ACT Wazalendo waanza mchakato kura za maoni

Chama cha ACT Wazalendo kimeanza mchakato wa upigaji wa kura za maoni ili kuwapata wagombea wa nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani utakaofanyika Oktoba 2025.
Muktasari:
- Mchakato huo unatarajia kukamilika Julai 5 mwaka huu baada ya kuwapata viongozi watakaopelekwa katika sekretarieti ya chama kwa ajili ya kupitishwa na kukiwakilisha chama katika ngazi mbalimbali.
Unguja. Chama cha ACT Wazalendo kimeanza mchakato wa upigaji wa kura za maoni ili kuwapata wagombea wa nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani utakaofanyika Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mchakato huo kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja Juni 26, 2025, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani amesema baada ya kukamilika mchakato huo wa kura ya maoni kwa majimbo yote chama kupitia kamati kuu itakaa na kuyapitia na kuyajadili majina ya wagombea waliochaguliwa.
Amesema kuwa baraza kuu litaheshimu maoni ya wanachama kuhusu majina ya wagombea waliopigiwa kura katika mchakato wa kura za maoni ili kumpata mgombea sahihi.
“Huu ni utaratibu wa kura za maoni hatua itakayofuata tutaenda katika sekreterieti ya taifa kwa ajili ya kuandaa vikao, tutaenda kwenye kamati maalumu na kamati kuu kwa mujibu katiba ya chama chetu ndio chombo kinachofanya uamuzi wa mwisho wa nani awe ndio mtetezi wa wananchi kupitia chama,” amesema Bimani.
Hata hivyo, amesema ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ni mzuri wamejitokeza kugombea nafasi hizo za uongozi.
Bimani amewataka wagombea watakaopitishwa na ambao hawatapata nafasi ya kupitishwa katika chama kuwa wagombea, kubaki kuwa wamoja na kumuunga mkono ambaye atapitishwa na chama kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu.
Naibu Katibu wa Haki za Binadamu wa chama hicho, Pavu Juma Abdallah amesema mchakato huo wa kura za maoni ni utekelezaji wa misingi ya haki za demokrasia.
Pavu amesema uchaguzi wa kura za maoni umekwenda vizuri bila ya uwepo viashiria vya vurugu au uvunjifu wa amani.
“Nimefurahi kuona wanawake wengi wamejitokeza kugombea nafasi za uongozi kwa ajili ya uchaguzi mkuu imani yetu kuwa chama kitawapitisha kupitia ushindi waliupata katika kura za maoni,” amesema Pavu.
Chama hicho bado kinaendelea na uchaguzi huo wa kura za maoni kwa majimbo mengine ya Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.