Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Simba zimefuzu na rekodi kali

Muktasari:

  • Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itachezeshwa Cairo, Misri kati ya Machi 12 au 13 mwaka huu.

Dar es Salaam. Timu za Simba na Yanga zimefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabigwa Afrika kwa pamoja ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.

Simba ilifuzu hatua hiyo juzi, baada ya kuichapa Jwaneng Galaxy mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, huku Yanga ikifanikiwa kufuzu wiki moja nyuma kwa kuifumua CR Belouizdad mabao 4-0, kwenye uwanja huohuo.

Kufuzu kwa timu zote ni historia nyingine ya maendeleo ya soka la Tanzania kwa kuwa ndiyo nchi pekee ambayo imefanikiwa kupeleka timu mbili robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Simba imefuzu ikishika nafasi ya pili kwenye Kundi B, kwa kukusanya pointi tisa, huku Yanga ikipitia kundi D, nayo ikiwa nafasi ya pili kwa pointi nane.

Hata hivyo, timu hizo sasa zinasubiri kufahamu zitakutana nani kwenye droo itakayopangwa Cairo Misri, siku chache zijazo.

Kanuni ya Caf ya hatua ya robo fainali inazizuia timu kutoka nchi moja kukutana, lakini pia timu kutoka kundi moja.

Hivyo, Simba ambayo ilimaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake inaweza kukutana na Mamelodi, Al Ahly au Petro de Luanda ambazo zilimaliza za kwanza, huku Yanga ikiwa na uwezekano wa kukutana na Mamelodi, Asec au Petro.

Kikanuni kwa kuwa Simba na Yanga zimemaliza nafasi ya pili zote zitaanzia michezo yake nyumbani na kwenda kumaliza ugenini.


Mabao ya rekodi:

Timu hizo zimeweka rekodi ya kumaliza hatua ya makundi zikiwa zimefunga mabao mengi zaidi kuliko nyingine zote, baada ya kila moja kufunga mabao tisa.

Zinafuatiwa na Belouizdad, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas ambazo kila moja imefunga mabao saba, Espérance de Tunis imefuzu ikiwa imefunga mabao sita sawa na TP Mazembe.

Kwenye kipengele cha kuruhusu mabao, Petro Atletic ya Angola ipo kileleni ikiwa haijaruhusu bao lolote, ikifuatiwa na Al Ahly na Mamelodi ambazo kila moja imeruhusu bao moja, Simba na TP Mazembe zinafuata zikiwa zimeruhusu mabao mawili.

Esperance de Tunis, imefuzu ikiwa imefungwa matatu, Yanga ndiyo timu iliyofuzu hatua ya robo fainali ikiwa imeruhusu mabao mengi baada ya nyavu zake kutikiswa mara sita.

Timu zilizofungwa mabao mengi zaidi ni Medeama kutoka Kundi D ambalo ipo Yanga mabao 12, sawa na Jwaneng Galaxy kutoka kundi B, ambalo ipo Simba.


Zimeshinda mbili na kufuzu:

Rekodi nyingine ambayo imewekwa na timu hizo mbili ndiyo pekee ambazo zimeshinda michezo miwili tu ya hatua ya makundi, lakini zikapenya kwenda robo fainali.

Simba ilishinda nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca 2-0 na Jwaneng Galaxy mabao 6-0, huku Yanga ikishinda dhidi ya CR Belouazdad 4-0 na Medeama 3-0.

Kwenye timu zote zilizofuzu hizi ndiyo zimeshinda michezo michache na kufuzu, Mamelodi Sundowns ndiyo pekee imeshinda michezo minne kwenye hatua ya makundi.

Petro de Luanda, Al Ahly, Espérance de Tunis, Asec Mimosas na TP Mazembe zimekwenda robo zikiwa zimeshinda michezo mitatu kila moja.


Saido, Pacome ana kwa ana:

Kwenye takwimu za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ukimtoa Sankara Karamoko, ambaye amehusika kwenye mabao matano na hayupo tena kwenye michuano hiyo,   wachezaji wawili Saido Ntibazonkiza wa Simba na Pacome Zouazoa wa Yanga ndiyo wachezaji waliopo kileleni kwa kutoa pasi za mabao na kufunga.

Pacome amehusika kwenye mabao manne, amefunga matatu na ana asisiti moja, huku Saido akiwa amefunga mabao mawili na kutoa asisiti mbili wakiwa ndiyo wapo kileleni kwa wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi.

Wachezaji wengine wanaofuata hapo ni Kennedy Musonda ambaye ana bao moja na asisiti moja na Stephen Aziz KI amehusika kwenye mabao matatu, amefunga moja na pasi mbili za mabao.

Kwenye kadi pia wamo:

Simba imemaliza hatua ya makundi ikiwa kinara kwa timu zilizozoa kadi nyingi za njano baada ya wachezaji wake kupewa jumla ya kadi 15.

Kinara wa jumla wa kadi kwenye hatua hiyo ni kiungo wa Simba, Sadio Kanoute ambaye ameshapewa kadi nne, anafuata Ibrahim Bacca wa Yanga ambaye ameshapewa kadi tatu huku klabu yake ikiwa na jumla ya kadi tisa katika nafasi ya 14.


Pacome, Chama tena:

Kiungo wa Yanga, Pacome Zouazoa anashika nafasi ya pili kwa wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi za kufunga akiwa nazo 17 nyuma ya Mohammed Chibi wa Pyramids, ambaye ametengeneza nafasi 19 kwa ujumla lakini timu yake imeshindwa kufuzu hatua ya robo fainali.

Anayefuata baada ya Pacome ni Stephen  Aziz Ki ambaye ametengeneza nafasi 14 sawa na Marcelo Allende wa Mamelodi na Salifou Diarrassouba wa Asec Mimosas, kiungo wa Jaredi ametengeneza nafasi 13, Chama anafuata akiwa  ametengeneza nafasi 12, kwenye hatua hiyo.


Kwenye pasi Yanga kama kawaida:

Kwenye hatua ya makundi Mamelodi Sundowns imeshika nafasi ya kwanza kwa timu zinazopiga pasi nyingi kwa mechi moja ikiwa ina wastani wa pasi 491.7 kwa mchezo,  inafuatiwa na Al Ahly 422.8, nafasi ya tatu ni Petro 401.7.

Nafasi ya nne ni Yanga ambayo ina wastani wa pasi 375.2, Simba yenyewe inashika nafasi ya 10, ikiwa na wastani wa pasi 295.7.


Mashuti yaliyolenga lango Yanga ipo:

Mamelodi inaongoza kwa wastani wa mashuti yaliyolenga lango ikiwa na wastani wa 5.2, nafasi ya pili inashikwa na Yanga ina wastani wa 5.2, huku Simba ikiwa nafasi ya nne na wastani wa 4.3, nyuma ya Al Ahly yenye 4.8.