Tanzania yaongeza kasi nishati safi ya kupikia, yafikia asilimia 23.2
Anita Ringia wa Wizara ya Nishati (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wa pembeni wa Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) jijini Abu Dhabi, UAE.
Muktasari:
- Serikali imeifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa na nguzo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Abu Dhabi, UAE. Tanzania imeendelea kuimarisha jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia, huku upatikanaji wa huduma hiyo ukiongezeka zaidi ya mara tatu ndani ya miaka minne, kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano wa pembeni wa Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) uliojadili upatikanaji wa fedha kwa miradi ya nishati safi ya kupikia, Anita Ringia wa Wizara ya Nishati amesema mafanikio hayo yametokana na dhamira ya Serikali kutenga na kutafuta rasilimali kutoka vyanzo mbalimbali.
Amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa na nguzo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tanzania imeendelea kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia na matokeo yake yanaonekana wazi katika ongezeko la wananchi wanaotumia nishati hiyo,” amesema Ringia.
Kwa mwaka wa fedha 2025/26, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo usambazaji wa majiko banifu 200,000 kwa ruzuku.
Pia, mradi wa majaribio wa kulipia majiko ya umeme 480 kupitia bili za umeme kwa kushirikiana na Tanesco, pamoja na usambazaji wa mitungi zaidi ya 450,000 ya gesi ya LPG kwa bei ya ruzuku.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ni kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika zaidi ya taasisi za umma 31,000.
Utekelezaji wa mpango huo unahitaji uwekezaji unaokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni moja.
Amesema sekta binafsi imekuwa mshirika muhimu katika mafanikio hayo, ikichochewa na ongezeko la uwekezaji kutoka taasisi za kifedha za ndani zikiwemo benki za NMB na CRDB, ambazo zimeanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wajasiriamali wa nishati safi ya kupikia ili kupanua mitandao ya usambazaji nchi nzima.
Katika mkutano huo, Tanzania pia imetangaza fursa za uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia, ujenzi wa viwanda vya ndani vya kutengeneza majiko, vifaa na mitungi, pamoja na matumizi ya mifumo bunifu ya ulipaji kama PAYGO, riba nafuu na malipo kupitia bili za umeme.
Akizungumzia mchango wa kimataifa, Ringia amesema Tanzania inaunga mkono wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo ili kuziba pengo la ufadhili wa nishati safi ya kupikia, hasa barani Afrika ambako takribani watu bilioni moja bado hawana huduma hiyo.
Katika vikao vingine vya awali, wataalamu wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Imani Mruma, walieleza juhudi za Tanzania katika kuimarisha mchango wa nishati jadidifu kwenye gridi ya Taifa.
Kwa sasa, nishati jadidifu inachangia asilimia 68 ya umeme unaoingizwa kwenye gridi, huku miradi mipya ikiendelea ikiwemo mradi wa umeme wa jua wa Kishapu wa megawati 150, unaotarajiwa kuanza kuzalisha megawati 50 ifikapo Februari mwaka huu.
Vyanzo vingine vinavyoendelezwa ni pamoja na miradi ya jotoardhi katika Ziwa Ngozi (70MW), Songwe (5MW), Kiejombaka (60MW), Natron (60MW) na Luhoi (5MW).
Akifungua mkutano wa IRENA, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Gaun Singh, amezihimiza nchi wanachama kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu ili kufikia lengo la dunia la kuwa na megawati 11,000 za umeme zitokanazo na nishati jadidifu ifikapo mwaka 2030.
Mkutano wa IRENA 2026 unaongozwa na kaulimbiu ya “Powering Humanity: Renewable Energy for Shared Prosperity” (Matumizi ya Nishati Jadidifu kwa manufaa ya pamoja kwa kila binadamu).