Tunaiangazia kesho yetu tukiwa na imani tunaposherehekea Siku ya Mtakatifu Patrick

Waziri wa Nchi wa Ireland kutoka Idara ya Mambo ya Nje na Biashara, Neale Richmond (kulia), Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dk Pindi Chana (kushoto) katika picha ya pamoja wakati wa sherehe za mapokezi ya Siku ya Mtakatifu Patrick.
Machi 17 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Mtakatifu Patrick, Sikukuu ya Kitaifa ya Ireland.
Hii ni siku inayowahusu mamilioni ya watu wenye asili ya Ireland duniani kote kusherehekea mambo yote ambayo yanaifanya Ireland iwe ya kipekee sana - fasihi yetu, muziki, utamaduni, historia na mtazamo wetu juu ya maisha.
Kwa sisi tulio Tanzania, mwaka huu una mvuto wa kipekee tukiwa tunaadhimisha miaka 45 ya uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Tunatazamia kuimarisha ushirikiano wetu katika miaka ijayo, wakati Tanzania inapojidhaatiti kufikia Dira yake adhimu ya 2050. Hii ni pamoja na kuwekeza kwa watu, hususan kwa wanawake na wasichana, kama msingi muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.
Neale Richmond, Waziri wa Nchi wa Ireland katika Idara ya Mambo ya Nje na Biashara, alitupa heshima ya kufanya ziara yake hapa nchini kujumuika nasi kuadhimisha sikukuu yetu ya kitaifa. Alikutana na mawaziri wa Serikali, na washirika wengi katika sekta ya biashara na maendeleo.
Tunaposherehekea, tunajua pia kwamba sababu za kushereheka haziko kwa wingi kila mahali mwezi huu wa Machi. Migogoro inaendelea kuharibu maisha ya watu duniani kote, ikiwamo ile inayoendelea katika nchi jirani ya DRC. Athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaonekana kwa njia nyingi na tofauti.
Ingawa hatuko salama kutokana na changamoto hizi za kidunia, sisi kama ilivyo kwa watu wengine, tunajitahidi kujaribu kuzishughulikia na kupunguza athari zake.

Waziri wa Nchi wa Ireland kutoka Idara ya Mambo ya Nje na Biashara, Neale Richmond (wa saba kulia),Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan (wa tano kushoto )na wafanyakazi wa bandari katika picha ya pamoja baada ya ziara yake katika Bandari ya Dar es Salaam wiki iliyopita.
Na kuhusu wawekezaji nchini Ireland na wageni wanaotembelea kisiwa chetu, tumejipanga kuwa na utaratibu wenye mwendelezo mzuri ambao unakabaliana na changamoto za nyakati zilizopo.
Pia ahadi yetu ya kutaka kuifanya Ireland kuwa ukanda muhimu wa biashara na kama mahali pazuri pa kutembelea, kusoma au kufanya kazi inabebwa kama ajenda kuu ya vyama vyote vikuu vya kisiasa katika bunge letu.
Mfano mzuri wa ahadi hii ya muda mrefu ni programu ya IrishFellows (Marafiki wa Ireland) ambayo ina zaidi ya miaka 50, na mwaka wa 2024 ilitoa nafasi 14 za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kusoma kozi za uzamili nchini Ireland.
Ireland ni mahali pazuri pa kufanya biashara pia. Zaidi ya makampuni 1,800 yanayomilikiwa na wageni yamechagua Ireland kama kituo chao cha kimkakati barani Ulaya na sasa yanaajiri zaidi ya watu 300,000. Tuna nia ya kupanua wigo wetu wa kiuchumi nchini Tanzania na tunafanya kazi na washirika wengi kufanya hivyo.
Tunajaribu kutengeneza utaratibu wa wazi na thabiti kwa sera yetu ya mambo ya nje pia, kulingana na misingi ya ukarimu na ushirikiano.
Katika nyakati hizi ngumu na zinazotia mashaka ndizo muhimu zaidi kukabiliana nazo kwanza, Ireland imeendelea kuunga mkono jumuiya ya kimataifa, ikiwamo Umoja wa Mataifa (UN). Lengo letu kuu ni kuwafikia wale walioachwa nyuma zaidi.
Mchango wa Ireland katika Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA) umeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni.

Waziri wa Nchi wa Ireland kutoka Idara ya Mambo ya Nje na Biashara, Neale Richmond (kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mabalozi wa Programu ya Femina Hip ya Vijana alipotembelea Kituo cha Afya cha Mikanjuni kilichopo mkoani Tanga.
mwaka 2025, uchangiaji katika Mpango wa Msaada wa Maendeleo wa Kimataifa wa Ireland utaongezeka tena hadi kufikia €810 milioni, kiwango chetu cha juu zaidi kuwahi kutokea.
Pia tunajivunia kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa Ireland na msaada wetu umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 15 tangu 2022 hadi kufikia zaidi ya €25 milioni mwaka huu.
Kama nchi ndogo, tuna hakika kwamba kufanya kazi nje ya mipaka yetu, katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, ndiyo njia bora ya kukabiliana na changamoto za kimataifa na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Tunaona ulinzi na uendelezaji wa haki za binadamu kama nyenzo muhimu katika kulinda na kudumisha amani na utulivu duniani kote.
Nchini Tanzania, hili linafikiwa kupitia ushirikiano wetu wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wale wanaojihusisha na masuala ya usawa wa kijinsia na kuimarisha jamii za pwani zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na uchumi wao.
Hii pia ni sababu mojawapo kwa nini Ireland inagombea nafasi ya uchaguzi katika Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kwa muhula wa 2027-2029. Tutachukua hatua kama hiyo kwenye G20 pia, ambapo Ireland imealikwa kushiriki kama mwangalizi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha 2025.
Kazi hii yote inaendelea huku tukiimarisha mipango yetu ya kuwania nafasi ya Urais wa wa Baraza la Umoja wa Ulaya katika nusu ya pili ya 2026.
Ireland ni nchi mwanachama wa kujivunia wa Umoja wa Ulaya, na nchini Tanzania, Ireland inachangia Miradi ya Timu ya Ulaya kuhusu mabadiliko ya hali ya tabianchi na uchumi wa buluu.
Kwa maneno ya Waziri Richmond: “Tanzania ni mshirika muhimu wa Ireland. Ireland, tunaendelea kuwa imara katika ushirikiano wetu na Tanzania na tutashirikiana na washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Serikali, kuchangia ukuaji na ustawi wa Tanzania na kuwalinda wanajamii walio hatarini zaidi.
Kuna msemo maarufu wa Ireland unaosomeka "Ní neart go cur le chéile - Hakuna nguvu bila umoja."
Jinsi tunavyosherehekea Siku ya Mtakatifu Patrick, vivyo hivyo tunapaswa kujitolea kuimarisha ushirikiano wetu tunapofanya kazi pamoja kufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi. Watu wetu wa Ireland na raia wa Tanzania wanastahili kilicho bora zaidi.