Kihongozi: CCM kinaunga mkono ripoti ya Tume ya Uchunguzi
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi.
Muktasari:
- Kihongosi amesema tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kwa uhuru na weledi wa hali ya juu, akibainisha kuwa ripoti yake imelenga kuliponya Taifa
Dodoma. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amesema chama hicho kinaunga mkono Ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kiko tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa.
Kihongosi amesema tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi kwa uhuru na weledi wa hali ya juu, akibainisha kuwa ripoti yake imelenga kuliponya Taifa.
Akizungumza leo Jumatatu Mei 4, 2026 jijini Dodoma, Kihongosi amesema CCM inawashukuru Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa tume hiyo.
Amesema chama hicho kinaunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na tume na kwamba Rais tayari ameyapokea na yuko tayari kuyafanyia kazi.
“Tunawahakikishia Watanzania kuwa CCM itatoa ushirikiano wa hali ya juu na pia itawahamasisha wananchi kuunga mkono hatua hizi zinazolenga kujenga umoja, upendo na mshikamano wa Taifa,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa CCM inaamini maridhiano ndiyo njia sahihi ya kushughulikia suala hilo, akisisitiza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vurugu hizo, waliohusika na hatua stahiki za kuwawajibisha.
“Kwa mnasaba huo, Chama cha Mapinduzi kinaunga mkono hatua inayofuata ya kuundwa kwa Tume ya Upelelezi ili kubaini ukweli wa mambo yalivyokuwa. CCM iko tayari kufuata njia ya maridhiano kwa mfumo shirikishi katika ngazi zote za jamii,” amesema.
Kihongosi amesema suala la Katiba mpya ni ajenda ya CCM na limo ndani ya ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/30, akieleza kuwa Rais Samia alinadi wakati wa kampeni na kwamba mchakato huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2030.
Amesema mchakato wa Katiba mpya ulianza mwaka 2011 chini ya Serikali ya Awamu ya Nne lakini uliishia kwenye rasimu ya Katiba inayopendekezwa baada ya baadhi ya vyama vya siasa kususia.
Amesisitiza kuwa, Katiba mpya siyo suala la vyama vya siasa pekee bali linahusisha makundi yote ya kijamii, wakiwamo wananchi wasio na vyama.
Aidha, amewataka vijana wasomi kuacha kushabikia vurugu na badala yake wawe mabalozi wa kulinda amani ya nchi, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila amani.