Yanga, Simba zinabebwa na mambo haya

Soka la Tanzania kwa upande wa klabu limetawaliwa zaidi na timu za Simba na Yanga. Hilo lipo wazi kwani hata ukiangalia listi ya mabingwa wa Ligi Kuu utapata jibu lisilokuwa na shaka ndani yake.

Tangu mwaka 1965 ilipoanza ligi hiyo, Yanga na Simba ndiyo timu zinazoongoza kwa kubeba ubingwa mara nyingi Zaidi. Yanga ikiwa kinara kwa kubeba mara 30 na Simba 22.

Inayofuatia ni Mtibwa Sugar iliyobeba mara mbili (1999 na 2000), huku zingine zilizochukua mara moja ni Cosmopolitan (1967), Mseto (1975), Pan Africans (1982), Tukuyu Stars (1986), Coastal Union (1988) na Azam (2013/2014).

Katika mara ambazo timu zimeshindani ubingwa huo, mara nane pekee ndiyo Simba na Yanga hazijawa mabingwa, huku zenyewe zikitawala kwa mara 52. Hii hatari.

Utawala wa Yanga na Simba katika soka la Bongo unabebwa na mambo mengi na hali hiyo inaweza kuendelea kwa miaka mingi ijayo kama mambo yataendelea kuwa hivihivi.

Kitendo cha kuanzia mwaka 2001 hadi 2024 ambapo ni takribani miaka 23 kushuhudia timu hizo zikigawana ubingwa mara 22 huku moja tu ikiachia kwa Azam, inafikirisha na kuonyesha wazi kwamba hakuna ushindani ambao tunautarajia utatokea misimu ya karibuni.

Tazama Ligi Kuu ya Uganda ndani ya miaka hiyo 23 iliyopita ina mabingwa sita tofauti ambao ni SC Villa, Police, URA, KCCA, Vipers na Express.

Kenya kwao ipo hivi; Oserian Fastac, Ulinzi Stars, Sony Sugar, Tusker, Mathare United, Sofapaka na Gormahia. Hiyo ni mifano tu ya ligi za majirani zetu ambazo kwao kuna mabingwa zaidi ya watano katika miaka 23 iliyopita, kwetu wapo watatu pekee huku Yanga na Simba wakibadilishana kwa miaka 22.

Kutokana na hilo, kuna sababu kuu tatu zinazofanya utawala wa Simba na Yanga kuwepo kwa muda mrefu katika soka la Tanzania.


MATAMANIO YA WACHEZAJI

Wachezaji wengi wa Kitanzania wamekuwa na ndoto ya kuzitumikia Simba na Yanga, hiyo inawafanya pale wanapoonyesha viwango bora wakiwa timu nyingine, wanaleta ushawishi wa kusajiliwa na vigogo hivyo na mwisho wa siku dili hufanyika kirahisi.

Mifano ipo mingi lakini kwa kukukumbusha tu ni kwamba, Yanga imeibomoa sana Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti ilipowasajili wachezaji wake muhimu akiwemo Dickson Job, Kibwana Shomari na Aboutwalib Mshery. Leo hii timu hiyo imeshindwa kutoa ushindani mkubwa na kujikuta ikishuka daraja. Pia Simba ilienda hapo na kuwabeba Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim na Shiza Kichuya ambao nao waliwapa mafanikio Msimbazi.

Simba pia ilipoona Azam kuna wachezaji wazuri ambao inaweza kuwasajili na kuwasaidia, ikaenda kuwachomoa Aishi Manula, John Bocco, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni ambao ndani ya misimu minne mfululizo wakawapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufanya vizuri kimataifa. Kumbuka wachezaji hao ndiyo walioipa Azam ubingwa wa ligi waliobeba mara moja.

Msimu wa 2019-2020 Coastal Union ilikuwa na ukuta chuma uliiongozwa na mabeki wa kati, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Ame, ubora wao ukawafanya Simba na Yanga kugawana, Ame akatua Simba na Mwamnyeto Yanga. Leo hii Simba imeenda tena hapo kumchukua Lameki Lawi.

Simba na Yanga zinapohitaji mchezaji kutoka timu nyingine, haitumii nguvu kubwa sana kumshawishi kwani mchezaji mwenyewe ndiye anakuwa na matamanio ya kusajiliwa na timu hizo.

Wapo waliotoboa kwa kufanya vizuri walipotua timu hizo, wengine walienda na kuondoka mapema tu.

Siyo wachezaji wa ndani pekee, bali hata wale wa kimataifa wamekuwa wakitamani sana kuzichezea Simba na Yanga.

Uwezo wa timu hizo kusajili wachezaji wazuri kutoka ndani na nje ya Tanzania umewabeba sana na unaendelea kuwabeba ndiyo maana leo hii unawaona wao wenyewe ndiyo washindani zaidi kulinganisha na wengine.


UWEKEZAJI

Msingi waliouweka Simba na Yanga leo hii ndiyo unawafanya kuendelea kuwa na lundo kubwa la wadhamini. Ukiangalia katika timu za Ligi Kuu zenye wadhamini wengi kutoka makampuni tofauti unazikuta zenyewe. Kuna wakati zote zilikuwa zikidhaminiwa na kampuni moja kabla ya baadaye kila mmoja kuchagua njia yake lakini bado wameendelea kuwa vizuri kiuchumi.

Licha ya kwamba katika hili Azam nayo ipo vizuri katika uwekezaji, lakini mvuto wa Simba na Yanga na ukongwe wao unayafanya makampuni tofauti kwenda kuweka mkono wao hapo katika udhamini na kuzidi kuwapa nguvu ya kuendelea kupambana na wapinzani wao.

Wadhamini hao wanawafanya Simba na Yanga kuwa vizuri kiuchumi na hata ikitokea siku timu hizo zimeyumba kifedha, lakini haziwezi kuwa kwenye hali mbaya zaidi kiasi cha kushindwa kusafiri kwenda kucheza mechi zao, hiyo ndiyo tofauti na timu zingine.


MTAJI WA MASHABIKI

Kuna msemo unaosema kwamba kila Mtanzania unayemuona kama siyo Simba basi ni Yanga, hiyo inatokana na kuonekana timu hizo ni kama vile za urithi tofauti na ilivyo mataifa mengine ambayo watu wake wanashangilia timu kulingana na maeneo zipotokea.

Mfano kwa Dar es Salaam, Simba mashabiki wake wangekuwa watu wa Mtaa wa Msimbazi, Yanga yenyewe pale Jangwani, Azam kule Chamazi ambapo hivi sasa ndiyo makazi yao. Na zile timu za mikoani zingekuwa na mashabiki wao na siyo mashabiki hao kuwa na chembechembe za Simba na Yanga.

Lakini cha ajabu ni kwamba, Simba na Yanga zenye maskani yao Dar es Salaam, zinapokwenda kucheza mechi nje ya mkoa huo jinsi zinavyosepa na kijiji. Mashabiki wanaamua kuziacha timu za mkoani kwao wanawashangilia wageni kitu ambacho kinawafanya kuwa na uhakika wa kupata matokeo mazuri popote pale kwani zinakuwa kama zipo nyumbani muda wote.

Leo hii mikoani kuna matawi ya mashabiki na wanachama wa Simba na Yanga, hiyo inakuwa rahisi kwa timu hizo zinapokwenda kucheza mechi zao huko kuandaliwa mazingira mazuri ya ushindi kwani wanachama na mashabiki wao wapo tayari kuzisaliti timu za nyumbani kwao ili tu wakongwe hao washinde.


MABINGWA WA LIGI KUU TANZANIA KUANZIA 2000 MPAKA SASA

2023-24        Yanga

2022-23        Yanga

2021–22       Yanga

2020–21       Simba

2019-20        Simba

2018–19       Simba

2017–18       Simba

2016–17       Yanga

2015–16       Yanga

2014–15       Yanga

2013–14       Azam

2012–13       Yanga

2011–12       Simba

2010–11       Yanga

2009–10       Simba

2008–09       Yanga

2007–08       Yanga

2007  Simba

2006  Yanga

2005  Yanga

2004  Simba

2003  Simba

2002  Yanga

2001  Simba

2000  Mtibwa Sugar