Kero ya mifugo yawatesa wakazi wa Lulanzi, wachukua uamuzi mpya wa ulinzi
Muktasari:
- Wakazi wa Mtaa wa Lulanzi, Kibaha, wamelalamikia wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba yao na kufanya uharibifu, huku baadhi ya wananchi wakidai kushambuliwa wanapowakataza wafugaji hao wananchi wameamua kuunda vikundi vya ulinzi vitakavyofanya doria saa 24, kila kaya ikichangia Sh 2,000 kwa mwezi.
Kibaha, Pwani. Kero ya mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakazi wa Mtaa wa Lulanzi, Manispaa ya Kibaha, imeendelea kuwa tatizo sugu na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wanasema wamechoshwa na uharibifu unaofanywa na wafugaji.
Inadaiwa kuwa baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo kwenye mashamba ya watu na kusababisha hasara, huku ikielezwa kuwa baadhi yao huwavamia wananchi wanapowakataza kuingiza mifugo katika maeneo yao.
Malalamiko hayo yameibuliwa leo Alhamisi, Novemba 20, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye mtaa huo chini ya Mwenyekiti wa Mtaa, Thobias Shilole.
Wakazi waliozungumzia kero hiyo ni pamoja na Hamis Rajabu, Michael Balele na Mauwa Mbwana, ambao wamesema uharibifu huo umekuwa ukiwaathiri kiuchumi na kijamii kwa muda mrefu.
Katika jitihada za kudhibiti hali hiyo, wananchi wamekubaliana kuunda vikundi maalum vya ulinzi vitakavyofanya doria usiku na mchana. Kila kaya itachangia Sh 2,000 kila mwezi ili kufanikisha uendeshaji wa vikundi hivyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Mtaa, Thobias Shilole, aliwataka wakazi kuzingatia maazimio hayo na kuyatekeleza bila kusukumwa.
“Naomba wananchi wenzangu tuwe na umoja, tuwajibike na kusimama kwenye makubaliano tuliyojiwekea. Bila kufanya hivyo hatutaweza kulinda mashamba yetu, mali zetu na usalama wa mtaa wetu kwa ujumla,” amesema Shilole.
Katika mkutano huo wakazi pia walieleza kero nyingine ya watoto kusafiri umbali mrefu kufuata shule, hali inayosababisha wengine kushindwa kuhudhuria masomo mara kwa mara.
Imeelezwa kuwa uongozi wa mtaa, kwa kushirikiana na wananchi, utawasilisha ombi rasmi la mradi wa ujenzi wa shule mpya ili kupunguza changamoto hiyo.