Wikiendi ya moto Premier League

Muktasari:
- leo Jumamosi saa 9:30 alasiri mashabiki wa Ligi Kuu England watashuhudia kipute cha mahasimu wawili wakubwa kwenye ligi hiyo, wakati Everton itakapokuwa nyumbani kukipiga na Liverpool. Mechi ya kibabe kabisa.
LONDON, ENGLAND. NI wikiendi nyingine ya kufosi kwenye Ligi Kuu England, wakati vigogo mbalimbali watakaposhuka uwanjani kusaka pointi tatu muhimu huku macho na masikio ya wengi yataelekezwa huko Goodison Park kutakakopigwa kipute cha Merseyside derby.
Ni hivi, mapema kabisa hii leo Jumamosi saa 9:30 alasiri mashabiki wa Ligi Kuu England watashuhudia kipute cha mahasimu wawili wakubwa kwenye ligi hiyo, wakati Everton itakapokuwa nyumbani kukipiga na Liverpool. Mechi ya kibabe kabisa.
Hiyo itakuwa mechi ya 65 kwa Merseyside derby kwenye Ligi Kuu England, ambapo katika mechi 64 zilizochezwa tayari, mara 25 timu hizo zilitoka sare, huku Everton ikishinda 11, nane nyumbani na tatu ugenini, wakati Liverpool imeonekana kuwa mtawala wa kipute hicho kwa kushinda mara 28, mara 17 nyumbani na 11 ugenini. Kwa takwimu hizo, ina maana Liverpool imeshinda mara nyingi kwenye uwanja wa Goodison Park kuliko wenyeji. Safari hii itakuwaje?
Mchakamchaka wa mikikimikiki hiyo utaendelea, ambapo Aston Villa ya kocha Unai Emery itakuwa nyumbani Villa Park kukipiga na Southampton, huku Newcastle United iliyotibua rekodi ya Liverpool kushinda mechi mfululizo kwenye Ligi Kuu England katikati ya wiki iliyopita, itakuwa ugenini huko Gtech Community kukipiga na Brentford. Ubabe ni mwingi.
Baada ya kumaliza jinamizi la kushindwa kupata ushindi kwenye mechi mfululizo na hatimaye kuwachapa Nottingham Forest 3-0 kwenye mchezo uliopita, jeshi la Manchester City linaloongozwa na kocha Pep Guardiola litakuwa ugenini huko Selhurst Park kukipiga na Crystal Palace katika moja ya mechi inayotazamiwa kuwa na mvuto mkubwa uwanjani.
Kwa mujibu wa takwimu za mechi za Palace na Man City zilipokutana kwenye ligi, kwenye karatasi mambo yanaonekana kuwa mepesi kwa upande wa Guardiola, baada ya kushinda mara 17 katika mechi 28 alizokutana na timu hiyo, huku mechi saba zikilimaliza kwa sare na Palace yenyewe imeshinda nne tu. Katika mechi za ushindi wa Man City, mara nane ilifanya hivyo ikiwamo uwanjani Etihad na tisa kwenye Uwanja wa Selhurst Park inapoenda kucheza leo, huku wenyeji wenyewe kwenye ushindi wao wa jumla wa mechi nne, mbili ilishinda ugenini na mbili nyingine ilipocheza nyumbani. Watatoboa?
Baada ya kuonja kipigo cha kwanza kwenye Ligi Kuu England, kocha Ruben Amorim atakuwa na vijana wake wa Manchester United uwanjani Old Trafford kuwakaribisha Nottingham Forest katika mchezo matata kabisa wa ligi hiyo. Bila shaka, kocha huyo Mreno atahitaji kuirudisha timu hiyo kwenye matokeo ya ushindi ili kuweka hai matumaini yao ya kuwamo kwenye timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi katika mchakamchaka wao wa kufukuzia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Namba zinasoma kwamba, Man United na Forest zimekutana mara 14 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, ambapo katika mechi hizo sare ni mbili tu na Palace imeshinda mbili, moja nyumbani na nyingine ugenini, huku Mashetani Wekundu wakiwa watawala wa mechi hizo, wakishinda 10, sita nyumbani na nne walipokwenda ugenini.
Shughuli nyingine pevu ya mikikimikiki hiyo itaendelea kesho Jumapili, ambapo kutakuwa na mechi kibao za mahasimu wa jiji la London. Kwanza kitakuwa kile kipute cha Fulham na Arsenal kabla ya mashabiki kushuhudia utamu wa Tottenham Hotspur na Chelsea katika mechi muhimu kabisa za kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Huko Craven Cottage, takwimu zinaonyesha kwamba hii itakuwa mechi ya 35 kwa Fulham kumenyana na Arsenal, ambapo katika mechi 34 zilizopita, sare ni saba huku wenyeji Fulham wakishinda nne tu, zote ilipocheza nyumbani kwenye uwanja huo, wakati Arsenal imeshinda 23, mara 11 nyumbani na 12 ilipoifuata Fulham kwao. Kwa takwimu hizo, Arsenal ambayo ipo kwenye msako wa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Balaa jingine la London derby ni Spurs na Chelsea. Hii ni mechi ya kibabe, lakini The Blues wamekuwa na rekodi nzuri, ambapo katika mechi 64 walizokutana kwenye Ligi Kuu England, wameshinda 35, mara 20 nyumbani na 15 ugenini, ambako watakwenda kucheza hiyo kesho. Wenyeji Spurs, kwenye mechi hizo wameshinda nane tu, saba nyumbani na moja ugenini, huku wakali hao wakishindwa kuonyeshana ubabe kwenye mechi 21 zilizomalizika kwa sare. Safari hii itakuwaje?
Mechi nyingine za kesho, Ipswich Town itakuwa nyumbani kucheza na Bournemouth, wakati Ruud van Nistelrooy atakuwa kibaruani kwenye mchezo wake wa pili, ambapo Leicester City itakapokuwa uwanjani King Power kucheza na Brighton.
Takwimu zinaonyesha, kwenye mechi 12 ambazo Leicester imekutana na Brighton kwenye Ligi Kuu England, sare ni nne, lakini vijana wa King Power wakishinda sita, tatu nyumbani na tatu nyingine ugenini, huku Brighton ikishinda mbili tu, tena zote ilipocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani. Brighton haijawahi kushinda King Power. Je, watapindua kibao?
Usiku wa Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu, ambapo West Ham United itakuwa nyumbani kucheza na Wolves.
West Ham na Wolves mechi zake zimekuwa na upinzani mkali kwelikweli, ambapo mara 16 ilizokutana kwenye Ligi Kuu England, sare ni moja, huku West Ham ikishinda nane na Wolves saba. Kwenye mechi hizo, West Ham imeshinda tano nyumbani na tatu ugenini, wakati Wolves imeshinda nne nyumbani na tatu ugenini. Kwenye rekodi hizo, patachimbika.