Makundi maalumu wawekewa akaunti Mfuko wa Bima ya Afya Zanzibar

Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman akizungumza Barazani wakati akihoji mpango wa Serikali kuyasaidia makundi maalumu na watu wenye ulemavu.
Muktasari:
- Serikali yasema imekuwa ikitambua na utoaji wa ithibati kwa watu wanaotaka kuwapatia bima ya afya watoto wanaowalea.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (ZMZ) kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (ZHSF) imeweka akaunti maalumu ya usawa, itakayosaidia kuimarisha shughuli za upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalumu, zikiwemo familia zinazowatunza watoto wenye ulemevu.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Athanas Paul ameeleza hayo leo Juni 6, 2025 barazani, alipojibu swali la mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman.
Dk Mohamed aliuliza kuhusu msaada unaotolewa na Serikali kwa familia zenye watoto wenye ulemavu wenye mahitaji maalumu, akihoji ni lini Serikali itakuja na mpango wa kuwapatia bima ya afya familia zinazowatunza watoto wenye ulemavu ili kupunguza changamoto zao.
Mwakilishi huyo pia ametaka kujua idadi kamili ya watoto hao.
Dk Mohamed amesema ripoti mbalimbali zinaonyesha watoto wenye ulemavu wanakabiliwa na ukosefu wa aina mbalimbali za mahitaji, ikilinganishwa na wasio na ulemavu.
Akijibu swali hilo, Naibu waziri amesema: “Kwa kuwa suala la afya ni la msingi na ni sehemu ya uhai wa mwanadamu, Serikali kupitia Mfuko wa Bima ya Afya imeweka akaunti ya usawa itakayosaidia kuimarisha shughuli za upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalumu.”
Amesema wizara imekuwa na jukumu la utambuzi na utoaji wa ithibati kwa watu wanaotaka kuwapatia bima ya afya watoto wanaowalea.
Lengo la kufanya hivyo, amesema ni kuwezesha kila mtu kupata huduma kwa ustawi wa afya zao na kuhuisha maisha.
Kuhusu idadi ya watoto wenye ulemavu Zanzibar, Naibu Waziri, Anna amesema kwa sasa hakuna taarifa rasmi zilizofanywa kuhusu idadi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya watu wenye ulemavu 169,944 sawa na asilimia 7.54 ya Wazanzibari wote.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, bado hakuna uchambuzi rasmi ambao umefanywa wa kutambua idadi ya watoto wenye ulemavu kwa mujibu wa sensa hiyo.
Kutokana na changamoto hiyo, Naibu Waziri amesema Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu limeomba kufanyiwa uchambuzi wa taarifa za sensa na nyingine za utambuzi wa watoto.
Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Dimani, Mwanaasha Khamis Juma amehoji hatua zinazochukuliwa na wizara kwani watoto wenye mahitaji maalumu wanakumbana na changamoto za kipekee ukiwemo ubaguzi na unyanyasaji.
Naibu Waziri, Anna amesema Serikali ina nyumba kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambayo ipo Mazizini na wanalelewa humo.
Amesema kuna zaidi ya wazazi 90 wanaojitolea kuwalea watoto hao ambao kila mwezi Serikali hutoa fedha kuwasaidia. Hata hivyo, hakutaja kiwango kinachotolewa kwa wazazi hao.