Wakazi Tarime waomba Serikali kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Kenani Kihongosi mjini Tarime.
Muktasari:
- Wakazi hao wamesema barabara hizo zimejaa mashimo na maji hivyo kushindwa kupitika kwa magari, pikipiki na watembea kwa miguu, na kuomba zijengwe kwa kiwango cha lami ili kupata suluhisho la kudumu.
Tarime. Wakazi wa eneo la Bomani, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukarabati barabara za mitaa ambazo zimeharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, hali inayosababisha kero na usumbufu kwa watumiaji wa barabara hizo.
Wakazi hao wamesema barabara hizo sasa zimegeuka kuwa kikwazo kikubwa kutokana na kujaa mashimo na maji, jambo linalofanya kushindwa kupitika kwa urahisi kwa vyombo vya moto na hata watembea kwa miguu.
Akitoa taarifa ya shina namba tatu tawi la Bomani kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, Mwenyekiti wa shina hilo, Ibrahim Hamisi amesema uchakavu wa barabara hizo ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
“Tunaomba barabara zetu zikarabatiwe ili ziweze kupitika kwa vyombo vya moto na watembea kwa miguu kwa sababu kwa sasa hazipitiki,” amesema Hamisi.
Mkazi mwingine, Enos Mwita amesema ubovu wa barabara hizo umesababisha hasara kwa wamiliki wa vyombo vya moto kutokana na kuharibika kwa magari na pikipiki wanapojaribu kuzitumia.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tarime, Mei 15,2026.
Kwa upande wake, Helena Mwita amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo ya kila msimu wa mvua, ni muhimu barabara hizo kujengwa kwa kiwango cha lami ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kupunguza kero ya mara kwa mara.
“Hii kero ya barabara kuharibika kila msimu wa mvua tumechoka nayo, tunaomba Serikali itenge bajeti ya kutosha zijengwe kwa kiwango cha lami ili tupate suluhisho la kudumu,” amesema.
Akizungumza na wanachama wa shina hilo, Kihongosi amesema ni wajibu wa CCM kusimamia Serikali kuhakikisha inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/30, ambayo inalenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema Serikali ya CCM inalenga kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Ametaja barabara ya Tarime–Nyamwaga kuwa miongoni mwa miradi inayotekelezwa, akisema tayari mchakato wa ujenzi umeanza na utekelezaji wake utaanza muda si mrefu.
“Nimepita kwenye barabara hii nimeiona ilivyo, habari njema ni kwamba Serikali imeshachukua hatua na muda si mrefu ujenzi utaanza,” amesema Kihongosi.
Awali, akiwa Butiama alikozuru kaburi la Baba wa Taifa, Kihongosi aliwataka viongozi vijana wa CCM na Serikali kuepuka kiburi cha madaraka na badala yake kujifunza uongozi bora kupitia misingi iliyowekwa na hayati Julius Nyerere.
Amesema Nyerere alisimamia misingi ya uongozi unaojenga umoja, upendo na mshikamano, misingi ambayo inapaswa kuendelezwa na viongozi wa sasa kwa maslahi ya taifa.