Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndio kitakachomaliza urasimu, migogoro ya ardhi Zanzibar

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali akionyesha kanuni za uhaulishaji wa ardhi wakati wa kuzizindua Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kanuni hizo, maeneo ambayo hayataruhusiwa kufanyiwa uhaulishaji ni pamoja na mabonde, wakfu, mito, vyanzo vya maji na umeme.

Unguja. Wakati Zanzibar ikizindua kwa mara ya kwanza kanuni za uhaulishaji wa ardhi, hatua hiyo inatajwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya ardhi na kuondoa urasimu uliokuwa ukifanywa na watendaji.

Pamoja na hayo, pia itapunguza muda na mchakato mrefu kwa wananchi kwasababu shughuli zote za uhaulishaji, ukodishwaji na kutoa hati zitafanywa sehemu moja tena kwa njia ya kilektroniki.

Awali kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na Bodi ya uhaulishaji na kamisheni ya ardhi tena kwa sheria mbili tofauti.

Akizungumza wakati wa kuzindua kanuni hizo Mei 3, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhaza Gharib Juma amesema awali kulikuwa na mwongozo wa uhaulishaji ambao haukuwa na nyenzo kisheria na ulikuwa ukidumu kwa miezi sita tu.

Amesema hatua hii hiyo itapunguza urasimu uliokuwapo awali kwani kipindi cha bodi ya uhaulishaji ilikuwa ikitoa cheti ambacho kilikuwa kinadumu kwa miezi sita.

“Mtu ambaye alifanyiwa uhaulishaji alitakiwa kuanza mchakato wa kutafuta hati na kupimiwa na bodi ilikuwa chini ya wizara sasa ikaonekana mamlaka hizi mbili zipo pamoja lakini zinafanya kazi tofauti na hali hii ilikuwa inaongeza urasimu kwa watu wanaofanya uhaulishaji na upimaji na kupatiwa hati kwahiyo, ikavunjwa,” amesema.

Akitaja sababu ya kupunguza migogoro hiyo, Katibu Mhaza amesema tayari kupitia kanuni hizo yameanishwa maeneo ambayo yanafaa kufanyiwa uhaulishaji na maeneo ambayo hayafai kufanyiwa.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, maeneo ambayo hayafai kuahulishwa ni pamoja na mabonde, wakfu, mito, vyanzo vya maji na umeme.

“Kanuni hii kwa namna moja ama nyingine itaturahisishia utendaji wa kazi na pia itawarahisiahia wananchi kupimiwa, kuhaulishiwa na kupewa hati kwa wakati mmoja,” amesema

Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Bakari amesema maeneo hayo yaliyotajwa na kanuni hayatahaulishwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwasababu umiliki wenyewe utakuwa na mashaka maana hayaruhusiwi kujengwa kitu chochote.

Amesema, Zanzibar kwa kiasi kikubwa ardhi yake inamilikiwa na watu ama taasisi mbalimbali kwahiyo ardhi itapatikana kupitia uhaulishaji kutoka kwa anayemiliki kwasasa kwenda kwa mtu mwingine kwani ardhi hata kama haijapimwa lakini inamilikiwa na watu ama taasisi.

“Asiyekuwa na haki ya kumiliki ardhi ataipata kwa njia ya uhaulishaji ni moja ya shughuli muhimu sana katika usimamizi wa ardhi na bahati mbaya sana hatukuwa na kanuni yoyote iliyokuwa inatuongoza katika kufanya shughuli hizi,” amesema Bakari.

Amesema kupatikana kwa kanuni hizo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi kwasababu itashirikisha viongozi wa taasisi mbalimbali wakiwemo masheha na wakuu wa wilaya kwani wao hususani maeneo ambayo hayajapimwa wana uwezo mkubwa kubaini uhalali wa mmiliki.

Hata hivyo, maeneo ambayo yameshapimwa na kutolewa nyaraka hawatashiriki katika hatua za uhaulishaji kwasababu tayari kamisheni na wizara wanazo taarifa za kutosha kuhusu maeneo hayo.

Pia, kanuni hizo zitasaidia kuwaibua wanaoleta ubabaishaji hivyo kwani kutakuwa na fomu maalumu ambazo zitathibitishwa na masheha na wakuu wa wilaya kwenye maeneo husika kabla ya mwombaji kuiwasilisha kamisheni ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali amesema asilimia 80 za kazi za kamisheni ya ardhi ni uhaulishaji wa ardhi hivyo mwongozo huo utasaidia kupuguza changamoto kubwa ikiwemo migogoro ya ardhi.

“Tunaamini hata wale watu wajanjawajanja watakwenda kukwama katika kanuni hizi, kwahiyo kila mmoja anayehusika basi ikatusaidie, siyo tunatunga kanuni au miongozo halafu haifanyi vizuri kwa hiyo tunapaswa zile changamoto ambazo zimetajwa zimalizike,” amesema Waziri Rahma.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, changamoto kubwa ilikuwa urasimu, “Kuna watu walikuwa wakija wanasema wana miaka mitatu wanaomba lakini hawapatiwi.”

Waziri amesema kilichokuwa kinaleta shida ni kazi hizo kufanywa na mamlka mbili bodi ya uhaulishaji ilikuwa inatumia sheria yake ya mwaka 1994 na kamisheni ya ardhi ilikuwa ikitumia sheria yake namba sita ya mwaka 2015 kwahiyo vitu vilikuwa ni tofauti huku kazi zikifanana.

Amesema kanuni hiyo ya pili ikitanguliwa na ile ada na tozo za ardhi, itapunguza malalamiko ya wananchi na wawekezaji

Amesema kumekuwapo na malalamiko mengi kwa kamisheni ya ardhi hivyo wanapaswa kushika kasi kubwa ili wananchi wafanikishe shughuli zao.

Mwenyekiti wa masheha Wilaya ya Kati Unguja, Ali Yusuph Mussa amesema suala la ardhi ni changamoto kubwa hivyo matatizo yanayowakabili kwenye ardhi yataondoka ambayo yanajitokeza mara kwa mara.

“Hili jambo lilikuwapo lakini halikuwa na kanuni kwahiyo kanuni hizi tukisimamia na kutekeleza yataondoka, na itaondosha hofu ya wananchi kama kulikuwa na ubabaishaji maana kila mmoja atapata haki yake kwa njia iliyowazi,” amesema.

Naye Sheha wa Shehia ya Kikwajuni Juu, Asha Ali Ali amesema uhaulishaji ndio umiliki wenyewe na kuna baadhi ya ardhi hazina uhaulishaji kwa hiyo itasaidia kupatikana kwa umiliki halali.

“Kuna wavamizi wa ardhi sio zao wanajimilikisha na kisha kuziuza kwa watu zaidi ya watatu kwa hiyo hii itazuia hilo hata umiliki wa kuuzia mara mbili, hata lawama zitaondoka,” amesema Sheha Asha.