Yanga na deni la miaka 55 Ethiopia

Muktasari:
- Msimu uliopita, Yanga iliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 3-2
Dar es Salaam. Ushindi wa Yanga ugenini dhidi ya CBE ya Ethiopia leo kwenye mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika utaifanya ilipe deni la miaka 55 ambalo inadaiwa nchini humo tangu 1969.
Yanga ina kibarua cha kuhitimisha historia isiyofurahisha ambayo imekuwa nayo ndani ya ardhi ya Ethiopia kwani haijawahi kupata ushindi katika mechi nne za mashindano ya klabu Afrika ambazo imewahi kucheza nchini humo.
Katika mechi hizo nne za nyuma ambazo Yanga ilicheza ikiwa ugenini huko Ethiopia dhidi ya timu za huko kuanzia 1969 hadi leo, ilitoka sare mara mbili na kupoteza michezo miwili.
Mwaka 1969 ilitoka sare tasa na St. George, 1998 ikatoka sare ya mabao 2-2 na Coffee na mwaka 2011 ikafungwa mabao 2-0 na Dedebit kisha mwaka 2018 ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Welayta Dicha.
Hata hivyo, Yanga ina historia nzuri dhidi ya timu za Ethiopia kwani katika awamu nne tofauti za mtoano ilizowahi kukutana nazo, ilisonga mbele mara tatu na ilitolewa mara moja.
Kwenye mechi nane ambazo Yanga imekutana na timu za Ethiopia, imeibuka na ushindi mara tatu, kupoteza mbili na kutoka sare tatu.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi hiyo ingawa watacheza kwa tahadhari kubwa katika mechi hiyo huku akisema kuwa atawakosa Nickson Kibabage pamoja na Farid Musa kwa sababu tofauti.
"Kibabage hatutokuwa naye kwa vile ana matatizo ya kifamilia amefiwa na baba yake na Farid Musa anauguza majeraha yake. Tuna habari nzuri hata hivyo ya Yao (Attohoula) kufanya mazoezi na timu.
"CBE ni timu nzuri na hatuwezi kuidharau. Jambo la muhimu ni kuhakikisha tunakuwa bora kwa kuzingatia kile tulichojiandaa nacho ili tuweze kufanya vizuri," alisema Gamondi.
Ushindi wa ugenini kwa Yanga leo, utaiweka katika mazingira mazuri ya kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Yanga inasaka tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo msimu uliopita pamoja na mwaka 1999.
Kitendo cha kutinga tu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kinaihakikishia timu kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.8 bilioni) kutoka shirikisho la mpira wa miguu Afrika (Caf).