Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ummy Mwalimu amuombea kura Samia, mgombea ubunge

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini aliyemaliza muda wake, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Ummy Mwalimu aunga mkono maamuzi ya CCM kumpitisha Makubeli, asema hana kinyongo na atahakikisha anashinda kwa kishindo Jimbo la Tanga Mjini.

Tanga. Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini aliyemaliza muda wake, Ummy Mwalimu amewataka wakazi wa Tanga kumchagua kwa kura nyingi mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan na mgombea ubunge Kassim Makubeli na madiwani wa chama hicho ili kuharakisha maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni  uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Majengo Komesho jijini Tanga, Ummy amesema kuwa maamuzi ya chama ni ya kuheshimiwa, na yeye kama mwanachama mtiifu hana budi kuyakubali kwa moyo mmoja.

Ummy amesema kuwa kutokuwa na kinyongo ni ishara ya uaminifu, uadilifu na shukrani kwa chama kilichomlea kisiasa kwa zaidi ya miaka kumi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mgombea ubunge kupitia CCM Jimbo la Tanga, Makubeli ameishukuru Kamati Kuu kwa kumpitisha kuwania nafasi hiyo na kuahidi kusimamia ujenzi wa nyumba za kuishi wauguzi katika vituo vya afya.

Amesema atasimamia kwa karibu usanifu na ujenzi wa barabara za juu (flyovers) eneo la Kwaminchi kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, pamoja na ujenzi wa madarasa na miradi mingine ya maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Ummy aliendelea kufafanua kuwa licha ya kuombwa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, kushiriki kwenye kampeni katika majimbo yote ya Mkoa wa Tanga, yeye binafsi ameomba kujielekeza zaidi katika Jimbo la Tanga Mjini.

Amesema amefanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika ushindi wa Makubeli, ambaye sasa ndiye mgombea wa CCM katika jimbo hilo.

“Niliombwa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, niungane na timu ya kampeni katika majimbo yote ya Mkoa wa Tanga. Lakini mimi nimeomba nijikite hapa Jimbo la Tanga, ili kuhakikisha kwamba Makubeli anapata ushindi wa kishindo, kwa sababu huu ni mji wangu na ni jukumu langu kuhakikisha bendera ya CCM inabaki juu,” aliongeza Ummy kwa msisitizo.

Amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Tanga kwa ujumla kuweka tofauti zao pembeni na kuungana kumpigia kura mgombea wa chama hicho, akisisitiza kuwa uchaguzi unapita, lakini mshikamano ndani ya chama ni jambo la msingi kwa ustawi wa kisiasa na maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo ya Ummy imepokelewa kwa shangwe na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi na viongozi wa CCM waliokuwepo, wengi wakimtaja kuwa kielelezo cha utii na uongozi wa mfano ndani ya chama hicho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Rajabu Abdurahman, amewaomba wakazi wa Jiji la Tanga kumpigia kura Kassim Amary (Makubeli) kuwa mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, akisema atakuwa kiendelezo wa kazi nzuri zilizofanywa na mtangulizi wake, Ummy Mwalimu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM katika jimbo hilo, Rajabu amesema kuwa Makubeli ni chaguo sahihi kwa sababu amepewa dhamana na chama kutekeleza Ilani ya CCM, ambayo msingi wake mkuu ni amani, maendeleo na mshikamano wa kitaifa.

“Makubeli ameaminiwa na Chama Cha Mapinduzi, si kwa bahati mbaya, bali kwa sababu ya uwezo wake wa kuendeleza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. Wananchi wa Tanga, nawaomba tumpe kura zetu ili aendeleze alipoishia dada yetu Ummy Mwalimu,” amesema Rajabu.

Kuhusu shughuli za maendeleo katika Jimbo la Tanga, Rajabu amesema kuwa miradi mikubwa ya kimkakati imeanza kutekelezwa, ikiwemo upanuzi wa Bandari ya Tanga, ujenzi wa viwanda, pamoja na kuimarisha sekta ya elimu kwa kujenga shule za sekondari mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Ameongeza kuwa katika sekta ya afya, Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwepo awali kwa kujenga vituo vya afya, zahanati, pamoja na kuboresha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo.

Amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, na kwamba ili yaendelee na kuimarika zaidi, ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuiamini CCM na kuichagua katika nafasi zote za uongozi.

Rajabu amewataka wana-CCM kuendesha kampeni za kistaarabu ili kuwaonyesha wapinzani kuwa CCM kina watu wema.

"Tumesema tutaongeza kujenga shule nyingine tatu za msingi, kuongeza madarasa ya msingi na Sekondari...tutatoa elimu kwa ada ya Rais," amesema Rajabu.

Amewataka wakazi wa Tanga kumchagua kwa kura nyingi Rais Samia Suluhu Hassan, Kassim Amary Makubeli na madiwani wa CCM ili kuharakisha maendeleo.