Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Othman ahamasisha mageuzi matumizi ya rasilimali

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud akizungumza na wananchi wa Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba leo Juni 8, 2024.

Muktasari:

  • Asema wananchi hawapaswi kukata tamaa, washirikiane kupigania mageuzi yatakayosaidia kuzitumia rasilimali kuleta neema kiuchumi.

Pemba. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema wananchi hawapaswi kukata tamaa badala yake washirikiane kupigania mageuzi yatakayosaidia kuzitumia rasilimali zilipo nchini na kuleta neema ya kiuchumi.

Othman ameyasema hayo Juni 7, 2024 katika Baraza ya Mtemani Wete, iliyopo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipozungumza na wafanyabiashara wadogowadogo, wanabaraza na wananchi.

Othman ambaye pia ni makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, amesema Taifa limejaliwa neema na rasilimali nyingi za kiuchumi ambazo zinahitaji kusimamiwa vyema ili zilete manufaa makubwa zaidi ya kimaendeleo katika kukuza na kuimarisha uchumi kwa Wazanzibari wote.

“Kwa hiyo ndugu zangu hatupaswi kukata tamaa tunapoona mambo yanakwenda kombo, kikubwa tushikamane tusonge mbele,” amesema Othman.

Amesema malalamiko ya wananchi yanapaswa kufanyiwa kazi ili kuweka mazingira sahihi ya shughuli za kibiashara na huko ndiyo kutatua kero za wananchi.

Amesema wamiliki wa serikali za mitaa ni wananchi wenyewe, hivyo watendaji wanapaswa kuwajibika kwa kusikiliza na kutatua kero zao, yakiwemo maeneo ya biashara na shughuli za kijamii.

Akizungumzia ujenzi wa Bandari ya Wete, Othman amesema Serikali ina nia ya kuijenga, akieleza hivi sasa inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu kufahamu namna sahihi ya kufanya ujenzi huo.

Kuhusu malalamiko ya wananchi kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, amesema suala hilo ni miongoni mwa hoja ambazo zimo katika masharti ya msingi ya chama hicho, kuendelea au kutokuendelea kuwamo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

“ACT-Wazalendo tunaendelea kuchukua jitihada kuinusuru Zanzibar na machafuko yanayotokea kila kipindi cha uchaguzi. Vichocheo na viashiria vyote vinavyosababisha kuzuka hali ya sintofahamu, vurugu na maafa ya namna hiyo kutokea ni lazima viondoke,” amesema.

Awali wananchi walimweleza Othman changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kukosa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Omar Kombo Said, amesema suala la kunyimwa vitambulisho kwenye shehia linaibua hofu ya uchaguzi, hivyo kumuomba ashughulikie jambo hilo.

“Wananchi wanakumbana na changamoto nyingi, hata za kibiashara, tunaomba kuangaliwa kwa sababu iwapo tukiendela hivi hali inakuwa ngumu,” amesema.