Yanga: Hatuihofii Mamelodi Sundowns

Muktasari:

  • Mtine ni mmoja kati ya watu wanaolijua soka la Afrika kutokana na kufanya kazi kwenye timu kubwa zilizoshiriki michuano mbalimbali mikubwa.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andrew Mtine amesema hawaiogopi Mamelodi Sundowns waliyopangwa nayo kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akisema wanaweza kufuzu nusu fainali.

Mtine ni mmoja kati ya watu wanaolijua soka la Afrika kutokana na kufanya kazi kwenye timu kubwa zilizoshiriki michuano mbalimbali mikubwa.

"Lazima tujiamini kwamba tunaweza kusonga mbele na wachezaji pia wajitolee kwa asilimia mia kupambana kwa ajili ya timu. Pia mashabiki nao wawe nyuma yetu kutusapoti," amesema.

"Tunaiheshimu Mamelodi kwa ukubwa wao na mafanikio waliyoyapata, lakini hatuwezi kusema tunakwenda kucheza nao tukiwa wanyonge. Itakuwa ni mechi kubwa, acha tuone nini kitatokea."

Ikiwa itashinda mchezo huo utakaopigwa Machi 28/29, Yanga itakutana na mshindi kati ya Asec Mimosas au Esperance de Tunis.

Msimu huu Mamelodi imeanza vizuri kwenye michuano ya kimataifa ikifanikiwa kuchukua ubingwa African Football League, mbele ya Al Ahly ambayo imepangwa kuchezwa na Simba.

Mechi za mkondo wa kwanza zitapigwa kati ya Machi 29-31 na kurudiana kati ya Aprili 5-7, 2024. Yanga itaanzia nyumbani kwenye mechi hiyo huku ikiwa na kibarua kizito mbele yao cha kumalizia ugenini.

Wakati Yanga ikiwa na kazi ya kufanya kwenye hatua hiyo, mechi nyingine za robo fainali ni kati ya Simba vs Al Ahly, TP Mazembe dhidi ya Petro Atletico na Esperance Sportive de Tunis dhidi ya ASEC Mimosas.


NUSU FAINALI

Esperance/ASEC vs Yanga/Mamelodi

TP Mazembe/Petro Atletico vs Simba/Al Ahly.