Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitila awashukuru wananchi wa Ubungo kwa kumchagua tena

Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na wananchi wa Ubungo wakati wa hafla ya futari ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo.

Muktasari:

  • Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua tena katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akiwaomba wamuombee ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumuamini na kumchagua tena kuwatumikia katika kipindi cha pili cha miaka mitano.

Hizi ni shukrani zake za kwanza hadharani tangu ashinde katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 uliofanyika Oktoba 29, 2025 na kufanikiwa kutetea nafasi aliyoshinda kwa mara ya kwanza mwaka 2020.

Profesa Kitila ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, alitoa shukrani hizo jana Machi 15, 2026 wakati wa hafla ya futari ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iliyofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Kitila aliwashukuru wananchi pamoja na viongozi wa dini kwa kumuunga mkono katika safari yake ya kisiasa.

“Masheikh wakiamua kukuunga mkono utajua, na wakiamua kukukataa pia utajua. Mambo yao hayafanyiki chini kwa chini bali hadharani. Nimekuwa mbunge kwa mara ya pili kwa sababu waliniunga mkono tangu mwaka 2020; walinitembeza kata kwa kata bila woga wa kusutwa,” amesema.

Amesema wakati mwingine viongozi wa dini hukumbana na changamoto kwa kuonekana kumuunga mkono mgombea fulani, lakini katika uchaguzi uliopita walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha anapata ushindi.

“Masheikh hawa hawakubaki nyuma; walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha nashinda kwa kishindo. Mwaka 2025 walifanya mara mbili zaidi ndani ya chama na nje ya chama,” amesema.

Amesema anatambua mchango mkubwa wa wananchi na viongozi wa dini katika ushindi wake, akieleza kuwa ana deni la kuwalipa kwa kuwatumikia kwa uadilifu.

“Niombeeni tuweze kuwaongoza wananchi wa imani zote na kuwaletea maendeleo bila ubaguzi wowote,” amesema.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa kituo cha EACLC, Catherine Wang, alisema kituo hicho kinalenga kutoa huduma bora za biashara na usafirishaji kwa wakazi wa Wilaya ya Ubungo na maeneo ya jirani.

Alisema uwepo wa kituo hicho unaongeza thamani ya eneo hilo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Dar es Salaam, huku akiwahimiza wananchi kutumia fursa zilizopo.

“Tukio hili linaonyesha mshikamano wa jamii hauishii kwenye biashara pekee, bali pia katika kukutana na kushiriki matukio muhimu ya kijamii kama haya,” amesema.

Sheikh wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Kibede, amesema mbunge huyo amekuwa na utaratibu wa kufuturisha waumini kila mwaka, tofauti na baadhi ya watu wanaofanya hivyo wakati wa kuelekea uchaguzi.

“Tunahakikisha tunakulinda ili uendelee kuwa mbunge wetu kwa miaka mingi ijayo ikiwa tutakubaliana hivyo,” amesema.

Naye Askofu wa Makanisa ya Ufunuo na Uzima wilayani humo, Paulo Bendera, amesema wilaya hiyo ina viongozi wakubwa serikalini, akiwemo Profesa Kitila pamoja na Mbunge wa Kibamba, Angellah Kairuki, jambo ambalo ni fursa kwa wananchi kushirikiana nao kuharakisha maendeleo.

“Tuwatunze kama tunavyotunza hirizi zetu ili kuhakikisha tunafanikisha mambo yetu na kupiga hatua kimaendeleo,” amesema.