Halmashauri Kuu CCM yaazimia mambo matano
Muktasari:
- Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, imeketi leo, Mei 7, 2026 na kuazimia mambo matano.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimepanga kujifanyia tathmini ili kujiboresha kiutendaji, kimuundo na kiuchumi, kuelekea kipindi kijacho cha siasa.
Mpango huo wa chama hicho tawala ni moja kati ya maazimio matano yaliyoazimiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).
Kikao hicho, kimefanyika jijini Dodoma leo, Alhamisi Mei 7, 2026 na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, maazimio mengine ni kumpongeza Rais Samia kwa kuunda Tume Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Taarifa hiyo, imeeleza NEC imefurahishwa na uamuzi wa Rais Samia kuunda tume hiyo maalumu, hatua iliyoonyesha dhamira ya kuendelea kuimarisha haki, uwajibikaji na maridhiano nchini baada ya uchaguzi uliokuwa na mijadala mikubwa kisiasa.
Wakati huo huo, NEC imeipongeza Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mohammed Chande Othman, kwa kazi iliyoelezwa kufanywa kwa weledi, uadilifu na kuzingatia sheria za ndani na viwango vya kimataifa.
Pia, CCM imeipongeza Serikali kwa hatua ambazo tayari zimeanza kuchukuliwa katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo, huku ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda amani na mshikamano wa Taifa.
Katika hatua nyingine, NEC imevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa jukumu lao la kuhakikisha hali ya utulivu inarejea haraka nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kikao hicho pia kimeunga mkono mpango wa kufanya tathmini ya kina ya CCM kwa lengo la kukiboresha zaidi kiutendaji, kimuundo na kiuchumi kuelekea kipindi kijacho cha kisiasa nchini.