11 wanusurika kifo nyumba ikiungua moto Pemba

Baadhi ya masalia ya vitu vilivyoungua baada ya nyumba kuwaka moto Shehia ya Wawi Chakechake Pemba
Muktasari:
- Ni baada ya moto kuwaka na kuunguza vitu vyote vya ndani bila kuokolewa kitu kisiwani Pemba.
Pemba. Watu 11 wa familia moja wilayani Chakechake Mkoa wa Kusini Unguja wamenusurika kifo baada ya nyumba yao kuungua moto.
Tukio hilo lililotokea eneo la Wawi Aprili 18, 2025 saa 3:00 usiku wakati familia hiyo ya Khamis Haji ikiwa ndani imejipumzisha. Hata hivyo licha ya moto huo kuunguza vitu vyote vilivyokuwamo ndani ya nyumba, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha katika tukio hilo ambalo chanzo chake hakijajulikana.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wanafamilia wamesema tukio hilo lilitokea wakati wakiangalia televisheni ghafla walisikia kishindo kikubwa juu ya bati kisha wakashtuka kuona moto ukaanza kuwaka.
Ali Mohamed Salum ni mmoja wa manusura wa tukio hilo amesema: “ Baada ya kuona moto unawaka tulitoka nje na wananchi wakaanza kujitokeza tukaanza jitihada za kuuzima lakini ilishindikana mpaka kilipokuja Kikosi cha Zima Moto na uokozi ndio walifanikiwa kuuzima lakini tayari vitu vilikuwa vimeshateketea,”
Amesema baadhi ya vitu vilivokuwemo ndani ni vitanda makabati magodoro na TV, friza pamoja na nguo zote hivyo wanaomba kusaidiwa makazi kutokana na janga hilo.
‘’Kwa kweli hatujui thamani ya vitu vilivyoungua maana tumeona vitu vyote ndani hakuna kinachobakia hakuna kodoro wala kitanda hivyo tunaomba tuangaliwe kwa jicho la huruma kutusaidia,” amesema Mohamed.
Mwanafamilia mwingine Asha Khamis Juma amesema mbali ya kuungua kwa vitu hivyo lakini kuna na vyeti vya kuzaliwa vya wakaazi wa nyumba hiyo pamoja na vitambulisho vyote vimeteketea kwa moto.
Amesema hiyo ni hasara kubwa kwao hivyo anaiomba Serikali kuishika na wadau wengine kuisaidia familia hiyo katika kuwasaidia ili kuwapa faraja katika kipindi hichi kigumu.
“Kuna vyeti vya kuzaliwa vitambulisho vya ukaazi vyote vimeteketea kwa moto hivyo tunaomba Serikali na jamii itushike mkono kuona vitu vyote hivyo vinapatikana,” amefafanua.
Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya amefika na kuifariji familia hiyo huku akiomba kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu ambacho Serikali inafanya kila juhudi kuona inawasaidia.

Amesema Serikali kwa ujumla imeguswa na tukio hilo na kueleza kuwa Serikali itawashika mkono kwa kutafuta njia za kuwasaidia wanafamilia hao.
‘’Serikali ya Wilaya ya Chakechake tumeguswa na tukio hilo tunaiomba familia ya Mzee Khamis kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu tutakuwa na nyinyi kila hatua,” amesema Mgeni.
Licha ya chanzo cha tukio hilo bado hakifahamika, Mratibu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Kisiwani Pemba, Khamis Arazaki amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika matumizi ya nishati ya umeme kwa kufanya maboresho kwenye nyumba zao.
Amefafanua kuwa mara nyingi wananchi hawana utaratibu wa kufanya maboresho kwenye nyaya za umme hivyo kuwa sehemu ya kusababisha madhara ya moto.