Vigogo ACT- Wazalendo wapishana kurejesha fomu

Makamu Mwenyekiti ACT- Wazalendo, Zanzibar, Othman Massoud Othman leo Jumamosi, Februari 24, 2024 amerejesha fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika Machi 5 na 6, 2024 jijini Dar es Salaam. Picha na Muhammed Khamis
Muktasari:
- Wakati pazia la kuchukua na kurejesha fomu likifungwa leo, vigogo wanaowania nafasi za juu wamekuwa wakipishana katika ofisi za ACT- Wazalendo kwa ajili ya kurejesha fomu zao.
Dar es Salaam. Pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo uenyekiti wa chama cha ACT- Wazalendo, linafungwa leo Jumamosi, Februari 24, 20204.
Tayari baadhi ya vigogo wanaowania nafasi za juu za uongozi wameanza kupishana kurudisha fomu hizo kuanzia jana, Februari 23, 2024 katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam na Vuga, mjini Unguja.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea wanarudisha fomu hizo katika ofisi za mikoa, kama ilivyokuwa kwa Dorothy Semu anayewania nafasi ya Kiongozi wa Chama (KC), anayerudisha fomu katika ofisi za ACT - Wazalendo mkoani Kilimanjaro, huku mpinzani wake, Mbarala Maharagande (Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu ACT- Wazalendo) akirejesha katika ofisi za Magomeni.
Wagombea wengine waliorudisha fomu ni Ismail Jussa anayewania umakamu uenyekiti Zanzibar na Isihaka Mchinjita (umakamu uenyekiti bara), ambaye katika nafasi hiyo yupo peke yake hadi sasa.
Hata hivyo, Jussa aliyewahi kuwa mwakilishi wa Mji Mkongwe Zanzibar atapambana na Hija Hassan Hija aliyechukua fomu jana kuwania nafasi hiyo, inayoshikiliwa na Othman Masoud Othman.
Kama ambavyo alivyochukua fomu juzi, Jussa alisindikizwa na mpambe wake, Mansour Yusuf Himid na leo pia wakati akirejesha ameambatana na mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mshauri wa Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu).
Mwingine ni Othman Masoud Othman anayewania uenyekiti wa ACT- Wazalendo amerejesha fomu. Ikumbukwe, Othman alichukuliwa fomu na wenyeviti na makatibu wa ACT- Wazalendo wa mikoa 27 ya chama hicho Tanzania Bara na Zanzibar waliosema ni wakati muafaka kwa kiongozi huyo kushika nafasi hiyo.
Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, atachuana na Juma Duni Haji aliyerejesha fomu jana, huku akisema uchaguzi kwenye chama hicho utapita na watabaki kuwa walimu wa demokrasia nchini kwa vyama vyote.
Duni maarufu kama 'Babu Duni' anayetetea nafasi hiyo, amesema mapambano kwenye chama hicho kila chaguzi si jambo geni na limeanza hata uchaguzi uliopita, pale Jussa alipopambana na Zitto Kabwe (KC) kuwania nafasi ya Kiongozi wa Chama.
‘’Kwa nini leo hili langu lionekane kuwa ajabu, wakati ni utaratibu wa kidemokrasia kwenye chama chetu?
"Wakati tunajiunga na chama hiki kutoka CUF, tulikikuta chama kidogo, lakini wote kwa pamoja tulitumia nguvu na muda kukijenga na sasa kimeweka safu ya uongozi nchi nzima," amesema Duni.
Uchaguzi wa Kiongozi wa Chama, uenyekiti na umakamu utafanyika kati ya Machi 5 na 6 katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ukitanguliwa na mdahalo wa viongozi utakaofanyika Machi 4.
Pia Sendwe Ibrahimu na Yassin Mohamed (anatetea) wanaowania uenyekiti wa ngome ya wazee ni miongoni mwa wagombea waliorudisha fomu na wa watachuana na Ahmad Matambara na Idsam Mapande katika uchaguzi utakaofanyika Machi mosi.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Uchaguzi ACT- Wazalendo, Mohammed Massaga amesema hadi mgombea anarejesha fomu anakuwa amekidhi vigezo vya kuilipia fomu na ada ya uanachama miezi 12 pamoja na mdhamini ambaye ni katibu wa tawi analotoka mgombea husika.
"Wakishamaliza hayo mambo matatu, basi wanarejesha fomu zao, isipokuwa kwa ngome ya wazee na vijana kuna masharti ya ziada ikiwemo kuambatanisha nyaraka zinazothibitisha umri wao sahihi," amesema Massaga.
Baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu mchakato ulioanza Februari 14 kukamilika, kuanzia kesho Jumapili hadi Februari 28, 2024 timu ya uchaguzi ya ACT- Wazalendo, yenye watu tisa itajifungia kufanya uhakiki wa nyaraka za wagombea hao, kabla ya kuwateua.