GGML: Kinara wa maendeleo endelevu ya mazingira Tanzania

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Kasamwa, Diana Magayane (aliyeketi katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na mwakilishi kutoka GGML pamoja na wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Kasamwa wakati wa mdahalo wa shule ulioandaliwa na GGML kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani 2025 chini ya kaulimbiu “Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki,” Kampuni ya Geita Gold Mine Limited (GGML), ambayo ni kampuni tanzu ya AngloGold Ashanti, inathibitisha upya dhamira yake madhubuti ya kulinda mazingira, kusimamia miradi uendelevu na uchimbaji madini usioharibu mazingira hapa Tanzania.
Wakati huu ambao dunia inasisitiza kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira, GGML inaonyesha mfano bora wa jinsi uchimbaji wa kisasa wa madini unavyoweza kuyatunza mazingira badala ya kuyaharibu.
Kampuni ya madini inayolinda mazingira
Siku ya Mazingira Duniani ni wito wa kimataifa wa kulinda dunia tunayoishi. Kwa GGML, kaulimbiu ya mwaka huu ina maana kubwa.

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Kasamwa, Diana Magayane, akipanda mti katika Shule ya Sekondari Kasamwa wakati wa mdahalo wa shule ulioandaliwa na GGML kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
“Tunaliangalia jambo hili kama fursa muhimu. Matumizi ya plastiki ni changamoto iliyo wazi, lakini pia ni nafasi ya kuchukua hatua. Tumejikita katika misingi ya uchumi endelevu ambao unalenga kupunguza taka, kurejesha taka kuwa malighafi mpya zinazoweza kutumika tena, na kusaidia jamii kuwa safi na endelevu.”
Kupambana na changamoto zilizopo za mazingira
GGML inafanya kazi katika Mkoa wa Geita, ambako inakabiliana na changamoto za kimazingira ambazo kampuni nyingi za madini huziepuka.
Kampuni hiyo inakabiliana na ukataji miti ovyo unaosababishwa na shughuli za kibinadamu; uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za uchimbaji madini na taka za mijini; inapunguza matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja kwa kushirikiana na wadau wa ndani; inalinda vyanzo vya maji vya asili na kuhamasisha uhifadhi wake na kusaidia jamii na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia programu za upandaji miti na uelimishaji. Haya ni sehemu ya mkakati wa kisayansi uliojikita kusaidia jamii.
Upandaji miti
Mojawapo ya miradi yenye mchango mkubwa ya GGML ni mradi wa kupanda miti, ambapo maelfu ya miti asilia hupandwa kila mwaka. Hili huambatana na urejeshaji wa ardhi katika maeneo yaliyochimbwa, ambako miti na uoto wa asili hurudishwa kwa lengo la kuhuisha tena viumbe hai na kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Maji pia ni kipaumbele kikubwa. GGML imewekeza katika mitambo ya kisasa ya kutibu maji machafu, kuhakikisha maji yanayorudi kwenye mazingira kutoka migodini yanakidhi viwango vya Tanzania na vya kimataifa.
Mbali na hayo, mgodi umepunguza utegemezi wa vyanzo vya maji safi kwa kuchakata na kutumia tena maji kutoka kwenye mabwawa ya akiba ya matope ya machimbo (Tailings Storage Facility – TSF).
Na mambo haya hayaishii hapo. Vifaa vya kutenganisha taka vimewekwa katika mgodi na maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Geita ili kusaidia usimamizi bora wa taka, hususan plastiki. Kujitoa huku kumeifanya GGML kuwa kampuni kinara katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira.
Ubunifu na miradi endelevu
Ili kupunguza athari kwenye mazingira, GGML imeamua kujikita kwenye ubunifu. Mgodi sasa umeunganishwa na gridi ya Taifa ya umeme wa Tanzania, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya majenereta ya dizeli na hivyo kupunguza hewa ya ukaa.
Aidha, GGML inatumia mifumo ya kidijitali kufuatilia uchafuzi wa hewa, maji, na kelele, kitu kinachowezesha hatua za haraka na uboreshaji wa mara kwa mara.

Mwanafunzi akitoa maoni wakati wa mdahalo wa mashule ulioandaliwa na GGML kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.
Eneo jingine lililofanyiwa mageuzi ni udhibiti wa taka kwa njia ya kidijitali, hususan plastiki na taka hatarishi. Hii huongeza uwazi na kuruhusu kampuni kuboresha mbinu zake za usimamizi wa taka, hivyo kupunguza hatari kwa watu na mazingira.
Uwekezaji katika jamii
Miradi endelevu ya mazingira ya GGML haishii ndani ya mgodi pekee. Kampuni inaamini kwamba mabadiliko ya kweli huanzia kwa watu, hivyo imewekeza sana katika kuelimisha jamii.
Shule, vikundi vya wanawake, na vyama vya vijana hushirikishwa katika mafunzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi, usimamizi wa taka, na uhifadhi wa mazingira.
Mfano mzuri ni Mradi wa Vitalu vya Miti ya Kupandwa, ambapo wanajamii huwezeshwa kukuza miche ya miti inayotumika baadaye kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na uchimbaji madini.
Huu ni ushindi kwa pande zote mbili ambapo vijana hupata huwezeshwa kiuchumi kupitia ajira zinazohusisha utunzaji mazingira na kujenga mazingira yenye afya ya mifumo ya ikolojia kwa vizazi vijavyo.
Jamii zinazopitiwa na bomba la maji kutoka Ziwa Victoria pia zinanufaika na upatikanaji wa maji safi, kupitia uwekezaji wa GGML katika miundombinu endelevu ya maji.
Katika maeneo ya vijijini, programu za kilimo endelevu na kilimo cha miti zinasaidia wakulima kuongeza mavuno huku wakilinda udongo na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Safari ya kujifunza, kujitoa
Licha ya changamoto zilizopo kwenye safari ya GGML kwenye ajenda ya mazingira, kampuni imetambua kwamba ushirikishwaji wa jamii mapema huleta mafanikio, na kwamba maamuzi yanapaswa kuongozwa na sayansi na taarifa (data).
Pia, imejifunza kwamba ushirikiano na Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na taasisi za elimu ni muhimu kwa matokeo ya muda mrefu.
“Tunapoangalia mbele zaidi, GGML haikusudii kushusha mapanga chini kwenye mapambano haya. Tumejipanga kufikia lengo la kimataifa la AngloGold Ashanti la utoaji sifuri wa hewa ya ukaa, kuongeza uwekezaji katika teknolojia rafiki kwa mazingira, kupanua mipango ya kuhifadhi bioanuwai, na kutekeleza mpango wa utunzaji wa maji unaolinda rasilimali hii adhimu,” anasema Dk Kiva Mvungi, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML.
Wito
Kuelekea katika Siku hii ya Mazingira Duniani, GGML inatoa ujumbe wa wazi na muhimu: Dunia haitaki ahadi zaidi, inahitaji maendeleo halisi. Kampuni inawaalika wadau wote, makampuni, jamii, na wananchi, kuchukua hatua muhimu kumaliza uchafuzi wa plastiki na kulinda mazingira yetu ya pamoja.
Tanzania inapoendelea na safari yake ya maendeleo, GGML inabaki kuwa kampuni mfano wa uchimbaji wa madini wenye dhamira ya dhati ambapo ukuaji wa uchumi, ulinzi wa mazingira, na ustawi wa jamii huenda pamoja.