Ripoti ya kampuni ya Carbon Tanzania yaonyesha maendeleo makubwa katika jamii kutokana na faida za miradi ya hewa ukaa

Zahanati ya Mpembe iliyopo katika Milima ya Ntakata.
Muktasari:
- TSh 9.4 Bilioni (Dola za Marekani 3.7Millioni) zimepokelewa na jamii na vijiji vilivyoko kwenye miradi kwa mwaka 2024.
- ‘REFLECT for Nature’, yafanya tathmini ya faida ya miradi na kugundua manufaa makubwa kwa jamii
- Mradi wa Makame Savannah waonyesha faida mara kumi zaidi kwenye kila uwekezaji uliofanyika
Juni 23, 2025 Carbon Tanzania ilizindua ripoti yake ya mwaka 2024, ikionyesha faida kubwa kwenye miradi yake ya kulinda misitu kwa jamii, bioanuwai na mazingira nchini. Lengo kuu la ripoti hii ni kuelezea jukumu muhimu la Ufuatiliaji, Kuripoti na Uthibitishaji (MRV) wa kijamii katika kuelewa na kuimarisha manufaa ya utunzaji wa misitu na mazingira kwa ulimwengu na jamii.
Ripoti hii inasisitiza dhamira ya Carbon Tanzania ya "kusikiliza kwa ukaribu zaidi na kujifunza kutoka kwa washirika wetu miradini." Hili limefaniikiwa kupitia mbinu bunifu ya REFLECT for Nature (RfN) ya tathmini ya faida za kijamii, ambayo inakusanya mitazamo ya jamii kuhusu jinsi mapato ya hewa ukaa yanavyonufaisha maisha yao na uhusiano na misitu wanayoilinda.
"Falsafa yetu kuu haijabadilika: watu ndio kiini hasa cha hadithi hii ya uhifadhi," wanasema Marc na Jo, Waanzilishi Wenza wa Carbon Tanzania. "Ripoti ya mwaka 2024, hususani kupitia kufanya kazi na REFLECT for Nature, imetuwezesha kufahamu mabadiliko makubwa ambayo yanaeleza faida na kuhakikisha kuwa hatusababishi madhara huku tukijenga ubia wenye usawa."
Matokeo ya ripoti ya mwaka 2024 yaonyesha manufaa makubwa kwa jamii
Utoaji wa fedha: Carbon Tanzania imeelekeza zaidi ya Sh 9.4 bilioni (Dola za Marekani 3.7M) kwenda kwenye baadhi ya jamii kwa mwaka 2024. Fedha hizi zimesaidia kuboresha huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na miundombinu huku manufaa mengine yakionekana katika ulinzi wa wanyamapori na mazingira.

Shule ya Msingi Makame iliyopo eneo la Makame Savannah.
Mabadiliko yanayoongozwa na jamii katika eneo la Makame: Tathmini iliyofanywa na REFLECT for Nature katika mradi wa Makame Savannah ulionyesha uwiano thabiti wa kijamii, kiutawala na maono ya pamoja. Tathmini hii ikiongozwa na jamii yenyewe, wamegundua mradi huu unaleta mabadiliko makubwa, ukikadiriwa kurudisha thamani ya kijamii mara 10 zaidi (1:10), na thamani kamili ya kijamii ikiwa Dola za Kimarekani 6,727,659 kupatikana, kulingana na tathmini za mwaka 2024 zilizofanywa kwa kushirikisha jamii husika kulingana na kiasi cha fedha zilizopatikana.
Ikiwa Elimu ni kipaumbele: Katika eneo la Makame, asilimia 94 ya jamii wanathamini sana elimu ya watoto wao na hivyo, kuweka kipaumbele kwenye mapato yatokanayo na hewa ukaa katika ujenzi wa madarasa na mabweni, pamoja na ufadhili kwa wanafunzi hadi elimu ya juu. Katika miradi yote, ada za wanafunzi 72 wa vyuo vikuu zililipwa, na watoto 9,840 wa eneo la Makame sasa wanafaidika na upatikanaji bora wa elimu kupitia miundombinu mipya na ufadhili.
Kuimarisha usalama wa ardhi na kupunguza mzigo wa kiuchumi: Ripoti ya mwaka 2024 inathibitisha jinsi jamii zinavyoweka ulinzi mathubuti unaotokana na uwezeshwaji kutoka kwenye fedha zitokanazo na mapato ya mradi kwenye maeneo yao. Wanakijiji wanaweza kuripoti shughuli zinazotiliwa shaka kwa walinzi wa uhifadhi (VGS), ambao wanafanya doria katika maeneo yaliyohifadhiwa ili kupunguza uvamizi na ujangili. Hii imeboresha malisho ya mifugo na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama kwa wananchi wengi wa jamii za Kimasai.
Kuwezesha wanawake: Mikakati ya uwezeshaji wanawake inapewa kipaumbele kikubwa, huku wanawake 64 wakifanya kazi kama walinzi wa uhifadhi; takriban asilimia 20 ya walinzi wote (VGS). Pia wanawake 183 wakiwa wanachama wa benki ya jamii ya uhifadhi (COCOBA) katika mradi wa Milima ya Ntakata, inayojumuisha asilimia 53 ya wanachama wote wa COCOBA.
Tathmini iliyofanywa kwenye mradi wa Makame umeonyesha kuwepo kwa viwango sawa vya umiliki wa mali kati ya wanawake na wanaume, jambo linalosaidia kupunguza changamoto za kijinsia na kuleta maendeleo chanya katika harakati za kupigania usawa wa kijinsia.
Uwazi na uwajibikaji: Katika eneo la Makame, asilimia 82 ya wanajamii waliohojiwa wamesema kuwa mradi wa hewa ukaa unasimamiwa kwa uwazi. Carbon Tanzania inatumia kikamilifu taarifa ya RfN kutoka eneo la Eyasi (mradi wa Yaeda-Eyasi), ijapokuwa asilimia 64 ya wanajamii walieleza kutokushirikishwa katika kufanya maamuzi kwenye mchakato wa kuboresha taratibu za ushiriki na ushirikishwaji.
Ajira na ukuaji wa uchumi: Utekelezaji wa mradi uliwezesha kutoa ajira kwa watu 448, wakiwemo VGS 325 (ongezeko la asilimia 15 kutoka mwaka 2023) na mabalozi 96 wa hewa ukaa (ongezeko la asilimia 533). Vikundi vya COCOBA, vikichochewa na fedha za hewa ukaa, vimetoa mikopo midogo iliyosaidia kukuza uchumi na kuboresha maisha, ikiwa ni pamoja na kuboresha makazi, ikiwemo kuhama kutoka nyumba za nyasi hadi za matofali.

Ngo’mbe dume wapya kwa ajili ya wafugaji wa eneo la Makame Savannah.
Dhamira ya Carbon Tanzania katika kuandaa na kutekeleza miradi yake inaenda mbali zaidi hadi kutumia vigezo vya uthibitisho na uhakiki chini ya taasisi ya kimataifa ya Verra, VM0048, ambayo imekidhi vigezo na Kanuni za Msingi vya Hewa Ukaa (CCP) na Baraza la Uadilifu la Soko la Hiari la Hewa Ukaa (ICVCM). Matumizi ya vigezo hivi yameimarisha uadilifu, uwazi na imani ya soko na hivyo kuhakikisha kwamba viumbe hai na jamii zinaendelea kunufaika na miradi hiyo chini ya viwango vinavyotambulika kimataifa.
Ripoti ya mwaka 2024 ni uthibitisho wa kweli kwamba jamii inapopewa mamlaka na haki miliki ya ardhi yao na kushiriki kikamilifu katika usimamizi na manufaa ya kifedha ya uhifadhi wa misitu, huleta maboresho makubwa na yanayopimika katika maisha yao, maendeleo, na kuboresha mifumo ya ikolojia wanayoilinda.
Ushirikiano na wadau, Serikali pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs)
Carbon Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano katika kufikia malengo ya uhifadhi endelevu. Kampuni imejenga mahusiano thabiti na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya uhifadhi nchini na kimataifa. Ushirikiano huu unajumuisha kubadilishana utaalamu, kushirikiana katika utafiti na ufuatiliaji, na kuunganisha nguvu katika utekelezaji wa miradi.
Kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi zisizo za kiserikali kama vile Honeyguide, Community Wildlife Management Area Consortia (CWMAC), World Wide Fund for Nature (WWF), The Nature Conservancy (TNC), Wildlife Management Areas (WMAs), Ujamaa Community Resource Team (UCRT) na halmashauri za wilaya, Carbon Tanzania inaweza kufikia maeneo makubwa zaidi, kuongeza ufanisi wa programu zake, na kuhakikisha kwamba juhudi za uhifadhi zinakuwa na matokeo makubwa na ya kudumu kwa jamii na mazingira.
Kuhusu Carbon Tanzania
Carbon Tanzania ni kampuni ya kitanzania ambayo inachangia katika kukuza uchumi wa nchi na watu wake kwa kutunza misitu asili na viumbe hai kupitia uuzaji wa vyeti vya hewa ukaa iliyookolewa na kuwawezesha watanzania kupata mapato kutokana na uhifadhi wa mazingira yao.
Vyeti hivi hununuliwa na mashirika mbali mbali ndani ya nchi pamoja na kimataifa yenye malengo na mikakati chanya ya kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa kuwekeza katika shughuli za uhifadhi zinazochochea na kuleta matokeo bora katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, jamii na wanyamapori nchini.
Here is the link to the Impact report https://carbontanzania.com/wp-content/uploads/2025/06/impact-report-2024-web.pdf