Siku 100 za Yas: Ubunifu, tuzo na huduma bora kwa Watanzania

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (katikati) akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa chapa ya Yas jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Novemba 6, mwaka jana, Kampuni ya Mawasiliano Yas (zamani Tigo) ilifanya mabadiliko makubwa ya chapa zake. Kampuni hii ambayo ilianza kutoa huduma nchini Tanzania miongo mitatu iliyopita kwa jina la Mobitel, ilibadilisha jina lake kuwa Tigo, na sasa jina jipya la Yas linatumika katika mataifa matano ya Afrika ambapo inatoa huduma.
Mbali na kubadilika kwa chapa ya kampuni, pia jina la huduma zake za kifedha kwa njia ya simu za mkononi ambalo awali lilijulikana kama Tigo Pesa, ilibadilika na kuwa Mixx by Yas. Huu ni mchakato wa kawaida katika biashara lakini una umuhimu mkubwa katika maendeleo ya kampuni na biashara kwa ujumla.
Katika uzinduzi wa jina hili jipya, uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa alielezea mabadiliko haya kama hatua muhimu kuelekea ujumuishwaji wa kifedha na kidijitali kwa Watanzania.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Yas, Isack Nchunda akizungumza kuhusu mafanikio ya siku 100 za chapa za Yas na Mixx by Yas tangu kufanyika kwa mabadiliko ya chapa hizo.
Mabadiliko haya ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya Axian Telecom Group ambayo ni kampuni mama ya Yas. Mabadiliko haya sio tu yamefanyika Tanzania, bali ni mpango wa Axian Telecom Group kuhakikisha kampuni zake tanzu kote Afrika zina jina moja lenye nguvu na linaloendana na maono ya kampuni.
Kwa Yas, mabadiliko haya yanaonyesha dhamira ya kampuni ya kuleta mabadiliko ya kisasa katika sekta ya kidijitali na kifedha. Ni njia ya kuimarisha biashara na kuongeza wigo wa huduma kwa wateja. Ingawa kuna changamoto zinazohusiana na mabadiliko haya, manufaa yake ni mengi na yanachangia ukuaji wa biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Katika siku 100 tangu Yas na Mixx by Yas kubadilisha chapa kutoka Tigo na Tigo Pesa, tumeshuhudia mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano. Kampuni ya Yas imelenga kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa za kidijitali na za kifedha zilizopo hapa Tanzania.
Akizungumzia siku 100 za Yas, Afisa Mkuu wa Biashara wa Yas, Isaac Nchunda anasema kuwa katika kipindi hiki cha siku 100 za kwanza tangu kufanya mabadiliko ya chapa, kimekuwa kipindi cha mafanikio makubwa kwa wateja na washirika wa Yas na Mixx.
“Yas na Mixx ni kampuni yenye lengo la kumuwezesha kila Mtanzania kunufaika na fursa za kidijitali. Vile vile, tunataka kutambulika kama wabia kwa kila mdau wetu,” anasema Nchunda.
Anasema: “Mimi kama Afisa Mkuu wa Biashara, kila nikiamka ninawaza ni jinsi gani tunawezesha Watanzania kunufaika na fursa zilizopo kwenye ulimwengu wa kidijitali popote walipo. Hilo ndio lengo letu kama chapa, hayo ndio maono yetu.”
Anaongeza kuwa: “Katika siku 100 za Yas na Mixx, tunatambua kuwa tusingefanikiwa kwa kiasi tulichofanikiwa bila wateja wetu na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano ambao wamekuwa nasi kuanzia siku ya kwanza tulivyozitambulisha chapa zetu za Yas na Mixx.”
Mafanikio ya siku 100
Mafanikio ya siku 100 za Yas ni pamoja na kubadilisha maisha ya Watanzania zaidi ya 1,300 kupitia promosheni ya Magift ya Kugift ambapo, wateja na washirika wa kibiashara wamepatiwa zawadi zenye thamani mbalimbali.
“Tumetoa magari mawili mapya aina ya KIA Sorento ambayo hayajatumika kabisa (kilomita sifuri), zaidi ya Sh 840 milioni zimetolewa kwa wateja na washirika wetu huku simu janja zaidi ya 540 zikinyakuliwa na washindi mbalimbali,” anasema Nchunda.
Hii ni sehemu ya dhamira ya dhati ya Yas ya kuwashukuru wateja wake na kuendelea kuwapa thamani zaidi kupitia huduma bora na promosheni za kipekee.
Yas imewekeza kwenye teknolojia za kisasa zinazowezesha upatikanaji wa mtandao wenye ubora na wa kasi zaidi. Vile vile, imeboresha huduma zake za Mixx kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinapatikana wakati wowote bila kujali maeneo mteja alipo.
Lengo ni kuwawezesha Watanzania kutumia fursa za kidijitali kwa urahisi zaidi iwe kwa mteja mmoja mmoja au makampuni/biashara.
Tuzo kedekede
Katika kipindi kifupi cha siku 100, Yas imeendelea kuthibitisha ubora wake kwa kushinda tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
YAS imenyakua tuzo ya Mtandao Wenye Kasi Zaidi Tanzania kwa miaka miwili mfululizo kutoka kampuni ya Kimataifa ya Ookla. Ripoti za robo mwaka za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zimeitaja Yas kuwa Mtandao Bora mara tatu mfululizo.
Pia, katika vipindi tofauti, kampuni hiyo imetajwa kama Mtoa Huduma Bora wa Intaneti Tanzania, Kampuni Yenye Teknolojia Endelevu za Tehama zenye Ufanisi wa Nishati, Mshindi wa Pili – Matumizi Bora ya Tehama kwenye Elimu (eShools Project), Mshindi wa Kwanza – Mlipaji Kodi Mkubwa wa mwaka (Ushuru wa Forodha) na Mshindi wa Kwanza – Kampuni inayozingatia misingi na kanuni bora za Ukusanyaji wa Ushuru wa Forodha.
Tuzo hizi zinadhihirisha dhamira yake ya kuwa kinara wa sekta ya mawasiliano Tanzania kwa ubora wa huduma na mchango katika maendeleo ya Taifa.
Ushirikiano wa kimkakati kufikisha huduma za kibunifu popote Tanzania
Katika siku hizi 100 za mwanzo, Yas imeingia kwenye makubaliano ya kimkakati ili kufikisha huduma za kibunifu kwa Watanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya ITHUBA ambao ni waendeshaji rasmi wa jukwaa la Bahati Nasibu ya Taifa.
“Ushirikiano wetu umejikita kwenye kutumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha kuwa Watanzania wanafurahia michezo ya kubahatisha popote pale walipo.”
“Tumeshirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuwezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja kwenye uwekezaji kwa kutumia teknolojia iliyorahisishwa na yenye usalama zaidi,” anasema Nchunda.
Hitimisho
Katika siku 100 za kwanza, Yas imeleta mabadiliko makubwa kwa wateja wake, imeimarisha huduma zake, imejizolea tuzo muhimu zinazothibitisha kuwa wao ni vinara wa sekta ya mawasiliano, na inashirikiana na wadau wa sekta mbalimbali kuhakikisha kuwa teknolojia inatumika ipasavyo kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali hapa Tanzania.
“Huu ni mwanzo tu – tunaahidi kuendelea kuboresha huduma zetu ili kuzidi matarajio ya wateja kila siku kwa sababu huu ni wakati wetu,” anahitimisha Nchunda.