Prime
Xavi afichua siri za Elie Mpanzu

Muktasari:
- Simba ilimtambulisha Mpanzu, Septemba 2024 kabla ya kuanza kumtumia mwezi uliopita kupitia dirisha dogo na hadi sasa amecheza mechi sita za Ligi Kuu, dakika 438, amefunga bao moja na asisti moja, huku akijiwekea programu ya mazoezi binafsi kwenye uwanja huo wa Bora.
Kocha anayefundisha mazoezi binafsi, Mohammed Mrishona maarufu kama 'Xavi' amefichua kile anachokifanya kiungo mshambuliaji wa Simba, Ellie Mpanzu anayejifua chini yake kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, akisema atawashangaza kwa mambo mawili anayoyafanya.
Simba ilimtambulisha Mpanzu, Septemba 2024 kabla ya kuanza kumtumia mwezi uliopita kupitia dirisha dogo na hadi sasa amecheza mechi sita za Ligi Kuu, dakika 438, amefunga bao moja na asisti moja, huku akijiwekea programu ya mazoezi binafsi kwenye uwanja huo wa Bora.
Xavi anasema Mpanzu amekuwa akifanya mazoezi anayoamini yatamjenga na kumfanya awe moto zaidi kwani anaonekana ni mchezaji anayejitambua.
Mazoezi anayoyafanya nyota huyo kutoka DR Congo ni ya umaliziaji (kufunga) na ukokotaji mpira mbele ya mabeki, kitu anachoamini kitamfanya kiungo huyo anayetumia miguu yote miwili kuja kutisha mbele ya safari.
Xavi alisema tangu aanze kufanya programu ya mazoezi na Mpanzu ni takribani wiki, kitu alichokiona kwake ni mchezaji anayekwenda na muda, anajituma katika mazoezi na anapenda kurekebisha makosa na kuongeza vitu vipya katika majukumu yake.
"Mpanzu ni mchezaji asiyependa kisingizio katika mazoezi yake, mfano ratiba ya Ligi Kuu inabana, anaweza akapata nafasi ndogo saa 12:00 jioni anakupigia simu ili mkafanye mazoezi, wakati mwingine tunaweza tukamaliza programu yetu, lakini bado unamkuta anajiongeza kufanya kitu kingine," alisema Xaxi na kuongeza;
"Nje na Mpanzu nina mastaa wengi wanaocheza ndani na nje, mfano Maxi Nzengeli nimefanya naye programu ya siku mbili ratiba yake imembana kasema kocha nikiwa tayari nitakwambia."
Kocha huyo ana rekodi ya kuchukua ubingwa akiwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana ya Zanzibar chini ya umri wa miaka 15 katika mashindano ya Cecafa mwaka 2023 na alikuwa msaidizi wa Bakari Shime wakati timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 ya Tanzania ikicheza michuano hiyo(Cecafa).
Baadhi ya mastaa wengine ambao wanafanya mazoezi binafsi na kocha huyo ni Simon Msuva (Al-Talaba SC), Abdi Banda (Dodoma Jiji), Abdallah Shaibu 'Ninja'(Huru), Feisal Salum 'Fei Toto'(Azam FC), Wazir Junior (Dodoma) na Opah Clement (Juárez), Enekia Lunyamila (Mazaltan), Diana Msewa (Trabzonspor) na Joyce Lema wa JKT Queens.