WCF na uboreshaji ustawi wa wafanyakazi Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan akikagua miche kwa ajili ya wakulima wa kati na wadogo wakati wa maonesho ya Kizimkazi yaliyofanyika Kusini Unguja, Zanzibar. WCF ilichangia katika upatikanaji wa miche hiyo.
Kwa kuwa ajenda ya ufunguaji nchi kiuchumi ya Dk Samia inahitaji wafanyakazi wenye mazingira bora ya kufanyia kazi, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umekuwa ukibeba majukumu hayo magumu kwenye mabega yake kuhakikisha azma hiyo ya Rais inafanikiwa.
Katika miaka minne ya uongozi wa Rais Dk Samia, zipo hatua kubwa za kimaendeleo zimepigwa na Mfuko huo ambazo zinahitaji kusherehekewa katika kipindi hiki.
Gazeti la hili limefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Mfuko huo ndani ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita. Na haya yalikuwa ni sehemu ya majibu yake:-
Swali: Kwa ufupi tuelezee kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF): Historia, malengo na majukumu ya kuanzishwa kwake
Dk Mduma: Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263]. Lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huu ni kushughulikia masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.
Majukumu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni pamoja na kusajili waajiri waliopo katika sekta ya umma na binafsi; kufanya tathmini ya mazingira hatarishi mahali pa kazi; kukusanya na kupokea michango kutoka kwa waajiri; Kuwekeza fedha za ziada zilizopo; kulipa fidia; kutunza kumbukumbu za matukio ya ajali, magonjwa na vifo mahali pa kazi; kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi; na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi.
Swali: Mfuko una manufaa gani kwa wafanyakazi?
Dk Mduma: Manufaa ya Mfuko wa Fidia ni pamoja na kutoa huduma ya matibabu; malipo ya ulemavu wa muda; malipo ya ulemavu wa kudumu; malipo kwa anayemhudumia mgonjwa; huduma za utengemao; msaada wa mazishi; na malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.

Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Bi. Mary Maganga akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk John Mduma Cheti cha Ithibati ya Utoaji wa Huduma Bora kwa Viwango vya Kimataifa (ISO Certification) katika hafla iliyofanyika Agosti, 2025 jijini Dar es Salaam.
Swali: Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka minne madarakani hivi sasa. Uongozi wake umesaidiaje Mfuko kiutendaji? Na, je, kuna fursa zipi za kuendelea kukua chini ya utawala wake wa awamu ya kwanza unaoelekea ukingoni?
Dk Mduma: Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, WCF imekua na kuimarika katika maeneo mbalimbali:
a) Kiasi cha fidia kinacholipwa kwa mwaka kimeongezeka kutoka Sh 13.19 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh 25.95 bilioni mwaka 2024.
b) Serikali ya awamu ya sita imefanya maboresho katika mfumo wa fidia kwa wafanyakazi ambapo imepunguza kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.5 ya mapato ya kila mwezi ya mfanyakazi. Hatua hii imewezesha waajiri wengi wa sekta binafsi kumudu kulipa michango hiyo kikamilifu na kwa wakati. Hatua hii pia inaenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya Serikali yetu kuvutia uwekezaji katika sekta binafsi.
c) Aidha, Serikali ya awamu ya sita imepunguza kiwango cha riba inatokana na ucheleweshaji wa michango kwa waajiri kutoka asilimia 10 hadi asilimia 2 kwa mwezi.
d) Serikali ya awamu ya sita pia imefuta malimbikizo ya madeni kwa waajiri waliokuwa wamechelewesha michango ya kila mwezi.
e) Chini ya Serikali ya awamu ya sita, mapato ya uwekezaji kwa WCF yameongezeka kutoka Sh 69.86 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh 88.56 bilioni mwaka 2024.
f) Thamani ya WCF imeongezeka kutoka Sh 445.33 bilioni mwezi Juni 2021 hadi kufikia Sh 747.92 bilioni mwezi Desemba, 2024.
g) WCF imejenga mifumo ya kutoa huduma ambapo takribani asilimia 90 ya huduma zake zote zinatolewa kwa njia ya mifumo ya TEHAMA ikiwemo huduma za usajili wa wanachama, uwasilishaji wa michango ya wanachama, utoaji wa taarifa za madai, n.k.
h) Hali ya uhimilivu wa Mfuko kuimarika. Taarifa ya uendelevu na uhimilivu wa Mfuko iliyofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2022 inaonesha WCF ni himilivu na endelevu kwa kipindi cha miaka 30 ijayo.
i) WCF imetambuliwa kimataifa na kutumiwa kama mfano wa kuigwa ambapo nchi za Kenya na Zambia wamefika kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya fidia kwa wafanyakazi.
j) Kutokana na ubora katika utoaji wa huduma zake, WCF imekabidhiwa Cheti cha Ithibati ya Utoaji wa Huduma Bora kwa Viwango vya Kimataifa (ISO Certification) mwezi Juni, 2024. Hatua hii inawaongezea wadau wetu imani chanya kuhusu uimara wa Taasisi hii.
Swali: Mifuko mingi hushindwa kuwa endelevu kutokana na kushindwa kusimamia ukusanyaji michango kutoka kwa waajiri kupelekea ukata wa mifuko na kushindwa kujiendesha. Je, mmechanga karata zenu vizuri kwa kiasi gani kwenye hili?
Dk Mduma: Mfuko umejipanga vyema kuhakikisha unakuwa endelevu kwa kuweka mifumo thabiti ya kutambua waajiri wote nchini kuhakikisha wanasajiliwa na kuwasilisha michango yao ya kila mwezi.
Ili haya yafanikiwe, WCF imewekeza katika mifumo iliyounganishwa na Taasisi nyingine za umma zinazohusika na waajiri, wafanyakazi, biashara, manunuzi, kodi na utambulisho wa wananchi.
Mifumo hii husaidia kuhakiki idadi ya waajiri, idadi ya wafanyakazi na viwango vyao vya mishahara hivyo kuwezesha WCF kukusanya kiwango sahihi cha michango kila mwezi.

Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa nne kutoka kulia) mara baada ya kuzindua rasmi Maadhimisho ya Miaka Kumi ya WCF katika hafla iliyofanyika Machi 4, 2024 jijini Dodoma. Kilele cha Maadhimisho hayo ni Juni 23, 2025.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa WCF inakuwa endelevu na himilivu, Mfuko unafanya uwekezaji salama na wenye tija kwa kuzingatia Sera yake ya Uwekezaji na Miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania.
Swali: WCF inachangiaje katika kukuza Pato la Taifa?
Dk Mduma: Uwepo wa WCF unatoa uhakika kwa waajiri kuendelea na uzalishaji na kuliacha jukumu la kushughulikia ajali au magonjwa yanayotokana na kazi kwa Mfuko.
Aidha, WCF inachangia katika pato la Taifa kwa kulinda nguvu kazi ya nchi kwa kuhakikisha wafanyakazi wanaopata madhila yatokanayo na kazi wanapata huduma bora za matibabu na utengamao ili waweze kupona haraka na kurudi katika kutekeleza majukumu ya uzalishaji.
Swali: Fursa zilizopo kwa WCF katika kuweka mazingira wezeshi ya kuwakaribisha na kuwavutia wawekezaji?
Dk Mduma: Wawekezaji ili waende kuwekeza katika nchi, pamoja na mambo mengine, huangalia uwepo wa mifumo ya fidia kwa wafanyakazi kwa kuwa mifumo hii huwapunguzia waajiri gharama pale wafanyakazi wanapopata ajali ama magonjwa yanayotokana na kazi. Hivyo, uwepo wa WCF ambayo inakidhi viwango vya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ni kivutio kimojawapo cha wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Swali: Ni changamoto gani ambazo Mfuko umekuwa ukikabiliana nazo tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake?
Mduma: WCF imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo baadhi ya waajiri kutojisajili na kuwasilisha michango yao kwa wakati na hivyo kuathiri utekelezaji wa malengo ya Mfuko na Serikali kwa ujumla.
Pia, kumekuwa na uelewa mdogo kwa baadhi ya wanufaika na umma kwa ujumla kuhusu uwepo wa WCF, mafao yanayotolewa na vigezo vinavyotumika katika utoaji wa mafao husika hivyo kuwafanya wadau hao kuwa na mategemeo yasiyo halisia.
Kama hiyo haitoshi, wapo baadhi ya waajiri wanashindwa kuwasilisha kwa wakati taarifa za matukio mbalimbali ya ajali, magojwa na vifo vitokanavyo na kazi hivyo kuathiri upatikanaji wa haki ya fidia kwa walengwa kwa wakati.
Swali: Ni ipi mikakati ya Mfuko katika kukabiliana na changamoto, ili makala hizi ziwe chachu kwa kampuni na taasisi nyingi zaidi kujiunga na WCF?
Dk Mduma: Mikakati ya WCF ni pamoja na:
a. Kuendelea kujenga mifumo rafiki ya utoaji huduma kwa njia ya mtandao ambayo inaweza kutumiwa na waajiri na wafanyakazi wa ngazi mbalimbali.
b. Kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wafanyakazi na waajiri ili waelewe umuhimu wa uwepo wa WCF, huduma /mafao yanayotolewa na namna ya kupata mafao hayo.
c. Kuendelea kuhimiza waajiri watekeleze kwa hiari wajibu wao chini ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 ikiwa ni pamoja na kujisajili, kulipa michango kwa wakati na kutoa taarifa za ajali ama magonjwa yatokanayo na kazi kwa wakati