Babu Duni ajitoa kinyang’anyiro cha uenyekiti ACT, amuunga mkono Othman

Aliyekua mgombea nafasi ya uenyekiti Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji (kushoto) akipongezana na mpinzani wake Othman Massoud ambaye ni mgombe nafasi hiyo mara baada ya kutangaza leo rasmi na kujiondoa. Picha na Muhammed Khamis
Muktasari:
- Mgombea nafasi ya uenyekiti chama cha ACT Wazalendo Juma Duni Haji na mgombea nafasi makamu mwenyekiti Zanzibar, Hijja Hassan Hija wameamua kujiondoa kwenye kinyanganyiro hicho.
Dar es Salam. Siku moja kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti wa ACT Wazalendo, mgombea anayetetea nafasi yake, Juma Duni Haji ameamua kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono mshindani wake pekee, Othman Masoud Othman.
Duni maarufu kama Babu Dunia amesema sababu ya kufanya hivyo ni nia njema ya ujenzi wa chama, hatua ambayo ambayo imekuwa siku moja baada ya kunukuliwa akilalamikia hujuma.
Babu Duni amejiondoa leo Machi 4, 2024 wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya ACT - Wazalendo katika ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Babu Duni alikuwa akilalamikia hujuma za watu waliokuwa wanamshinikiza ajiondoe kwa kuwa ni mzee na kitendo cha wenyeviti kadhaa wa mikoa kumchukulia fomu mshindani wake, kitendo ambacho Kimeelezwa na msimamizi wa uchaguzi, Joram Bashange kuwa hakikatazwi.
Hata hivyo, leo, Babu Duni amesema amelazimika kujiondoa baada ya kutafakari kwa kina akijua kuwa chama hicho kina malengo makubwa ya kushika dola, hivyo kubaki kwake bila shaka kungeleta madhara katika chama hicho.
Amesema amefanya uamuzi huo yeye mwenyewe bila kutaka wala kutafuta ushauri wa mtu yoyote na ndiyo maana hata familia yake haifahamu jambo hilo.
“Nimeamua kujiondoa kuweka heshima kwenye chama kwa sababu tuna muda mfupi kuelekea kwenye uchaguzi, hatuhitaji msuguano,” alisema.
Sambamba na hilo, Babu Duni amewataka viongozi wakuu wa chama hicho na watakaochaguliwa kutowatenga kabisa wale wote ambao wamekuwa wakimuunga mkono kwenye kampeni zake.
Wakati huohuo, mgombea mwingine aliyejiondoa kwenye uchaguzi huo ni Hija Hassan Hija aliyekuwa anagombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar.
Kupitia barua yake iliyosomwa na Katibu Mkuu, Ado Shaibu, Hija amesema haoni sababu ya kuendelea kuwa mgombea kwenye nafasi hiyo.
Shaibu amesema kwa masilahi mapana ya chama chao, ameamua kumwachia Ismail Jussa kuwa mgombea pekee ambaye atamuunga pia mkono.
Jussa sasa atakuwa mgombea pekee kwenye nafasi hiyo.
Hadi sasa nafasi ambayo imebaki kuwa na wagombea wawili ni Kiongozi wa Chama (KC) ambao ni Mbarala Maharagande na Dorothy Semu.
Baada ya taarifa hiyo, Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe amesema wanaheshimu uamuzi wa kujitoa wa Babu Duni.
Amesema chama hicho kitaendelea kumuenzi na kumtunza kiongozi huyo mwenye historia kubwa kwenye siasa za mapambano Tanzania.
“Sisi chama cha ACT Wazalendo ni waumini wakubwa na kuheshimu haki za binadamu an ndio maana tumeanza kukuenzi tangu ukiwa hai leo, kila mjumbe wa kamati kuu anataja jina lako kwa kuupa jina lako ukumbi wetu, asante sana,” amesema.
Zitto amesema chama hicho hakitawaadhibu wale wote waliokuwa wakimuunga mkono kiongozi huyo na watachukulia kuwa sehemu ya demokrasia.