kwa nini inakuwa hivyo,” ameongeza na kuhoji Sheikh Jongo, wakati akieleza chanzo cha kuasisiwa kwa kamati hiyo.
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amesema lengo la kamati hiyo ni kuwafikia viongozi na watendaji wakuu wa nchi.
“Lengo kuu ni kuzinduana kupitia mambo mawili ya msingi, ambayo ni kutafakari ile historia iliyosababisha kuasisiwa kwa chombo hiki pamoja na kuwagawia na kuwawasilishia wahusika nakala ya kitabu maalum kinachohusu amani ya nchi,” amesema.