Migogoro ya ardhi yatawala kampeni ya Mama Samia Legal Aid ikizinduliwa Z'bar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora, Haroun Ali Suleiman akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Muktasari:
- Kampeni hiyo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa Aprili, 2023 ikilenga kutoa elimu na kuwasaidia wananchi mbalimbali katika mikoa ya Tanzania Bara na visiwani kwa gharama ya Sh6 bilioni.
Unguja. Wakati kampeni ya msaada wa kisheria inayojulikana kama Samia Legal Aid ikizindiliwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkuu wa Mkoa huo, Mattar Zahor amesema changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni migogoro ya ardhi inayosababishwa na shughuli za utalii.
Hivyo, amewataka wananchi hao wajitokeze kwa wingi kupatiwa ufumbuzi wa matatizo hayo, kwani suala la haki ni maisha ya kila siku ambayo yatawafanya kuwa na amani.
Mattar ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 23, 2025, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC), ambapo huduma hiyo itatolewa kwa siku tisa mkoani humo.
"Kampeni hiyo ni jawabu kwa wale wenye changamoto juu ya sehemu ya kupata haki zao, kwa maana hiyo hilo ndio jawabu ya maswali yenu, muitumie vyema ili kupata haki zanu," amesema Mattar.
"Changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni migogoro ya ardhi, ," amesema bila kutaja idadi ya migogoro hiyo.
Hata hivyo, hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Rashid Msaraka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu migogoro ya ardhi, alisema katika ukanda huo pekee kuna zaidi ya migogoro 1,000 ambayo waathirika wakuu ni wazee.
Akitoa salamu za Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Makamu wa rais wa chama hicho, Jambia Said Jambia amesema kampeni hiyo ina dhamira ya kutoa haki bila kujali jinsia wala kabila.
Amesema, chama hicho kinaunga mkono juhudi za kutoka msaada huo kwani hawawezi kupata bila ya kusimamiwa na sheria.
Ameeleza kuwa, hatua hiyo imewafanya wananchi kuwa na sauti juu ya kupata haki zao, hivyo watoe ushirikiano ili kupata jamii yenye haki, usawa na uwajibikaji.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mansura Kassim amesema kampeni hiyo sio tu kutoa msaada wa kisheria, bali pia itatoa elimu ya sheria na kutatua migogoro ya ardhi.
Ameeleza kuwa msaada wa sheria sio zawadi ni haki ya kila mtu kupatiwa msaada ili kupata haki zao za msingi.
" Waziri wa wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman amesema kampeni hiyo ni mwarobaini kwa wote wenye matatizo ya sheria ikiwemo migogoro ya ardhi na wafanyakazi.
"Katika mkoa huu kesi nyingi ambazo zinaongoza ni migogoro ya ardhi hivyo wananchi mutoke nyumbani kufika hapa kupata msaada wa sheria," amesema Haroun.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania Bara, Franklin Rwezimula amesema mategemeo yao ni wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata haki zao.