Samia aahidi mradi wa Liganga na Mchuchuma kuanza kazi
Muktasari:
Mradi wa Chuma Liganga ni mradi wa kimkakati unaolenga kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kuzalisha madini muhimu na kuchochea ajira, uwekezaji na maendeleo ya kitaifa.
Njombe. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa Liganga na Mchuchuma uko katika hatua za mwisho na kwamba baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, mwekezaji ataanza kazi.
Samia ametoa ahadi hiyo leo Septemba 5, 2025 kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika mjini Njombe.
Mradi wa Chuma Liganga ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha uchumi wa viwanda wa Tanzania kwa kuanzisha sekta za msingi zitakazosaidia sekta nyingine katika mnyororo wa thamani.
Mradi huo unakadiriwa kuzalisha mapato ya zaidi ya Dola bilioni 1.2 za Marekani kila mwaka ambazo ni karibu Sh3 trilioni za Tanzania kutokana na uzalishaji wa madini ya Chuma, Titani, Vanadium, na Sulfati ya Alumini.
Hata hivyo, licha ya umuhimu wake, mradi huo umechelewa kuanza kazi kutokana na sababu mbalimbali zilizokuwepo ikiwamo ya ulipaji fidia kwa wananchi waliokuwa wakizunguka eneo hilo lenye utajiri wa madini.
Tayari Serikali imewalipa wananchi fidia ya zaidi ya Sh15 bilioni ili kupisha mradi huo ambao unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi siyo tu kwa wakazi wa Mkoa wa Njombe, bali pia Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni, Samia ametoa matumaini mapya ya kuanza kwa mradi huo huku akiahidi kwamba baada ya shughuli za uchaguzi, mwekezaji ataanza kazi.
"Kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma, tuko katika hatua za mwisho, mwekezaji amepatikana, tukimaliza shughuli hizi za uchaguzi, mwekezaji ataanza kazi ili vijana wetu wapate ajira katika mradi ule," amesema mgombea huyo.
Mbali na mradi huo, Samia amesema Serikali itaongeza jitihada za uwekezaji kwenye mazao ya parachichi na chai ili wakulima wanufaike na kazi zao hasa katika masoko ya nje.
Ameongeza kuwa wanakuja na kongani za viwanda katika kila wilaya ili kusaidia vijana kuongeza thamani mazao yao na kuhimili soko la ushindani.
"Tumeanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Njombe kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa parachichi zetu, na huko tutakuwa na sehemu za kuhifadhia mazao hayo ili yasiharibike na urahisi wa kuyasafirisha," ameeleza mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi.
Waeleza kazi aliyoifanya
Chifu wa Mkoa wa Njombe, Mkongwa amesema wananchi wa Njombe wamefurahi ametupatia mbolea ya ruzuku na huduma nyingine za kijamii kama vituo vya afya, shule, huduma ya maji na umeme.
Amemwombea kura Samia ili apate ushindi aendeleze kazi aliyoifanya ili watoke hapa walipo, wapige hatua mbele zaidi kimaendeleo.
"Ndugu mgombea, Mungu akusaidie upate kura kwa wingi ili ututoe hapa tulipo, tupige hatua zaidi mbele. Umetusaidia sana, tunaomba uendelee kutukumbatia sisi watoto wako wa Njombe," amesema Chifu huyo wa Mkoa wa Njombe.
Mbunge wa viti maalumu katika Mkoa wa Njombe, Rebecca Nsemwa amesema tangu ameingia madarakani, Rais Samia amepunguza vifo vitokanavyo na uzazinkutoka vifo 27 mwaka 2021 hadi kufikia vifo 22 mwaka 2024.
"Ni mengi umeyafanya hapa Njombe kwenye elimu, afya, maji na umeme. Wahenga wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, nataka niseme hanyongwi mtu na haki yake tunampatia," amesema Rebecca.
Mgombea ubunge wa Makete, Festo Sanga amesema kazi alizozifanya katika jimbo lake ndizo zimeweka imani ya wananchi hata kwake kama mgombea ubunge.
Amesema katika kipindi hicho, amejenga shule 11 huku katika jimbo hilo, hali ya upatikanaji wa maji ni asilimia 99, hivyo amefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani, kama ilivyo kaulimbiu yake.
"Kwa haya uliyoyafanya, Oktoba 29, 2025, utapata kura za kishindo. Sisi wana Makete tunakuhakikishia kwamba kura zote zitaelekea kwa wagombea wa CCM, kuanzia Rais, wabunge na madiwani," amesema mgombea huyo.
Mgombea wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swale amesema wananchi wa Lupembe wamekwenda kumshukuru kwa sababu amegusa maisha yao kwa kuwapatia huduma za afya kwenye kata ambazo hazikuwa na vituo vya afya.
Amesema katika jimbo lake, zimejengwa zahanati 17, barabara za Tarura zimechongwa na umeme umefika katika vijiji vyote vilivyopo katika jimbo lake.
"Wananchi wa Lupembe wanakushukuru kwa maelekezo yako ya kufufua zao la chai, tunaamini umishapita mambo yatakuwa shwari. Tumejipanga Oktoba 29, 2025 tunakupigia kura ushinde kwa kishindo," amesema Swale.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Wanging'ombe, Festo Dugange amesema jimbo lake halikuwa na hospitali ya wilaya na vituo viwili vya afya, lakini sasa wana hospitali ya wilaya, vituo vya afya 13 na zahanati 20.
Amesema mwaka 2021 kilikuwa na changamoto ya barabara, Serikali yake imetoa Sh37 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe, jumla ya kilomita 537 na kilomita 31 kwa kiwango cha lami.
"Wakati unaingia madarakani, vijiji 108 havikuwa na umeme, lakini sasa vijiji vyote vina umeme, kazi iliyobaki ni kufikisha umeme kwenye vitongoji 228 vilivyobaki," amesema mgombea huyo huku akiwataka wananchi kwenda kupiga kura za heshima kwa Samia.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Makambako, Daniel Chongolo amesema wamejipanga kumpatia kura za kishindo siku ya uchaguzi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.
Amesema Samia amekuwa tiba ya miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa muda mrefu ilikwama ambayo ni Maganga Matitu na ule wa Liganga Mchuchuma ambao amewalipa fidia wananchi jumla ya Sh15 bilioni.
"Kwa mapenzi makubwa, hujatuacha vijana wa Njombe, umetuamini sisi vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi, nikiwemo mimi...nikushukuru na kukuhakikishia kwamba Oktoba 29 utapata ushindi mkubwa wa heshima," amesema.
“Jah People” atia neno
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Deo Sanga "Jah People" amesema Samia amefanya kazi kubwa katika mkoa huo
"Tutafanya kazi kubwa ya kwenda kuwaomba wananchi kura za shukrani, chaguzi zilizopita Njombe iliongoza, kwenye uchaguzi ujao tunakwenda kufurika," amesema mwenyekiti huyo.
Ameonya makundi ya wagombea katika mkoa huo huku akieleza kwamba kura za maoni ndani ya chama zimekwisha, hivyo amewataka wote kuwa kitu kimoja katika kutafuta kura za mgombea urais, wabunge na madiwani.
Ameomba halmashauri ya mji wa Njombe ipandishwe hadhi na kuwa manispaa. Pia, ameomba Makambako iwe wilaya kwani taasisi zilizopo katika jimbo hilo ni wilaya.