Joto la uchaguzi ACT Wazalendo lazidi kupanda, siku zakaribia

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo akiwa na wafuasi wanaomuunga mkono muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Muktasari:
- Februari 29, 2024 utafanyika uchaguzi wa ngome ya vijana ya ACT Wazalendo utakaomchagua mwenyekiti na makamu wake, tayari wagombea wanne wameshachukua fomu za kuwania kiti hicho.
Dar /Unguja. Wajumbe 117 wa mkutano mkuu wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wataamua nani awe mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa ngome hiyo katika kinya'nga'nyiro chenye ushindani kitakachofanyika Februari 29, 2024.
Uchaguzi wa ngome wa safari hii unatajwa kuwa na ushindani mkubwa tofauti na mwaka 2020 kutokana na aina ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, ambayo kiongozi wake anaingia moja kwa moja katika vikao vya juu vya chama hicho.
Hadi leo Jumanne, Februari 20, 2024 wagombea wote wanne Abdul Nondo, Julius Massabo, Ruqaiya Nassir na Petro Ndolezi wameshachukua fomu za kuwania kiti hicho wakiambatana na wagombea wenza. Tayari wagombea hao wameshaanza kufanya kampeni za kusaka kura zitakazowawezesha kuibuka kidedea.
Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Nondo alipata ushindi mwembamba dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Witson Mogha ambaye baada ya matokeo hayo alitimkia NCCR Mageuzi, kabla ya kurejea tena ACT Wazalendo. Katika mchakato huo Massabo alishika nafasi ya tatu.
Uchaguzi wa safari hii utakuwa mchuano mkali kwa sababu kati ya wagombea wanne waliojitokeza, watatu wanatoka mkoa wa Kigoma, ukimuondoa Ruqaiya anayetokea Mafia, mkoani Pwani. Hivyo, vijana hawa wanaojuana na wanajua udhaifu na uimara wa Nondo anayetetea nafasi yake kwa mara nyingine.
Pia, uchaguzi wa mwaka huu, ngome hiyo inawakutanisha wagombea waliowahi kuwa katika uongozi wa Nondo kwenye sektararieti ya ngome kabla ya mwenyekiti huyo kuwaondoa kwa nyakati tofauti baada ya kutofautiana nao kimtizamo.
Lingine linalofanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani, ni aina wagombea kuwa maarufu ndani ya chama hicho ambapo walishawahi kutia nia na kugombea nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge, sambamba na kuaminiwa kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe aliyewateua kuwa mawaziri vivuli.
Februari 29, wajumbe wa mkutano mkuu wa ngome watakuwa na kibarua pevu cha kuwachagua mmoja kati yao atakayepeperusha bendera ya uenyekiti ngome hiyo kwa miaka mitano.
Mbali na uchaguzi wa ngome ya vijana, ushindani mwingine utakuwa katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, itakayowakutanisha vigogo; Juma Duni Haji anayetetea kiti hicho na Othman Masoud Othman ambaye ni makamu mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar.
Mchuano mwingine itakuwa katika nafasi ya Kiongozi wa Chama (KC) unaowakutanisha Dorothy Semu na Mbarala Maharagande. Pia, nafasi ya uenyekiti ngome ya wanawake inayowaniwa na Severina Mwijage na Janeth Rithe ambao uchaguzi wao utakuwa Machi 2, 2024.
Nondo achukua fomu
Leo Februari 20, 2024, Nondo alitinga ofisi za makao ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, huku akijivunia masuala mbalimbali aliyoyatekeleza katika kipindi cha mwaka 2020/24 ikiwemo kuitangaza ngome na kuwa chombo cha utetezi wa haki za vijana nchini.
Nondo amechukua fomu hiyo akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Nassor Ahmed Marhun kutoka Zanzibar. Baada ya kuchukua fomu, Nondo ambaye ni Waziri Kivuli wa Kazi, Vijana na Ajira, amesema vipaumbele vyake vitakuwa saba.
kabla ya kuvitaja vipaumbele, Nondo alianza kueleza mafanikio katika uongozi wake wa miaka takribani mitatu, akisema amefanikiwa kuitangaza Ngome hiyo kwa kiasi kikubwa na kuifanya itambulike kama taasisi nyingine za vijana.
“Nimekuja kuchukua fomu, wenzangu wameshachukua na kusema watafanya nini wakipata ridhaa, sipaswi kusema nitafanya nini? Ninaamini kusema nitafanya nini ni jambo jepesi na mtu yeyote ana uwezo wa kulitamka.
“Jambo la msingi ni kusema kwanini uaminiwe, katika uongozi wangu hadi hapa tulipofikia huwezi ukataja jumuiya tatu za vijana pasipo kuitaja ngome ya ACT Wazalendo,” amesema Nondo anayetetea nafasi hiyo.
Nondo amesema katika utekelezaji wa majukumu yake amefanikiwa kusemea uhuru wa vyombo vya habari, demokrasia na haki za binadamu kazi aliyodai aliifanya kikamilifu, hivyo wajumbe wa mkutano mkuu wa ngome wana kila sababu ya kumchagua Februari 29, kuwa kiongozi wao.
“Ngome ya vijana ya ACT Wazalendo ndicho kilikuwa chombo pekee cha kupigania haki za vijana hasa masuala ya ajira, kunyanyaswa na vyombo vya dola, tulikuwa mstari wa mbele kusemea changamoto hizi,” amesema Nondo.
Baada ya maelezo hayo, Nondo, akataja vipaumbele yake saba atakavyovitekeleza kwa mwaka 2024/29 endapo akitetea nafasi hiyo akisema ataanza kuongeza wigo wa ngome hiyo kwa kufungua matawi ya nje ya nchi kupitia daispora. Pia, atahamasisha vijana kujitokeza kugombea, kupiga kura na kulinda ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
“Nitatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo na ujasiri wa kiongozi, viongozi wote wa ngome waliochaguliwa nchi nzima, tutaongeza wigo wa mapato ili kuimarisha utendaji kazi na ujenzi wa taasisi hii.
“Tutaendelea kutetea maslahi na madai ya vijana kwa Serikali na kwenye vikao vya uamuzi vya chama, ili kulinda maslahi yao, nitahakikisha nadumisha na kuimarisha zaidi mtandao wa ngome kote nchini na kufanya ziara ya mara kwa mara,” amesema Nondo.
Ndolezi arejesha fomu
Wakati Nondo akieleza hayo, mgombea mwenzake, Ndolezi leo Februari 20, 2024 amerejesha fomu katika ofisi ya chama hicho, Vuga Mjini Unguja na kusema endapo atafanikiwa kushika nafasi hiyo ataifanya ngome hiyo kuwa kimbilio la vijana wote Tanzania.
Ndolezi ambaye ni Waziri Kivuli wa Ardhi, amesema kwa muda mrefu vijana wa Tanzania wamekosa jukwaa sahihi la kueleza shida zao na yale yote, yanayowakabili hususani changamoto za ukosefu wa ajira pamoja na fursa muhimu.
Amesema hali hiyo ndiyo iliyomsukuma kuwania nafasi hiyo akiamini kuwa vijana wa chama ACT- Wazalendo watafanya uamuzi sahihi kumchangua, ili kuwa kiongozi mpya wa ngome kwa miaka mitano ijayo.
“Nitatumia muda wangu wote kuhakikisha Tanzania inapata baraza la vijana lilikosekana kwa miaka yote licha ya kuwa na sera na kanuni kwa miaka tisa tangu kupitishwa kwa sheria.
“Hili ni jambo la kushangaza sheria na sera zote zipo, lakini cha ajabu baraza hilo halipo hadi sasa na ni kwa sababu vijana wamekosa watu muhimu wanaoweza kuwapambania,” amesema.
Mgombea mwenza wa Ndolezi, kutoka Zanzibar, Malik Juma Mohamed amesema wakipata ridhaa watahakikisha wanaongeza idadi kubwa ya vijana kwenye chama hicho, ili kusongeza mbele harakati za kisiasa hususani chama cha upinzani.